Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.
MJUMBE wa Baraza kuu la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzani (UWT) Mkoa wa Mara,Rhobi Samwelly ametoa wito kwa Watanzania, kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan za utunzaji wa mazingira.
Rhobi ameyasema hayo kwa nyakati tofauti Juni 3, 2025, wakati akizungumza na Walimu na Wanafunzi wa shule za Sekondari Mwisenge na Sekondari ya Ufundi Musoma (Musoma Technical Secondary School) zilizopo Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.
Ambapo waliambatana na Balozi wa Mazingira nchini ambaye pia ni Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Mara Ahidi Sinene ikiwa ni hatua yao ya kufanya ufuatiliaji wa mazingira,kuangalia ustawi wa miti iliyopandwa na kutoa hamasa ya utunzaji wa mazingira katika kuadhimisha wiki ya mazingira duniani ambayo kwa mwaka huu hapa nchini kauli mbiu inasema ‘Mazingira yetu na Tanzania ijayo tuwajibika sasa, kudhibiti matumizi ya plastiki.
Katika Hotuba yake Rhobi amesema kuwa, Rais Dkt.Samia ameonesha dhamira yake thabiti ya utunzaji wa mazingira nchini na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia Kampeni ya Upandaji Miti ambapo ameendelea kuhamasisha upandaji wa miti kama njia ya kukabiliana na uharibifu wa misitu na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia Rhobi amesema, serikali ya Rais Samia imekuwa ikiboresha mipango ya kitaifa ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa rasilimali maji, kilimo himilivu, na uhifadhi wa maeneo ya ikolojia kwa manufaa endelevu.
“Rais Samia ameonesha nia ya kuendeleza nishati mbadala kama vile jua, upepo. Hii inalenga kupunguza utegemezi wa nishati ya mafuta ambayo huchangia uchafuzi wa mazingira. Na amekuwa akihamasisha ushiriki wa vijana, mashirika ya kiraia, na sekta binafsi katika masuala ya mazingira. Katika hotuba zake nyingi tutaona , anahimiza uwajibikaji wa kila mtu katika kutunza mazingira.” amesema Rhobi.
Hivyo, Rhobi amesema juhudi za utunzaji mazingira zifanywe na watu wote na makundi yote katika Jamii kwani si jukumu la serikali pekee, bali la kila Mtanzania kulifanya kwa ukamilifu kuanzia katika eneo lake anapoishi hadi mazingira ya kazini kwa ubora unaokidhi viwango.
Balozi wa Mazingira nchini Tanzania ambaye pia ni Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mara Ahidi Sinene amesema kuwa serikali ilitoa maelezo ya kuhakikisha kila Halmashauri inapanda miti Mil. 1.5 kwa Kutumia bajeti zao, ambapo amesema kila Halmashauri imetekeleza kwa kiwango chake.
Ameongeza kuwa, “nikiwa Balozi wa mazingira nilipanga kila Halmashauri katika Mkoa wa Mara ipande miti 5,000, ambapo jumla tulifanikiwa kupanda miti 45,000 kwa Halmashauri zote, na miti 10,000, ilikufa kwa sababu mbalimbali na miti 35,000 ilipona. Kwa halmashauri ya Manispaa ya Musoma naHalmashauri ya Wilaya ya Musoma jumla ya miti 25,000 imepona. Niiombe Jamii kushiriki kikamilifu kufanya usafi wa mazingira, kuondosha taka za plastiki sehemu zote na kuachana na shughuli ambazo zina athari kwa mazingira na viumbe hai.” amesema Sinene.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma Magita Nyangore amesema shughuli za utunzaji mazingira shuleni hapo ikiwemo upandaji miti zimeendelea kufanya mazingira kuwa bora, kutopata majanga ya asili kutokana na.uwepo wa miti, hewa safi, kupata mbao ambazo hutumika kutengenezea samani na kwa Sasa wanaelekeza juhudi katika upandaji wa miti ya matunda kuimarisha lishe kwa wanafunzi.




More Stories
Kiongozi wa Mwenge apongeza wananchi kupelekewa huduma ya maji Handeni
TFS yawakaribisha wawekezaji katika vivutio vya utalii wa misitu
Waziri Bashungwa:Tumieni teknolojia za kisasa kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka