March 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA wapaka rangi jengo la watoto MNH ,wakisherekea miaka 30

Na Penina Malundo,Timesmajira

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeendelea kupiga hatua katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma, baada ya leo kupokea msaada wa rangi wenye thamani ya TZS. 22.3 Mil. kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya VETA tangu ilipoanzishwa.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ambaye alikua mgeni ameeleza kufurahishwa na mabadiliko makubwa yaliyofanyika Muhimbili na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kuboresha huduma za afya nchini.

Kwa upande wake, Dkt. Faraja Chiwanga, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa MNH ameeleza kuwa hospitali hiyo ni kubwa yenye mahitaji mengi yanayohitaji rasilimali nyingi hivyo kupata msaada kutoka VETA na wadau wengine ni jambo muhimu linalopaswa kupongezwa.

Zamani, tulikuwa tunaamini kuwa hospitali ni mahali pa tiba tu, lakini sasa tunajua kuwa mazingira nayo yana mchango mkubwa kwa afya na ustawi wa wagonjwa, hususan watoto, tunapenda hospitali yetu iwe mahali ambapo watoto wanapokuja, wasijisikie kama wako kwenye mazingira ya hofu, bali wajione wako sehemu salama na yenye faraja,” amesema Dkt. Chiwanga.

Naye CPA. Antony Kasore, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Tanzania, ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya dhamira ya VETA ya kurudisha kwa jamii.

“Katika kuadhimisha miaka 30 ya VETA, tuliona ni muhimu kushiriki katika miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Kupaka rangi Jengo la Watoto hapa Muhimbili ni moja ya njia za kuonyesha kuwa kile tunachofundisha kina tija kwa jamii. Tunaamini kuwa mazingira safi na yenye mvuto yanaweza kusaidia watoto waliolazwa kupata ahueni haraka,” amesema Kasore.