January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwekezaji bandari ya Dar-es-Salaam utaongeza fursa za kiuchumi Kahama

Na David John,Timesmajira Online, Kahama

MKURUGENZI wa Manispaa ya Kahama ,Mkoani Shinyanga Anderson Msumba,ameeleza kuwa uwekezaji unaokwenda kuwekezwa katika bandari ya Dar-es-Salaam utaongeza fursa za kiuchumi katika Mji wa Kahama.

Msumba ameyasema hayo wilayani humo katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya Manispaa hiyo yaliyofanyika ofisini kwake,ambapo amesema kuwa baadhi ya nchi zinazotumia bandari ya Dar-es-Salaam njia yao kuu ni Mji wa Kahama.

Pia ameeleza kuwa ni mji ambao unahudumia mikoa ya Kigoma,Geita, Tabora, Kagera kibiashara hivyo ndio maana amesema kupitia uwekezaji unaokwenda kufanyika katika bandari ya Dar es salaam utaongeza fursa katika Mji wa kahama.

“Naiona Kahama inakwenda kuwa kama Dubai na kupitia uwekezaji mkubwa utakaofanyika pale bandari ya Dar-es-Salaam niwazi biashara katika mji wa Kahama itakuwa kubwa,kama mnavyojua kwamba Kahama ni njia kuu kwenye ya nchi za maziwa makuu kwa maana ya Rwanda, Burundi, Drc Congo,na Uganda,”.

Aidha amesema Manispaa hiyo ya Kahama imetenga maeneo makubwa ya uwekezaji na viwanda na mpaka sasa kuna hekari 6000 pia Kuna hekari 2000 Nyashimbi na eneo jingine ni eneo la mgodi wa Buzwagi ambalo linamilikiwa na PANGEA pamoja na maeneo mengine ya uwekezaji kama Zongomela eneo la viwanda na kwingineko.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa Kahama tangu 2017 kupitia mpango mkakati wao wa miaka mitano mitano, wanataka kuona Kahama iwe eneo kubwa la biashara.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Msumba amesema kuwa kwa sasa wamewekeza nguvu kubwa kwenye miundombinu ya elimu,afya na Kwa kiasi fulani waendelea kufanya vyema kama Manispaa wamejipanga vilivyo.Mbali na hayo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumuacha aendelee kuiwakilisha vyema serikali kwa kuwatumikia wananchi wa Manispaa hiyo.

“Wenye sifa wapo wengi na wanafaa kuwa wakurugenzi lakini kwa imani yake Rais Dkt Samia kwangu amendelea kunipa nafasi na mimi naahidi siyomwangusha nitaendelea kuchapa kazi ili kuleta matokeo chanya Kwa wananchi wetu,”amesema Msumba.

Ameongeza kuwa kazi kubwa ya Halmashauri ni ustawi wa wananchi wake huku akisema kuwa Manispaa hiyo ni kubwa sana na inaendelea kukua kwa haraka kila kukicha hivyo kutokana na hali hiyo changamoto zinakuwa ni nyingi lakini amefarijika kubaki Kahama ili yeye pamoja na timu yake watimize ndoto yao ya kuiona Kahama mpya yenye maendeleo makubwa na ya Kasi ya ajabu.

“Mimi Nimefarijika nimebaki Kahama angalau mimi na wenzangu tunataka kuona zile ndoto zinatimia, na kubwa zaidi kuifanya Kahama kuwa kitovu cha biashara,”amesema Msumba.