January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia masuala ya vijana nchini, (TYC ), Lenin Kazoba, akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu vijana 50 kuweka kambi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kujengewa uwezo katika masuala ya ubunifu,tehama na ujasiriamali. Na mpiga picha wetu.

Vijana 50 kujengewa uwezo mkoani Kilimanjaro

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

TAKRIBANI vijana 50 wanatarajia kuweka kambi ya siku tano mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kujengewa uwezo katika masuala ya ubunifu, teknolojia ya habari na mawasiliano, biashara, ujasiriamali na ushauri.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia masuala ya vijana nchini, (TYC ), Lenin Kazoba amesema leo kuwa kambi hiyo siku tano inatarajiwa kuzinduliwa Agosti kesho na kumalizika Agosti 7,2020.

Amesema vijana hao watapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayokwenda sambamba na Taasisi hiyo ambayo ni uwezeshaji kwa vijana na uwekezaji kwa maendeleo endelevu.

“Wakati dunia ikisubiria maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani Agosti 12 mwaka huu,TYC imeandaa kambi maalum kwa ajili ya vijana ambao watajengewa uwezo katika masuala mbalimbali ikiwemo ubunifu,”amesema na kuongeza;

“Kupitia kambi hiyo vijana watapata fursa ya kuwasilisha mafanikio waliyoyapata hasa katika eneo la uwezeshaji na uwekezaji.”

Amesema kambi hiyo inatarajiwa kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.John Jingu lengo likia ni kuwasaidia vijana kujifunza na kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya ujasiriamali,Tehama na Ubunifu.

Aidha amesema hii ni mara ya tatu kwa TYC,kuandaa kambi maalum kama hiyo ambapo kwa mara ya kwanza ilifanyika mwaka 2018 na ya pili ilikuwa 2019.