December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijiji vya Majani Mapana na Kwamwazala kupata maji ya uhakika

Na Yusuph Mussa, Handeni

Wananchi wa vijiji vya Majani Mapana na Kwamwazala katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wana uhakika wa kupata maji safi na salama baada ya Serikali pamoja na Shirika la World Vision kujenga miradi ya maji.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM), Mhandisi Yohana Mgaza wakati akisoma taarifa ya mradi wa maji Majani Mapana mbele ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava wakati alipotembelea mradi huo Aprili 17, 2024.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akimkabidhi ndoo yenye maji mkazi wa kijiji cha Majani Mapana, Mangaiya Julius wakati alipotembelea mradi wa maji Majani Mapana

Mhandisi Mgaza amesema Kijiji cha Majani Mapana ni moja kati ya vijiji vilivyopo katika Kata ya Kabuku ndani katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

Kijiji kilipata ufadhili wa kujengewa mradi wa maji kupitia fedha za UVIKO 19 kwa usimamizi wa HTM,unaotekelezwa na Mkandarasi Saxon Building Contractors Ltd kwa mkataba Na. AE/093/2021-2022/W/01 ulianza Novemba 17, 2021 na ulikamilika Septemba 15, 2022.

Mradi huo unatoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Kijiji cha Majani Mapana wapatao 2,521 ambao umegharimu kiasi cha milioni 395.5 kati ya hizo Serikali Kuu ni milioni 352.4 huku HTM ni milioni 18.1 na Comfort Aid International (uchimbaji wa kisima) ni milioni 20 pamoja na wananchi ni milioni tano.

Kazi zilizopangwa na kutekelezwa katika mradi huu ni pamoja na kuchimba kisima kirefu (borehole), kujenga nyumba ya mitambo katika eneo la Mijohoroni palipo na kisima, kujenga tenki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 katika mnara wa mita sita.

Tenki la maji Mradi wa Majani Mapana

Ujenzi wa vituo tisa vya kuchotea maji katika vitongoji vya Mikoroshini, Misufini, Mkulima,Ujamaa, Kibango na Kwamaluli,kuchimba na kulaza bomba kuu lenye urefu wa mita 2,622 kutoka katika kisima hadi katika tanki la maji.

“Kuchimba na kulaza mabomba ya kusambazia maji yenye urefu wa jumla ya mita 3,777, kufunga pampu ya maji katika kisima kwa ajili ya kusukuma maji kwenda katika tanki, Kufunga mfumo wa nishati ya jua (Solar) kwa ajili ya kuendeshea pampu ya maji na ujenzi wa Valve Chambers 12,” amesema Mhandisi Mgaza.

Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza akionesha michoro ya mradi wa maji Majani Mapana kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava

Akisoma taarifa ya mradi wa maji Kwamwazala mbele ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava kabla ya kuzindua mradi huo Aprili 17, 2024,Meneja wa RUWASA Wilaya ya Handeni Mhandisi Hosea Mwingizi amesema mradi huo umetekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la World Vision Tanzania ambalo liliingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya BCI HOLDING (T) Ltd kujenga miundombinu ya kusambaza maji vitongoji vya Kwamwazala – Mkalamo na Npande – Kwamsisi.

Mradi huo ulianza kutekelezwa Februari 2, 2023 na kukamilika Mei 2, 2023 huku ukigharimu kiasi cha milioni 205.2 pamoja na kodi kutoka kwa Wahisani ambapo hadi kufikia hatua ya ukamilishwaji fedha zote zilitumika kwa kazi za
ichimbaji wa kisima mita 180 kinachozalisha lita 8,800 kwa saa.

Pia ujenzi wa vituo vinne vya
kuchotea maji, ujenzi wa tenki la maji lenye lita 30,000 ujenzi wa nyumba ya mtambo, ufungaji wa pampu ya Solar, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa mabomba kilomita 3.9.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akizindua mradi wa maji Kwamwazala

“Manufaa ya mradi huu ni upatikanaji wa uhakika wa huduma ya maji kwa Wananchi wapatao 1,778 hivyo kuwasaidia kuongeza muda wa uzalishaji mali ili kukuza Uchumi wa nchi na umekabidhiwa Ofisi ya RUWASA Handeni na kwa sasa unaendeshwa na Chombo cha utoaji
huduma ya Maji Kwamsisi-Kwasunga chenye Usajili Na. R-TNG-HD-006″ amesema Mhandisi Mwingizi,”.

Nyumba ya Mitambo (Pump House) Mradi wa Maji Kwamwazala
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Handeni Mhandisi Hosea Mwingizi akisoma taarifa ya mradi wa maji Kwamwazala