Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar
VITENDO vya rushwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa kupata wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) limekuwa donda ndugu la muda mrefu hapa nchini.
Tatizo hilo, limekuwa likisababisha baadhi ya maeneo CCM kupata wagombea wasiokuwa chaguo la wananchi. Mfano, imekuwa ni jambo la kawaida wagombea kuhonga wapiga kura za maoni fedha tasilimu, pombe, kofia, khanga na vitu vingine vidogo vidogo.
Rushwa hizo zimekuwa zikisababisha wapiga kura za maoni, kuwapima wagombea kwa rushwa na sio kwa uwezo wao wa kuwatumikia wananchi. Rushwa hizo ndani ya CCM zimekemewa kwa muda mrefu, lakini watoa rushwa nao wamekuwa wakibadili mbinu.
CCM kupitisha wagombea wasio na sifa baada ya kutoa rushwa na kuongoza kura za maoni, imekuwa sababu za CCM kupoteza majimbo, kata, vijiji na vitongoji kwenye chaguzi.
Na wakati mwingine wana CCM ambao wanaona kwamba wamekosa sifa ya kugombea ndani ya chama hicho kwa sababu ya rushwa ,wamekuwa wakihamia vyama vya upinzani na kushinda.
Lakini sababu nyingine ambayo imekuwa sababu ya CCM kupoteza ushindi, ni vikao vya maamuzi kuwapitisha watu ambao sio chaguo la wananchi.
Pamoja na Katiba ya CCM ya mwaka 1977, toleo la 2012, kukemea vikali vitendo vya kutoa na kupokea rushwa, lakini ambacho Watanzania wamekuwa wakishuhudia katika kura ya maoni, kinafanya wajiulize kama wana CCM hao wanaitii Katiba yao inayokataza ruswa.
Ni muhimu wana CCM wakatambua kwamba siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao, endapo CCM ikipitisha mgombea aliyepenya kwa rushwa, akawa hana sifa ambazo wananchi wanazitaka, atakutana na mgombea wa vyama vingine vya upinzani.
Kwa bahati nzuri, tayari Rais Samia Suluhu Hassan, ameliona hili, na kuweka bayana kwamba wagombea ubunge, udiwani, uwakilishi watapimwa kwa kazi walizozifanya wakati wapo madarakani, wala sio kwa khanga na elfu kumi, kumi wanazotoa kwa wajumbe wanaowapigia kura.
“Kwa wale ambao wapo kimya kiuetendaji waanze sasa kutimiza wajibu wao. Bado kidogo mwaka mmoja hivi na nusu tutaanza kuchujana. Hata na wanaokwenda kuchagua, wawapime wabunge na wawakikilishi wao kwa kazi walizozifanya,” anasema Rais Samia na kuongeza;.
“Hata wapiga kura wasikubali kutembezewa vijikhanga na elfu 10 ndani.”
Rais Samia amekemia rushwa kwa wagombea wa nafasi mbalimbali wakati wa kura za maoni katika kipindi muafaka, wakati nchi yetu ikitarajia kufanya uchaguzi mkuu mwakani.
Rushwa wakati wa kura za maoni imekuwa kilio cha wagombea wengi wa ubunge, udiwani na uwakilishi walioshiriki mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Rais Samia amekemea vitendo hivyo, kwanza kutokana na ukongwe wake ndani ya chama hicho, amekuwa Mjumbe wa Baraza la wawakilishi na Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Lakini pia rushwa anayoikemea ndani ya chama imekuwa moja ya sababu ya chama kupata viongozi wasiokuwa na sifa. Unapofika wakati wa uchaguzi wa ndani kupata wagombea watakaopeperusha bendera ya chama, Wana-CCM wanasahau ahadi namba 4 ya mwanachama wa CCM kulingana na katiba hiyo.
Kwa mujibu wa ahadi hiyo, “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.”
Inapofikia hatua Mwenyekiti wa Chama, Rais Samia anawaambia waziwazi wana CCM kuhusu tabia ya kutoa rushwa ya khanga na elfu kumi, kumi maana yake anawakumbusha kwamba hataki ahadi hiyo ibaki kwenye makaratasi.
Katika nafasi ya ubunge na udiwani, wapo wagombea wenye uwezo wa kifedha waliotoa rushwa hadi sh.20,000 kwa kila mwanachama aliyempigia kura ya maoni.
