February 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwekezaji ufanyike maporomoko ya maji Kalambo

Na Israel Mwaisaka,Rukwa


WAKAZI wa mkoa Rukwa wameiomba serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kufanya uwekezaji wa kutosha kwenye maporomoko ya maji Kalambo ambayo ni ya pili kwa afrika itakayowezesha jamii kunufaika kiuchumi kutokana na maporoko hayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamedai kuwa kulingana na ukubwa wa maporomoko hayo uwekezaji wake umekuwa ni mdogo kiasi kwamba umeshindwa kuwavutia watalii wengi zaidi kwenda kwenye maporomoko hayo ili hari maporomoko hayo ni mazuri na kwa watalii waliofika wamefurahishwa na maporomoko hayo na wengi kusema eneo hilo ni eneo moja zuri sana kiutalii.
Festo Godwin mkazi wa kijiji cha Kapozwa amesema kuwa maporomoko hayo hayajatangazwa vya kutosha lakini pia kutokuwepo na mahoteli makubwa kumekuwa kukiwafanya Watalii wengi kushindwa kwenda kwenye maporomoko hayo na kufurahia utalii huo na kukimbilia mjini Sumbwanga zilipo hotel.
Amesema kuwa vitu hivyo vikiboreshwa vitasaidia hasa vijana na wao kupata shughuli za kufanya kutokana na uwingi wa watalii watakaofika katika maporomoko hayo hayo ambayo ni ya pili kwa Afrika.
Mpoli Philimoni kwa upande wake aliiomba serikali kufanya kila liwezekanalo kuboresha miundo mbinu katika eneo hilo na kuwezesha Watalii wengi kufika ni fursa kwao kufanya shughuli za ujasiliamali ikiwa ni pamoja na kuutangaza hata utamaduni wetu unaopatikana mkoa Rukwa ikiwemo ngoma za kabila la Wafipa .
Afisa utalii wa uhifadhi wa mazingira TFS kalambo , Rose Aloyce amesema kuwa mpaka sasa serikali imefanikiwa kuweka miundo mbinu ya ngazi kuelekea kwenye maporomoko hayo ikiwa ni pamoja na kujenga vibanda vichache vya kupumzikia ikiwemo na mahema imeweza kuongeza idadi ya Watalii kutoka 1000 kwa mwaka hadi kufikia 4500 na kuwa hayo ni mafanikio makubwa,.
Amesema kuwa maporomoko hayo ambayo ni ya pili Afrika yenye urefu wa mita 235 yakitanguliwa na maporomoko ya tugera water falls yenye urefu wa mita 947 ya Afrika kusini, yakifuatiwa na Victoria water falls ya Zimbabwe yenye mita 108 na kuwa mazingira ya Kalambo falls ni mazuri ambayo kama yakiwekezwa vizuri kuna nafasi kubwa ya kuvuna watalii wengi zaidi .
Afisa utamaduni na michezo mkoa Rukwa Adamu Evarist amesema kuwa kazi kubwa ya serikali katika eneo hilo ni la kuhifadhi mazingira na kuhakikisha TFS wanakuwepo eneo hilo na kuwa maporomoko hayo ni sehemu ya maendeleo endelevu ya urithi wa utamaduni usioshikika na kuwa katika kuuendeleza ulithi huo serikali itaendelea kuwekeza katika eneo hilo kama ilivyokwishaanza.
Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la (TAMCODE) chini ya ufadhili wa UNESCO Rose Ngunangwa amesema kuwa shirika hilo linatumia vyombo mbalimbali vya habari kuchagiza malengo endelevu juu ya urithi usioshikika na moja ya eneo ambalo Tamcode wanalifanyia kazi ni Maporomoko hayo ya kalambo falls kwa kubainisha fursa mbalimbali kwa vijana na Wanawake endapo yatajengwa Mahoteli na watalii wengi wakafika watapata fursa ya kuuza bidhaa zao hasa zile za asili zinazopatikana katika mkoa Rukwa.
Amesema eneo hilo la Kalambo ni zuri sana na kuiomba wizara ya maliasili na utalii kuyaona kwa jicho la pekee maporomoko hayo ya Kalambo falls kwani yanaweza kukuza uchumi uchumi wa taifa kwa haraka na vijana na Wanawake kukuza uchumi wao ikiwa na kulinda urithi wetu na kuwa endelevu zaidi katika vizazi vijavyo