January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UTPC kuhakikisha umma inauelewa juu ya uhuru wa vyombo vya habari

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na klabu zake zote kwa kushirikiana na wadau wengine wanapaswa kuhakikisha kuwa umma unaelewa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa habari.

Kwa kufanya hivyo kutaongeza ufahamu wao juu ya jinsi vyombo vya habari vinavyochangia na kujenga jamii yenye habari na taarifa sahihi na uelewa sahihi.

Hayo yameelezwa na Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo, wakati akifungua mkutano wa siku ya kimataifa ya kukomesha uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari ambayo yamefanyika kwa njia ya mtandao(zoom meeting) ambayo huadhinishwa kila ifikapo Novemba 2 kila mwaka.

Ameeleza kuwa hiyo inaweza kusaidia kuzuia misimamo ya upande mmoja na kupotosha habari hivyo amesisitiza umuhimu wa kuelimisha umma juu ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya waandishi wa habari katika jamii.

Ambapo vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kufichua uhalifu na ufisadi hivyo kuelimisha umma juu ya jinsi waandishi wa habari wanavyochunguza na kuripoti masuala haya kunaweza kusaidia katika kupambana na vitendo hivyo visivyo vya maadili.

“Umma ulioelimishwa unaweza kushiriki zaidi katika mchakato wa kisiasa na kijamii na hivyo kuwa na mchango mzuri sana katika ujenzi wa taifa kwa kuelewa jukumu la waandishi wa habari katika kuchunguza masuala ya umma, umma unaweza kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao,”ameeleza Nsokolo.

Pia ameeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika demokrasia hivyo umma unaoheshimu na kuelewa umuhimu wa vyombo vya habari huru unaweza kuchangia katika kudumisha demokrasia thabiti kwa kushiriki kwa ufahamu katika mchakato wa uchaguzi na kutoa maoni kuhusu sera na masuala ya umma, ambayo ni muhimu katika ujenzi wa taifa.

Aidha ameeleza kuwa vyombo vya habari vina jukumu la kuchunguza na kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Kuelimisha umma kuhusu jinsi vyombo vya habari vinaweza kusaidia kugundua na kusimamia haki za binadamu kunaweza kusaidia katika kuzuia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu,”ameeleza Nsokolo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko ameeleza kuwa inapaswa kuwa na sheria inayomlinda mwandishi wa habari moja kwa moja ambayo ipo tofauti na Rai wa kawaida kwani ni kundi maalumu katika kufanya kazi.

“Sheria ambayo haimchanganyi na rai wa kawaida kwani ni kundi maalumu kuliko kundi jingine kwani yanapotokea majanga mfano kipindi cha UVIKO-19,rai waliambiwa wajifungie ndani lakini waandishi wao walikuwa wanatoka nje kwa ajili ya kuhabarisha umma,”ameeleza Soko.

Novemba 2 kila mwaka kuanzia mwaka 2013, Duniani kote tunaadhimisha siku ya Kimataifa ya kukomesha Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari, (International Day to End Impunity for Crimes against Journalists).

Maadhimisho haya kwa mwaka 2023 yanalenga kuongeza uelewa kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao lakini pia kuonya juu ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili na ukandamizaji dhidi ya waandishi wa habari.