January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana wazalendo wahamasika kupata mafunzo ya kuendesha mitambo kiwanda cha sukari Mbigiri

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online

UJENZI wa kiwanda cha sukari Mbigiri mkoani Morogoro umeibua fursa kwa vijana wazalendo wa Kitanzania ambao wamehamasika kupata mafunzo ya kuendesha mitambo ya kiwanda hicho kuanzia mwanzo wa ujenzi hadi kitakapokamilika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya vijana waliopata kazi katika ujenzi wa kiwanda hicho, waliishukuru Serikali kwa kupata fursa hiyo ya kujifunza kuendesha mitambo kutoka mwanzo wa ujenzi wa kiwanda chenyewe mpaka wakati wa kufunga mitambo hiyo mpango ambao ni mzuri.

Afisa Utawala wa Kampuni ya BQ Contract Limited,
Joseph Marua amesema kupitia mradi huo wa ujenzi wa kiwanda cha sukari, kampuni yake imeshatoa ajira kwa vijana 60.

Amesema wanaishukuru kampuni ya Mkulazi kwa namna walivyotoa fursa kwa vijana wazawa kuweza kufanya kazi katika mradi huo ambao ni muhimu kwa uchumi wa nchi kwa ujumla.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kushoto) akipata ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Nishati, Medard Kelemani (katikati) kuhusu mpango wa upatikanaji wa umeme katika mradi wa Sukari wa Mbigiri uliopo Mkoani Morogoro alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo wiki hii. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella . Mradi huo unamilikiwa kwa ubia kati ya NSSF na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza. Na mpiga picha wetu.

Marua alisema vijana wanaofanya kazi katika mradi huo wanaifanya kwa moyo mmoja na kwamba mpaka sasa mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho upo katika hatua mzuri na upo ndani ya muda.

Naye, Frenk Nyari ambaye ni miongoni mwa vijana waliopata ajira katika mradi huo, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyousimamia mradi huo ambao umeshatoa ajira kwa vijana.

Amesema vijana wote wanaotekeleza mradi huo ni wazawa na wanafanya kazi kwa moyo mkubwa. Ameongeza kusema kwamba mradi utakuwa umetoa ajira nyingi zaidi baada ya kukamilika.

Kwa upande wake, Jonas Steven, amesema kupitia mradi huo vijana wengi watapata ajira na ameahidi kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili mradi uweze kuleta tija na kutimiza lengo kusudiwa.

Awali, akizungumza na wananchi wakati alipotembelea mradi huo, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, alisema amefarijika kusikia watakaofunga mitambo ya mradi huo kuanzia hatua ya awali mpaka mwisho ni vijana wa Kitanzania.

Waziri Mkuu alisema mara nyingi wamezoea kuona mitambo hiyo inapoletwa nchini inafungwa na watu kutoka nje lakini utaratibu huo wa kuwashirikisha vijana wazawa unasaidia kuwapa ujuzi mkubwa zaidi wa kuendesha kiwanda hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema NSSF na Jeshi la Magereza ndio wamiliki wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi, ambapo kupitia ziara hiyo ya Waziri Mkuu msisitizo aliotoa ni kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kulima miwa na shughuli nyingine ambazo zinaendana na mradi huo ili waweze kunufaika kikamilifu.

Amesisitiza kwamba NSSF na mbia mwenza yaani Jeshi la Magereza wataendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali na kampuni ya Mkulazi ili mradi ukamilike, malengo yaliyokusudiwa yafikiwe na wananchi wafaidike kutokana na matunda ya mradi huu