December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utoro wakithiri kwa walimu,105 washitakiwa,wapewa adhabu mbalimbali

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KATIKA kipindi cha kuanzia Julai 2020 hadi Septemba 2021 walimu 931 wamefanya makosa ya utoro kazini ambayo ni sawa na asilimia 51.9 ya makosa yote yaliyofanywa huku katika kipindi cha Julai –Septemba  mwaka huu walimu 105 ambao ni asilimia 57.1 wameshtakiwa mahakamani kwa kosa hilo.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi  wa Walimu Willy Komba wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma huku akisema,katika makosa mazito matano ambayo yamekuwa yakijitokeza na kufanywa na walimu,kosa la utoro linaongoza.

Mwenyekiti huyo ameyataja makosa mengine kuwa ni kughushi vyeti ambapo katika kipindi cha Julai 2020-Septemba mwaka huu kulikuwa na kesi  461  ambayo ni asilimia 25.7 huku katika kipindi cha   Julai –Septemba mwaka huu kesi za kughushi vyeti ni 41 asilimia 22.3.

Vile vile amesema,jambo lingine la utovu wa nidhamu kwa walimu ni suala la walimu kujihusisha  kimapenzi na wanafunzi ambapo mwaka Julai 2020- Septemba 2021 walimu 211 sawa na asilimia 11.8 wameshitakiwa.

Aidha amesema katika kipindi cha  Julai-Septemba pia wapo walimu waliokiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kufanya ukaidi huku wengine wakifanya makosa ya ulevi.

“Kwa hiyo hayo yote ni makosa mazito ambayo yanashughulikiwa na TUME  ya Utumishi wa Walimu ..,lakini yapo makosa mepesi ambayo yanashughulikiwa katika ngazi ya shule.”amesema Komba

Komba amesema,walimu wote waliofanya makosa hayo  wamepata adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi ,kupewa karipio ,kupunguzwa  mshahara,kushushwa vyeo na wapo waliopewa onyo.

Hata hivyo mwenyekiti huyo amewapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kufundisha na kulea watoto katika nyanja mbalimbali huku akiwasihi kuendelea kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia maadili,taratibu,miongozo na sharia zinazowaongoza.

Vile vile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupandisha madaraja walimu wote waliostahili kupanda.

“Tangu Rais aingie  aingie madarakani kumekuwa na neema hasa mwaka huu katika sekta ya elimu na kwa walimu baada ya kutoa kibali cha kupandisha madaraja kwa walimu wenye sifa ambapo jumla ya walimu 126,346 waliokuwa na sifa walipandishwa madaraja.”amesema

Kwa mujibu wa Komba ,walimu  waliopandishwa vyeo walirekebishiwa mishahara yao kwa wakati tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.