Lakini, huko nyuma wapo makada waliokula njama na watendaji wa CCM na kupatiwa kadi mpya za wanachama na kuzilipia miaka kadhaa mbele na kuzigawa kwa wapigakura.
Maeneo mengine wajumbe walikutanishwa sehemu moja usiku na kununuliwa pombe. Huko nyuma katika maeneo mengine wapo watu waliopiga kura baada ya kupewa kadi siku hiyo hiyo au siku moja kabla, kadi zikiwa zimeshalipiwa ada.
Ibara ya 39 inayohusu kazi za Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM ya tawi, imebainisha dhahiri kuwa chombo hicho ndicho kitajadili na kutoa mapendekezo ya wanachama wapya.
Sehemu ndogo ya (e) ya katiba hiyo, imefafanua kuwa inapofika siku ya kupiga kura za maoni, chombo hicho ndicho kitahakiki uhalali wa mwanachama wa CCM kwa kila tawi.
Kama sio kuwapo kwa mazingira ya rushwa, inakuwaje watu walipewa kadi za uanachama kiholela bila kujadiliwa na kamati za siasa za tawi na kisha kuruhusiwa kupiga kura ya maoni?.
Pamoja na huko CCM kubadili utaratibu kuhusiana na wanaostahili kupigia kura wagombea ndani ya CCM, badala ya kila mwana CCM mwenye kadi katika eneo husika, bado vitendo vya rushwa ndani ya chama ni tishio, hivyo kauli ya Mwenyekiti wa Chama, Rais Samia, inaleta matumaini mapya ndani ya CCM.
Rais Samia anatambua wazi kwamba wanaoshinda kura za maoni kwa rushwa ndi wanakipa wakati mgumu chama wakati wa kampeni kuwanadi wagombea hao.
Kwa mara kadhaa tumeshuhudia wagombea wa CCM walioshinda kwa kura nyingi, wakizomewa na wananchi wakati wa kuomba kura. Tunajiuliza, iweje mgombea aliyeshinda kwa ushindi wa kimbunga kwenye kura za maoni ndani ya CCM anaposimama jukwaani anazomewa?
Wakati fulani aliyekuwa Mwenyeiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete, aliwahi kusema kuwa kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho, huenda kikaanguka vibaya Uchaguzi Mkuu 2015.
Rais Kikwete alienda mbali zaidi na kuwapasha wanachama wa chama hicho kuwa kama kitanusurika katika uchaguzi huo na kama kitaendekeza rushwa basi hakitapita kwenye Uchaguzi Mkuu 2020.
Kikwete (sasa Rais Mstaafu), alitoa onyo hilo, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa, makatibu na wenyeviti wa wilaya.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika Serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani,” alisema na kuongeza; “Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea sh. 200,000 za muda wa maongezi (airtime), ndugu zangu hatutafika ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema .
Wakati huo, aliendelea kusema kuwa tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho na wanachama linazidi kuwa kubwa kila siku, hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapigakura wao.
Pamoja na Kikwete kutoa ushauuri huo miaka mingi iliyopita, lakini bado watu waliopewa dhamana ya kuogoza wananchi kwenye nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi hawatimizi wajibu wao kikamilifu, wanashindwa kuwaletea maeneo wananchi wakiamini watatoa khanga na shiligi elfu kumi kumi.
Hiyo ni kwa sababu mara baada ya kura za maoni, wagombea wengi huwa wanalalamika wakiwatuhumu wenzao kushinda kwa rushwa.
Kwa msingi huo, kauli ya Rais Samia inaenda kumaliza kilio kikubwa cha rushwa. Ni muhimu wana CCM wakatambua kwamba hata vijana ndani ya CCM wanakerwa na vutendo vya rushwa.
Mfano, aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Kheri James aliwahi kuzitaka Jumuiya za chama hicho kutojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato kuelekea uchaguzi mkuu ili kuhakikisha viongozi watakao patikana wanakuwa bora.
“Kaeni macho na wagombea wanaoibuka katika maeneo yenu wakiomba uwakilishi wa ubunge na udiwani huku wakigawa fedha ili wachaguliwe, waulizeni walikuwa wapi siku zote wakati mlipokuwa mnajinyima, mnahangaika usiku na mchana kukijenga chama na iweje waje sasa,” alisema James.
Alisema wasikubali kununuliwa na fedha badala yake wachague viongozi bora watakao waletea maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano kupitia chama hicho imara chenye kujali maslahi ya wananchi.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia