May 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utekelezaji wa Ilani kwa kishindo kete ya ushindi CCM Uchaguzi 2025-Dkt. Dimwa

Na Is-Haka Omar, Timesmajiraonline,Zanzibar

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, hivi karibuni alifanya ziara muhimu ya kisekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC, CCM Taifa Zanzibar, yenye lengo la kuimarisha uhai wa chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2025.

Katika ziara hiyo, Dkt. Dimwa alikutana na kuzungumza moja kwa moja na wajumbe wa kamati za siasa za CCM katika matawi, wadi, na majimbo ya wilaya zote 12 za kichama kwa Unguja na Pemba.

Katika mikutano hiyo, Dkt. Dimwa alisisitiza mambo tisa ya msingi ambayo wanachama, viongozi, na watendaji wa CCM wanapaswa kuyapa kipaumbele na kuyafanyia kazi ili chama kishinde na kuendelea kubaki madarakani

***Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Dola 2025

Dkt.Dimwa,alihimiza wanachama kuanza maandalizi mapema kwa kuhakikisha mipango na mikakati ya ushindi inawekwa bayana na kutekelezwa kwa ufanisi.

Katika maelezo yake Dkt. Dimwa,amefafanua kuwa kutokana na kazi nzuri ya utekelezaji wa ilani iliyofanywa na Serikali zote mbili chini ya utekelezaji wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi,ametekeleza miradi mbalimbali inayomaliza changamoto za wananchi.

Alisema ufanisi huo wa utekelezaji wa ilani ndio nyenzo kubwa ya CCM kujinadi na kueleza kwa kina juu ya sera za maendeleo za chama hicho zitakazoleta hamasa kwa wananchi kuchagua CCM kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“ Viongozi wetu ambao ni Rais Dkt.Samia pamoja na Rais Dk.Mwinyi ni hakika msemo wa siku hizi ‘’Wameupiga mwingi’’ kwani hata wapinzani wameishiwa sera badala yake wanafanya porojo na kauli za uchochezi ili kutafuta huruma ya wananchi sote tuendelee na mapambano”, alisema Dkt.Dimwa.

***Mabadiliko ya Katiba ya CCM:

Alifafanua kuhusu mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1997 (Toleo la 2022) yaliyofanyika katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa Januari 18-19, 2025, ambayo yameongeza idadi ya wapiga kura ya maoni kwa nafasi za kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani.

Uhamasishaji wa Wanachama Kuchukua Fomu:

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akikagua Gwaride la Vijana wa UVCCM Wilaya ya Kaskazini Unguja Kichama katika ziara yake ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar.

Aliwahimiza wanachama wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kujitokeza kuchukua fomu kuanzia Juni 28 hadi Julai 2, 2025, kabla ya saa 10:00 jioni.

***Ushirikishwaji wa makundi maalum:

Dkt. Dimwa anasisitiza umuhimu wa kujitokeza na kushiriki kwa makundi maalum hasa wanawake,watu wenye ulemavu,wajane na vijana katika mchakato wa kura za maoni ili kukuza usawa na uwakilishi jumuishi.

***Kukemea makundi yasiyofaa ndani ya CCM

Ametoa onyo dhidi ya makundi ya kuvuruga umoja wa chama, hususan katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya CCM.

Dkt.Dimwa,ambaye pia ni Mwenyekiti wa Sekretarieti hiyo anaeleza kuwa huu ni wakati wa wanachama wote kushikamana huku wakiepuka vitendo vya kuleta mpasuko na migogoro isiyokuwa ya lazima ndani ya chama.

“Viongozi na wanachama wenzangu kwa ujumla nasaha zangu kwenu tuwe na umoja na mshikamano ili kuziba mianya ya wapinzani na makundi maovu kujipenyeza kwa lengo la kutugawa ili tusipate ushindi tuliokusudia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Tumetekeleza kwa ufanisi mkubwa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 ili kila mwananchi awe na maisha bora na yenye hadhi, hivyo tujiandae kikamilifu kuhakikisha ifikapo octoba sote tunaenda kupiga kura asiachwe mtu majumbani.”,alisema Dkt.Dimwa.

***Heshima kwa wanachama

Alikumbusha juu ya umuhimu wa kuheshimu utu, haki na heshima ya kila mwanachama kama inavyoelezwa katika Ibara ya 4 ya Katiba ya CCM.

