January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijiji 192 vilivyobaki Lindi kufikiwa na umeme

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Lindi

NAIBU Waziri wa Nishari Wakili Stephen Byabato amesema, jumla ya vijiji 192 kati ya vijiji 524 vilivyopo mkoani Lindi,vinakwenda kupatiwa huduma ya umeme,baada ya kuzinduliwa kwa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika mkoa wa Lindi.

Naibu Waziri wa Nishati Wakili Stephen Byabato akimkabidhi mama Opeta Sijui Bure kifaa cha UMETA (Umeme Tayari) kwa ajiri ya matumizi ya nyumbani kwake Katoka kijiji cha Narungimbe, wilayani Ruangwa,Lindi alipopokwenda kuzindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili.Mpigapicha Wetu

Ameyasema hayo juzi alipokuwa akifanya uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika kijiji cha Narungombe, Wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Amesema Serikali ya Awamu ya sita inayo azma madhubuti kabisa ya kuhakikisha watanzania wote wanapata umeme kwa ajili ya kufanya shughuli za kijamii pamoja na za kiuchumi na kuwa umeme huo unaletwa na Serikali kwa asilimia mia moja.

Naibu Waziri wa Nishati akiwa ameshikilia utepe kwa ajili ya kuukata na kuzindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili mkoa wa Lindi.

Amewataka wakandarasi kutekeleza mradi huo kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na miradi ambayo serikali inatekeleza kwa ajili yao.

Amewaomba wananchi kutumia fursa hiyo ya kujiunganishia umeme utakapokuwa tayari na kuwa kwa sasa waanze kutandaza nyaya kwenye nyumba zao ili kujiandaa na fursa iliyojitokeza ya kuunganishiwa umeme.

Amewaomba wananchi kuitunza miundombinu ya umeme ili idumu kwa kuacha tabia ya kuchoma moto maeneo yenye nguzo za umeme kwani Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa katika kuweka miundombinu ya umeme kwenye maeneo yao kwa lengo la kuwanufaisha wananchi.

Naibu Waziri Byabato, amewataka watumishi wa TANESCO kuwachukulia hatua wale watakaobainika kuhujumu miundombinu hiyo ya umeme.

Aidha Mh. Byabato, amemuagiza Meneja wa TANESCO mkoa wa Lindi Mha. Kainda Museru Kuhakikisha anahamishia ofisi ya malipo vijijini ili kuwarahisishia na kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda katika ofisi za makao makuu ya mkoa ama wilaya kufanya huduma za malipo.