March 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uzinduzi mpango wa ZERA nchinii waibua fursa kiuchumi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

SERIKALI na wadau wa sekta ya nishati na usafiri, wamesema hatua ya kuanza rasmi kwa matumizi ya magari ya umeme nchini, itafungua ukurasa mpya wa matumizi ya nishati safi, kupunguza gharama za uendeshaji wa usafiri, kuimarisha uchumi wa taifa na kuzalisha fursa za ajira kwa Watanzania.

Hatua hiyo imetokana na kampuni ya ZERA kuzindua magari yake ya umeme, yanayolenga kutoa suluhisho la usafiri wa magari ya umeme nchini.

Hafla hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, aliyekuwa mgeni rasmi, amesema mageuzi ya usafiri wa magari ya umeme ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuongeza matumizi yenye tija ya umeme na kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje.

Amesema Tanzania inaendelea kupanua uzalishaji na upatikanaji wa umeme, hivyo sekta ya usafiri wa umeme ni fursa muhimu ya kuongeza matumizi ya nishati hiyo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Magari ya umeme siyo mtindo wa muda mfupi, bali ni mwelekeo wa kimkakati unaoweza kusaidia kupunguza gharama za usafiri, kuimarisha mazingira na kufungua fursa za ajira kupitia viwanda na teknolojia mpya,” amesema.

Kwa mujibu wa tafiti za United Nations Environment Programme (UNEP), matumizi ya usafiri wa umeme yanapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji.

Tathmini iliyowahi kufanywa nchini, imeonesha gharama za usafirishaji wa mizigo kwa pikipiki ya petroli ni takribani sh.31,000 kwa siku, huku pikipiki ya umeme ni sh.3,000 pekee.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ZERA, Emmanuel Kazimoto, amesema kampuni hiyo inalenga kujenga mfumo kamili wa usafiri wa umeme unaojumuisha uuzaji wa magari, ufungaji wa miundombinu ya kuchaji, ushauri wa kubadilisha magari ya kampuni kuwa ya umeme, pamoja na huduma za matengenezo.

Ameeleza mpango wao utaanza kwa kuingiza nchini magari ya kampuni hiyo ya ZERA yaliyokamilika (CBU), kisha hatua ya pili italenga kuingiza yaliyoandaliwa nusu (SDU) ili kuongeza ushiriki wa wataalamu wa ndani, huku hatua ya tatu ikilenga kuanzisha mkusanyiko wa magari hayo hapa nchini.

Katika hatua za mwanzo, kampuni hiyo imeingiza magari kadhaa ya umeme kwa ajili ya maonesho na matumizi ya majaribio, ikiwa ni pamoja na yale ya abiria na mabasi madogo yanayoweza kutumika katika usafiri wa mijini.
Mpango huo pia unatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika masuala ya nishati na miundombinu ya kuchaji.