Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hassan Kabeke,amewaonya vijana wasikubali kushawishiwa na baadhi ya wanasiasa kutumika vibaya kwa kuvuruga amani ya nchi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.
Akizungumza katika sala ya Idd el Fitri iliyofanyika Machi 31,2025 kimkoa katika uwanja wa Nyamagana,Sheikh Kabeke amesisitiza umuhimu wa amani na utulivu kipindi hiki cha uchaguzi, akiwataka Waislamu kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama vya siasa kwa kuwa wanayo sifa ya kuwa raia wa nchi hii.

“Si vyema kusema uchaguzi siyo wetu, kila Mwislamu ni raia wa nchi hii na anayo haki ya kugombea, kuchagua, na kuchaguliwa kama ilivyo kwa raia wengine.”
Ameeleza kuwa vijana wanapoambiwa na viongozi wao wa kisiasa wanapaswa kutafakari kwa makini kabla ya kujiunga na maandamano au shughuli yoyote inayoweza kusababisha machafuko, madhara yake yataathihiri familia zao na jamii kwa ujumla.
“Ni muhimu kwa viongozi wa dini na Watanzania kuungana na kusema ‘hapana’ kwa chama chochote cha siasa kinachovunja amani.Watanzania zaidi ya milioni 60 wengi wao licha ya kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa,bado wana haki ya kushiriki uchaguzi na kuamua mustakabali wa nchi yao,”amesema Kabeke na kuongeza:
“Tumeanza kusikia maneno kwamba tutaleta fujo, uharibifu na kuipasuapasua nchi kwa nguvu ya umma,mtu anayesema hayo tafsiri na maana yake anawaandaa watu waingie barabarani wakafanye maandamano ,”.
Amesema katika hilo hakuna kulemba ni vyema wanasiasa wenye nia hiyo waambiwe ukweli kuwa,nchi zingine amani ilipovurugika mustakabali wao ni hapa nchini,hivyo tunawajibika kuilinda nchi yetu na amani iliyopo.

“Mtume S.A.W anasema kufikiri saa moja ni bora kuliko ibada ya mwaka mzima pia, unapotaka kufanya jambo litazame hadi mwisho ,likiwa la heri fanya na likiwa la shari acha.Amani ni kama yao,ni lulu, ni kama yai likivunjika huwezi kuliungaunga, tutunze amani ya nchi tusikubali ushawishi wa aina yoyote,”amesema.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Baraza la Wazazi Mkoa wa Singida, Ahmed Misanga,amesema mwaka huu wa uchaguzi hategemei vijana kujitoa ufahamu kwa kurubuniwa na wanasiasa wenye malengo ya kuvuruga amani ya nchi.
“Vijana wanategemewa na taifa kujenga uchumi wake, Serikali imeboresha maisha yao na wengi wanafanya kazi,wapo wanaonufaika kwa mikopo asilimia kumi isiyo na riba kutoka Halmashauri ili kujiinua kiuchumi,hivyo wasidanganywe na wana siasa kwenda kuvuruga amani,”amesema.
Misanga amesema mwanasiasa anayewadanganya na kuwahamasisha kuingia mitaani kufanya vurugu,hawawezi kuinuka na familia yake zaidi ya kujificha,ikitokea amepata madhara katika vurugu atatibiwa nje ya nchi .
“Wewe kijana unayehaingaka na kesho yako kwa maisha ya kuunga unga kupitia ujasiriamali utatibiwa kwa gharama kubwa tena kwa kujificha,utakuwa unatafutwa na dola mithili ya mhalifu kwa kufanya vurugu,”amesema.
Misanga amesema wanasiasa wanaohubiri bila mabadiliko hakuna uchaguzi, Tanzania ni kubwa kuliko chochote na watanzania hawaamini katika vurugu,hivyo hawawezi kusikiliza maneno ya chama kimoja kati ya takribani vyama 20 vya siasa.

More Stories
Wataalamu wabobezi katika sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi wakutana nchini
Wizara ya afya yachukua hatua sakata la Mzazi anayedai kubadilishiwa Mtoto Arusha
EWURA yatangaza bei za Mafuta kwa mwezi Aprili 2025