November 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana waliokatiza masomo waendelea kupata fursa

NDOTO ya Modesta Gabriel ya kuwa mhandisi wa majengo ilikwama akiwa Kidato cha Pili mkoani Manyara, baada ya kukumbwa na changamoto za makuzi na kushawishiwa na makundi yasiyofaa yaliyomfanya kupoteza mwelekeo wa masomo. Hata hivyo, kupitia fursa inayotolewa na Serikali chini ya Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), sasa amerejea darasani akiwa na matumaini mapya ya kutimiza ndoto yake.

Mama yake, Rose Barnabas, anakumbuka namna alivyopambana kumsaidia bintiye kurejea katika mstari wa elimu, ikiwemo kutafuta msaada wa vyombo vya dola ili kumwelekeza kubadili mwenendo wake.

Pamoja na juhudi za mama yake kumrejesha shuleni, Modesta hakubadili uamuzi wake na hatimaye akaandika barua ya kuacha masomo.

“Mama yangu alinipeleka Polisi, lakini nilisisitiza kuwa sitaki kuendelea na masomo, nikaandika barua ya kuacha shule” anasimulia Modesta.

Hata hivyo, mama yake hakukata tamaa, aliendelea kumshauri na kumkumbusha umuhimu wa elimu katika kujenga maisha na kufikia malengo yake.

“Hata ungenipa pesa zako zote, bado wewe si bora kwangu, kwa sababu huna elimu,” anakumbuka Modesta akimnukuu mama yake, kauli iliyomchochea kurejea masomoni.

Modesta ameanza safari mpya ya kitaaluma ambapo mwaka huu amefanya mtihani wa hatua ya kwanza inayolingana na Kidato cha Pili, akiwa na azma ya kuendelea na masomo hadi kufikia ndoto yake ya kuwa mhandisi wa majengo.

Rose ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa kutoa fursa nyingine za elimu kwa vijana waliokatiza masomo. Amewasisitiza wazazi kuendelea kuwa karibu na kupigania ndoto za watoto wao.

Kwa upande wake, Mkufunzi Mkazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mkoani Manyara, Mwalimu Emmanuel Deogratius Geidan, amesema vijana waliorejea masomoni, akiwemo Modesta, wanaonesha dhamira na ari ya kutimiza ndoto zao kupitia elimu.

Ameeleza kuwa, kupitia Mradi wa SEQUIP, Serikali imewekeza katika miundombinu na kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuwawezesha vijana hao kuendelea na masomo.