Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini Tanzania,imekuja na mbinu ya kutatua changamoto zinazokabili sekta ya Ukarimu na Utalii kwa kuwakutanisha watoa huduma wote wa sekta hiyo jijini Dodoma.
Akizungumza na watoa huduma hao jijini hapa leo,Novemba 29,2024 kwenye Kongamano la Wadau wa Sekta ya Ukarimu na Utalii, Mkuu wa Wilaya ya Bahi,Rebecca Sanga amewataka Vijana wote wanaosomea Sekta Ukarimu na watoa huduma ya ukarimu kwa ujumla Mkoani Dodoma kuhakikisha kuwa wanakuwa waaminifu,Wasafi na Wachangamfu nyakati zote wawapo katika majukumu yao ambapo amesema uaminifu siku zote unalipa.
“Sekta ya Ukarimu ni nguzo muhimu sana katika Mkoa,lakini sekta hii si kwamba inachangia pato la mkoa tu bali linatoa ajira kwa vijana wetu.Serikali ya Mkoa wa Dodoma imeweka usalama wa kutosha hivyo watu wanaweza kutanua biashara kwa kufanya muda wote kwasababu usalama upo na anatarajia kuona Dodoma ikishamiri,”amesema Sanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA Tanzania CPA Anthony Kasore amesema kuwa kwasasa wana vyuo 80 vinavyotoa mafunzo ya Ufundi katika Mikoa yote Nchini, na vipo vyuo 65 vinavyoendelea kujengwa katika mikoa hiyo vinavyojumuisha wilaya 64 lakini matarajio ni kuwa ifikapo mwaka 2025 ni Veta kuwa na jumla ya vyuo 145, ili kuendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuwa kila Mtanzania kuwa na ujuzi kutoka katika vyuo vya ufundi Stadi hapa Nchini.
“Sasa hivi tuna vyuo 80 vinavyotoa mafunzo ya ufundi katika mikoa yote na katika mikoa hiyo ujenzi unaendelea wa vyuo 65 vinavyojumuisha wilaya 64. Na matumaini yetu ni kwamba ifikapo mwaka 2025 Veta tutakuwa na jumla ya vyuo 145 ambavyo vitakuwa ndani ya Mikoa yote na Wilaya zote Nchini”.
Naye Ramadhani Ali Mataka ambaye ni Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati amesema lengo na madhumuni ya kukutana na wadau wa sekta ya Ukarimu na Utalii mkoa wa Dodoma ni kuona namna gani bora ya kutatua changamoto zinazoikabiki sekta hii kwani Dodoma ni mji Mkuu na watu wengi wanaingia kila siku,hivyo ni vema wageni watakapoingia wakakutana na Ukarimu wa hali ya juu,kwani sekta hii imekuwa ikilalamikiwa sana.
Wakati akitoa taarifa ya Chuo cha Veta Dodoma, Mkuu wa chuo hicho Deodatus Orotha amesema kuwa chuo kinaendelea kutoa mafunzo yanayokidhi viwango ili kuendana na soko la Dunia hasa katika Sekta hii ya Ukarimu.
More Stories
Wahitimu waliosoma MNMA washauriwa kutumia kusanyiko kutoa maoni ya kuendeleza chuo
Viongozi wa mitaa Korogwe TC watakiwa kusimamia maendeleo ya wananchi
Mahakama yashindwa kumtia hatiani Dkt.Nawanda