November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, (picha ya Mtandao)

Vijana saba kizimbani wakidaiwa kuingiliana kinyume na maumbile

Na Mwandishi Wetu

VIJANA saba wakazi wa jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 12 ya vitendo vya kuingiliana kinyume na maumbile, huku mfanyabiashara Nkinda Shekalage (34) Mkazi wa Tegeta Wazo akidaiwa kuwaingilia vijana sita kati ya hao.

Mbali na Nkinda, washtakiwa wengine ni Ahmad Mrisho (36) mwanafunzi Mkazi wa Kivule, Gift Emmanuel (20) Mkazi wa Tegeta, Jackson Kiss (20) mwanafunzi mkazi wa Gongo la Mboto, Christopher Songea, (20), Mkazi wa Gongo la Mboto, Salum Kachende (21), mkazi wa Tegeta na Ramadhani Mlekwa, (25), mlinzi Mkazi wa Manzese.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon akisaidiana na Mkude Mshanga alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Huruma Shaidi kuwa, katika shtaka la kwanza hadi la tano mshtakiwa Nkinda kati ya Januari 2017 hadi Machi 2020, kwa nyakati tofauti aliwaingilia washtakiwa wenzake kinyumbe na maumbile. washtakiwa haoni Ahmad, Gift, Jackson, Christopher, Salum

Pia katika shtaka la sita hadi la kumi imedaiwa kuwa, kati ya Januari 2004 hadi Machi 2020 washtakiwa Ahmad, Gift, Jackson, Christopher, Salum walimruhusu mshtakiwa Nkinda kuwaingilia kinyume na maumbile.

Aidha katika shtaka la 11 mshtakiwa Jackson anadaiwa kati ya Januari 2019 na Machi 2020 alimuingilia mshtakiwa, Ramadhani,  huku katika shtaka la 12 mshtakiwa Ramadhani anadaiwa kumuingilia mshtakiwa Jackson.

Hata hivyo, washtakiwa walikana kutenda mashtaka hayo na walirudishwa rumande kwa kuwa Hakimu Huruma Shaidi aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo ana majukumu mengine ya kikazi.

Hivyo washtakiwa hao watasomewa masharti ya dhamana na Hakimu husika tarehe ijayo. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo umekamilika na imepangwa kusomewa maelezo ya awali Mei 5,2020.