***Rushwa

Naibu Katibu Mkuu huyo Dimwa, aliweka wazi kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitovumilia vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa ndani hadi uchaguzi mkuu na kwamba vitendo hivyo vimekuwa na vikiwakosesha haki ya kupata nafasi za uongozi watu wenye sifa na maadili mema.

Alieleza kuwa kutoa na kupokea rushwa ni kosa la jinai hivyo tabia hizo zinatakiwa kuthibitiwa ipasavyo kabla havijaleta madhara ndani ya chama hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa dola.

“Rushwa ni adui wa haki, wengi wameumizwa na kuachwa na majeraha kwa kukoseshwa haki zao na watu wenye fedha au mamlaka ya kutengua maamuzi ya wengi,naahidi katika uongozi watu sitokubali rushwa ipate nafasi kwani madhara yake ni makubwa katika ujenzi wa demokrasia na siasa jumuishi kwa wote”,alisema Dkt.Dimwa.

***Utekelezaji wa kauli mbiu ya “Ushindi ni Lazima”:

Akisisitiza utekelezaji wa Ibara ya 5 ya Katiba ya CCM, Dkt. Dimwa alieleza kuwa ushindi wa CCM siyo hiari bali ni jukumu la kila mwanachama.

Onyo kwa watendaji wanaokiuka kanuni:

Alitoa onyo kali kwa baadhi ya watendaji wanaowapigia debe wagombea kabla ya muda rasmi wa kampeni, akisema hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa watakaobainika.

Katika ziara hiyo, Dkt. Dimwa akiwa Wilaya ya Micheweni, Pemba, ambako alitoa maagizo kwa Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Nishati, Maji na Madini Zanzibar kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hasa kuondoa urasimu wa huduma za afya katika hospitali ya wilaya na ucheleweshaji wa kuwaungia wananchi huduma za umeme.

Katika hatua ya kuhitimisha ziara yake, Dkt. Dimwa alikutana na mabaraza ya wazee wa CCM kutoka mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba kupitia kikao hicho,aliwatambua kama nguzo muhimu ya chama kutokana na mchango wao wa kihistoria katika harakati za ukombozi na uendelezaji wa CCM kutoka enzi za ASP na TANU hadi sasa.

“Ninyi ndio msingi wa harakati za ukombozi na pia mna mchango mkubwa katika uimara wa CCM hadi leo. Ni lazima tuendelee kuimarisha CCM katika kila ngazi – kuanzia mashina hadi taifa,” alisema Dkt. Dimwa.

Alisisitiza pia kuwa ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 lazima uwe wa haki, halali na wa kishindo, akitoa wito kwa wazee kuendelea kuwa mfano kwa wanachama na kuwahamasisha wananchi kwa ujumla kuipigia kura CCM.

Katika ziara hiyo Dkt.Dimwa,alibainisha kuwa azma ya uongozi wa CCM ni kukirudisha chama kwa wanachama wenyewe ambao ni wakwezi,wakulima na wafanyakazi wakitafsiri kwa vitendo falsafa ya ‘’ujamaa na kujitegemea’’ ili kwenda na zama za Mapinduzi ya kiuchumi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za CCM ngazi za Matawi,Wadi,Matawi na Wilaya ya Micheweni kichama katika ziara ya kuimarisha uhai wa Chama iliyofanywa na Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar kisiwani Pemba.

Dkt. Dimwa aliahidi kuhakikisha chama kinabaki imara, kinazingatia katiba na misingi yake, na kinalinda mshikamano wa wanachama kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuwa wa kihistoria.

Alisema amesema Chama kimejipanga kuhakikisha kinashinda majimbo yote ya Pemba,kutokana na wananchi wa kisiwa hicho kukiri kuwa CCM imeisimamia vizuri Serikali yake katika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa kijamii.

Alieleza kuwa maelfu ya waliokuwa Wanachama wa ACT-Wazalendo wakiwemo vigogo,makada na wanachama wa miaka mingi wameendelea kujiunga na CCM huku wakieleza kuridhishwa na sera za Chama Cha Mapinduzi hatua inayoongeza uhalali wa ushindi katika uchaguzi ujao.

Alisema ushindi huo utapatikana kupitia uchaguzi huru,haki na wa demokrasia na kwamba utang’oa mizizi yote ya upinzani hasa ACT-Wazalendo ili kuendeleza safari ya kuifungua kiuchumi baada ya ushindi huo kuelekea 2030.