November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWT yatakiwa kushikamana kuiwezesha CCM kushinda kwenye chaguzi

Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Shinyanga


WANACHAMA wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wameshauriwa kuondoa tofauti zao na kushikamana pamoja ili kukiwezesha Chama cha Mapinduzi (CCM) kuibuka na ushindi mkubwa katika chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.


Ushauri huo umetolewa na mmoja wa Wabunge wa Vitimaalum mkoani Shinyanga, Santiel Kirumba katika mkutano maalumu wa wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT Mkoa kutoka wilaya za Shinyanga mjini na Vijijini.

Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa, Christina Gule akiwahutubia wajumbe wa mkutano maalum wa UWT katika ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga.


Santiel amesema Jumuiya ya Wanawake Tanzania ni miongoni mwa Jumuiya muhimu za Chama cha Mapinduzi (CCM) na moja ya majukumu yake ni kukitafutia ushindi mkubwa chama hicho vipindi vya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Amesema wanawake nchini ni kundi kubwa hivyo likijipanga na kusimama imara Chama Cha Mapinduzi lazima kiibuke na ushindi wa kishindo iwe katika chaguzi za Serikali za Mitaa ama uchaguzi mkuu.


“Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi tusipokuwa na mtaji wa kutosha, mtaji wa nchi yoyote ni mwanamke, kwa sababu mwanamke kila kitu kinamgusa,Rais Samia Suluhu Hassan lazima ashinde kwa kishindo, lazima tumheshimishe, heshima ile tunaijenga sisi UWT, kwa sababu yeye ni zao letu,”amesema.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT Mkoa kutoka wilaya za Shinyanga Mjini na Vijijini wakifuatilia mkutano.


Amefafanua kuwa iwapo wanawake wote watashikamana na kuachana na makundi miongoni mwao hakuna kitakachoshindikana na kwamba uchaguzi wa mwaka 2025 siyo mgumu kama wengi wanavyofirikia, kwa sababu aliyepo madarakani kwa sasa ni mwanamke mwenzao.


“UWT lazima tusimame kidete, tujuwe ni wanawake wangapi watakaotia nia ya kugombea nafasi mbalimbali kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji, udiwani na ubunge ili tuweze kuwaunga mkono, tuwaandalie namna bora ya kuwasapoti, ili Shinyanga iwe ya tofauti, tumetia nia, tutaweza na Mungu atatusimamia,” ameeleza.


Katika hatua nyingine Mbunge Santiel ametoa msaada wa vyerehani vipatavyo 120 kwa wajumbe wa mkutano wa UWT wa Wilaya za Shinyanga vijijini na mijini ambapo pia kwa wilaya ya Kishapu ametoa vyerehani 76 vyote vikiwa vimegharimu kiasi cha zaidi ya milioni 45.


Akikabidhi vyerehani hivyo kwa walengwa Santiel amesema lengo ni kuwazesha wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT kuwa na kitega uchumi kitakachomsaidia pia kufanya shughuli za Jumuiya na Chama pasipo matatizo mfano gharama za usafiri kwa ajili ya shughuli za utafutaji wanachama wa CCM.


“Najua mna changamoto, Jumuiya tunaombwa kununua kadi, nauli kwa ajili ya kwenda kwenye vikao nimeona niwashike mkono kidogo kwa kuwanunulia vyerehani hivi, cherehani hii unaweza usiitumie wewe lakini utakodisha na kuingiza kipato,ukipata fedha si utaweza kununua kadi kwa ajili ya kutafuta wanachama wa CCM na Jumuiya, lakini pia utapata nauli ya kuja kwenye vikao vya Jumuiya, yaani huu mradi jifanye kama unaenda kukitumikia chama chako, hiki ndicho nilichokiwaza na nikaona niwasaidie, na hii ni kwa nia njema,” ameeleza Santiel.


Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga, Grace Bizuru mbali ya kumshukuru mbunge huyo wa msaada ambao ameutoa lakini pia amewataka wajumbe wa UWT kuachana na makundi na kupanga safu za wagombea kabla ya vipindi vya uchaguzi na kwamba kufanya hivyo ni kinyume na maadili ya chama.


Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa, Christina Gule amewataka wajumbe wote wa UWT kuwathamini wabunge wote watatu wa vitimaalumu walioko katika mkoa wa Shinyanga na wasikubali kugawanywa na kuyumbayumba hali inayoweza kusababisha viongozi wa mkoa kushindwa kutimiza majukumu yao.


Makatibu wa CCM wa wilaya za Shinyanga mjini, Majeshi Ally Majeshi na Shinyanga vijijini Ernestina Richard wamempongeza mbunge Santiel kwa hatua yake ya kuwashika mkono wajumbe wa UWT mkoa na kwamba ni muhimu hivi sasa wanawake wote wajitokeze kugombea kwenye chaguzi za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Wajumbe wakiserebuka mara baada ya kumalizika kwa mkutano maalum wa wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa kutoka wilaya za Shinyanga Mjini na Vijijini.