December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwakilishi wa wanawake katika masomo ya sayansi bado ni changamoto

Na Penina Malundo,TimesMajira, Online

LICHA ya wanawake kupata maendeleo makubwa katika kuongeza ushiriki wao kwenye elimu ya juu bado hawajawakilishwa vizuri katika nyanja za masomo ya sayansi nchini katika fani za Sayansi,Teknolojia,Uhandisi pamoja na Hisabati.

Aidha wadau hao wamesema wanaendelea kuunga mkono Jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan chini ya Serikali yake kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika kukabiliana na pengo la kijinsia katika elimu hususani katika masomo ya sayansi kwa watoto wakike.

Akizungumza hayo juzi jijininDar es Salaam, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Shirika la Stemship ,Eng.Juliana Marko,wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi amesema takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa wanawake wana uwakilishi mdogo katika masomo ya sayansi kuliko kundi la wanaume.

Amesema licha ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya Sita katika miongo ya hivi karibuni elimu ya sayansi bado haipatikani kwa usawa kwa wote huku ukosefu wa usawa wa kijinsia bado unaendelea.

“Wasiwasi Mkubwa katika nchi nyingi sio tu idadi ndogo ya wasichana wanaokwenda shule,lakini pia njia finyu za elimu kwa wale wanapoingia darasani hii inajumuisha zaidi jinsi ya kushughulikia ushiriki hafifu na mafanikio ya kujifunza ya wasichana katika Elimu ya Sayansi, “amesema na kuongeza

“Pengo kubwa la kijinsia limeendelea kuongezeka kwa miaka mingi katika viwango vyote vya taaluma za sayansi, teknolojia, uhandisi na Hisabati (STEM) kote duniani,”amesema

Amesema Shirika la Women Level Up Initiative na Tanzania STERMAship Foundation kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini wamezindua Kampeni ya kuhakikisha watoto wa kike wanaosoma
Masomo ya Sayansi wanaongezeka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Taasisi inayoshughulikia masuala ya Mazingira ijulikanayo kwa jina la Human Dignity and Enviroment Care Foundation (HUDEFA) ,Sara Pima amesema katika kampeni hiyo ya kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya Sayansi wameweza kuzindua kampeni hiyo itakayodumu kwa miaka mitatu 2022-2025.

Amesema kampeni hiyo inalenga kujenga uwezo kwa jamii kuhusu fani za Sayansi,Teknolojia, Uhandisi na Hisabati hivyo kampeni hiyo itakuwa chachu ya kuongeza kasi ya wasichana kupenda masomo hayo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jielimishe Kwanza,Henry Kazula, amesema kampeni hii pia inahamasisha mabinti kutumia Sayansi katika kutatua changamoto zinazowazunguka hasa katika sekta mbalimbali.

Amesema kumekuwa na ushiriki mdogo kwa wanawake na kuwa na dhana kuwa masomo ya sayansi ni magumu na ni ya wanaume hivyo wengi wao kuyaacha.

“Kwa kushirikiana na Mashirika mbalimbali ikiwemo Hudefa,Jielimishe kwanza,Tanzania Stemship pamoja na tumeamua kuungana kupitia kampeni hiyo ili kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko,”amesema