*Wahimizwa kushiriki kongamano la Tanzania Trade and Logistics Forum 2026
Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online-Dar
WATANZANIA hususani vijana wametakiwa kuchangamkia fursa za kibiashara na uwekezaji kwa kushiriki kongamano la Tanzania Trade and Logistics Forum 2026 , linalolenga kukuza biashara, uwekezaji na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kongamano hilo limeandaliwa na TANFORD, jukwaa rasmi la kuratibu, kuunganisha na kuwakilisha watanzania wanaofanya biashara za cargo, logistics na trade ndani ya UAE, linatarajiwa kufanyika Februari 13 na 14 kjini Dubai kwa lengo la kukuza biashara na ushirikiano kati ya Tanzania na Dubai.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TANFORD, Hussein Jamali, amesema
kongamano hilo litawakutanisha wadau wa biashara, uwekezaji, usafirishaji na uchumi kutoka Tanzania, UAE, Afrika Mashariki, nchi za GCC pamoja na nchi zisizo na bandari (Land Locked Countries).
Amesema kongamano hilo pia litatumika kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania kupitia ushiriki wa taasisi za umma na sekta binafsi.
Jamali amesema miongoni mwa taasisi zitakazoshiriki ni Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), TANTRADE, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA), Zanzibar Investment Promotion Authority (ZIPA) pamoja na taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi.
“Kongamano hili litajenga majukwaa ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika kusaini mikataba, ubia na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, sambamba na kuyaunganisha makampuni ya Cargo, Clearing & Forwarding na Logistics na masoko ya UAE, GCC na Asia,” amesema Jamali.
Ameongeza kuwa kongamano hilo litaweka msukumo maalumu kwa vijana kupitia programu ya Youth Innovation and Business Stage, itakayowapa vijana wabunifu fursa ya kuwasilisha mawazo na miradi yao ya kibiashara mbele ya wawekezaji, hatua inayolenga kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) kutoka UAE kwenda Tanzania.
Aidha amesema yapo manufaa yanayotarajiwa baada ya kongamano hilo ni pamoja na makampuni ya Tanzania kupenya katika masoko ya kimataifa, kuimarika kwa mitandao ya biashara, kufunguliwa kwa fursa za ushirikiano kwa nchi zisizo na bandari zinazotumia Tanzania kama lango la biashara, pamoja na kuboreshwa kwa taswira ya Tanzania kama kitovu cha biashara, utalii na uchumi wa viwanda.
Akitaja mada zitakazojadiliwa, amesema ni pamoja na biashara na masoko ya kimataifa, logistics na supply chain, teknolojia na biashara ya kidijitali, uwekezaji katika viwanda na kilimo, bandari, reli na anga, ufadhili wa biashara na mauzo ya nje, pamoja na ubunifu wa vijana na uwasilishaji wa miradi ya kibiashara (startups pitching).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Wamiliki Malori Tanzania (TATOA), Elias Lukuamay, amewahimiza vijana kutumia kongamano hilo kama fursa ya kukuza biashara zao na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kiuchumi.
Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio, amesema kongamano hilo lina umuhimu mkubwa kwa sekta ya usafirishaji wa mizigo, hasa kwa nchi zisizo na bandari zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la biashara.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi