November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Victor apania makubwa kitaifa, kimataifa

Na Mwandishi Wetu

MSHINDI wa jumla wa mashindano ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi ‘CDF Trophy Cup 2020’ yaliyoshirikisha nyota zaidi ya 200, Victor Joseph ameahidi kushinda mataji zaidi katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Nyota huyo wa mchezo wa gofu hapa nchini pia ni bingwa mtetezi wa mashindano ya ‘Kenya Amateur Open Golf Championship’ ambapo aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Mchezaji huyo amesema kuwa, ndoto yake kubwa ni kuendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yaliyo mbele yake ili kuendelea kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali.

Amesema, ushindi wa jumla alioupata kwenye CDF Trophy Cup 2020 unampa hamasa zaidi ya kufanya mazoezi ili kuendelea kufanya vizuri na kujikusanyia mataji zaidi.

“Ubingwa huu nilioupata unanipa hamasa zaidi ya kufanya mazoezi kwani nimefikia hapa kwa ajili ya kujituma hivyo
nitaendelea kupambana zaidi kutwaa mataji makubwa na kuiletea heshima nchi yangu, ” amesema Victor.

Kuhusu mashindano ya Kenya Open, nyota huyo amesema kuwa, baada ya mashindano hayo kusogezwa tena mbele kutoka Novemba hadi mwakani, sasa hivi anaendelea na mazoezi kujiandaa na mashindano yoyote yatakayokuja mbele yake.

Awali mashindano ya Kenya Open yanayotambulika dunia nzima yalipangwa kufanyika Machi 12 hadi 15 lakini yaliahirishwa kutokana na mlipuko wa maambikizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona ambavyo hadi sasa bado vinaendelea kulitesa Taifa hilo.

Mashindano hayo yaliahirishwa wakati ambao alikuwa amejiandaa vema kwenda kufanya vizuri lakini baada ya kuahirishwa nyota huyo alishiriki mashindano ya gofu ya Tanapa Lugalo Open yaliyofanyika katika Viwanja vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania vya Lugalo Jijini Dar es Salaam na kuchukua ushindi baada ya kupiga mikwaju 153.