January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utalii, michezo sekta zenye ukaribu, zinaweza kuinua pato la nchi

Na Philemon Muhanuzi, TimesMajira Online

UKIWA umekaa ndani ya mgahawa wa uwanja wa ndege pale Cairo kila baada ya dakika kumi inatua ndege moja na kuondoka nyingine. Utakunywa kahawa au chai ukiwa unaongea na msafiri mwenzako huku masikio yenu yakizipokea sauti za milio ya ndege za mashirika makubwa duniani.

Ni uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi muda wote. Cairo likiwa ni jiji lenye idadi wakazi wasiopungua milioni 20 ni mojawapo wa majiji ya Afrika yenye pilika nyingi za kila aina.

Wenyeji wanasema jiji lile ndani ya siku za kazi huwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 40. Misri kwa ujumla wake ina idadi ya watu milioni 80 hivyo nusu nzima inakuwa ndani ya jiji la Cairo!.

Chanzo kikubwa cha mapato ya jiji lile ni ile historia ya tangu enzi za kabla ya Yesu Kristo. Zile pyramids zinapeleka watu wa mataifa yote ndani ya miezi yote kumi na mbili ya mwaka pale Cairo.

Na wamisri wamekuwa wajanja kwa kuhakikisha kuwa mtalii anayekwenda kuzitazama pyramids anakuwa na ukaribu na tamaduni zao. Mabasi yakitoka kule zilipo pyramids yanawapeleka watalii katika maduka yenye kuuza vitu vya kiutamaduni.

Tanzania ni tajiri kama ilivyo Misri na pengine kama alivyozoea kusema Hayati Rais wa awamu ya tano John Magufuli, sisi ni matajiri na tutembee tukitambua juu ya ukweli wa utajiri tulionao.

Kazi ya kuutafsiri kivitendo utajiri huo ni ya kufanywa na sekta mbalimbali. Naamini ile ya utalii ikishirikiana vyema na ya michezo tutaweza kupiga hatua kubwa sana za kiuchumi.

Uwepo wa pyramids za Cairo na umaarufu wake unao uhusiano wa moja kwa moja na ubora wa miaka mingi wa vilabu vikubwa vinavyotawala soka la afrika. Walichofanya wamisri ni kuhakikisha kunakuwepo na ule usawa wa umaarufu kati ya hazina zao za kihistoria na klabu zao zenye uwekezaji bora usiotetereka.

Tunavyo vivutio vingi sana vyenye sifa za juu ambazo tunazaliwa, tunakua na tunakufa huku zikiwa vile vile. Mbuga ya Serengeti ambayo inatambuliwa kidunia kama ni urithi wa binadamu haijawahi kupungukiwa na heshima.

Ule ukweli kwamba asilimia takriban 35 ya nchi nzima kuwa ni sehemu ya asili ya wanyama, ni nembo tosha ya utalii kimataifa. Hii faida ya asili tuliyonayo kwa kutulinganisha na majirani zetu ni mtaji ambao ungeweza kuzikuza sekta za michezo.

Simba wamezitumia mechi sita za hatua ya makundi kwa kuvaa jezi zenye kuwakaribisha wageni waje Tanzania, ni ubunifu fulani wenye kila sababu ya kuhamia katika michezo mingine.

Kwamba anapokuja kutembelea Tanzania, mgeni awe katika nchi yenye umaarufu wa kuwa na asili iliyopendelewa na Mungu lakini awe pia mahali ambapo pana umaarufu mwingine wa kimichezo.

Atakayevutiwa na maneno karibu Tanzania akiitazama Simba inayopambana ugenini anayo haki ya kujua mbali na timu hiyo kuna ulinganifu upi wa kimichezo wenye kulingana na hilo tangazo linalomkaribisha kutembelea nchi maarufu barani afrika.

Ni ukweli huu wenye kuifanya serikali iweze kuona sababu ya kina ya kuwa na wenye kuiongoza sekta ya utalii wakiwa na maono mapana yenye vionjo vya kiulimwengu.

Wale wenye kuongoza sekta ya utalii pasipo ule upeo wa ziada wenye kuweza kuleta jipya, hao ni bora wakawekwa mbali na vyeo vya kimaamuzi. Sehemu kubwa ya Misri ni jangwa.

Hata ukiyatazama majengo mengi ya Cairo utaona yamejaa vumbi litokanalo na upepo wa jangwani. Rasilimali chache za asili za kiutalii zinatumika na kuchagiza maendeleo ya sekta nyinginezo zikiwemo za michezo.

Sisi ambao sehemu kubwa ya nchi ina ile hali ya kijani yenye rutuba, tumependelewa na Mungu. Kuutumia huo upendeleo ili utalii uweze kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na sekta kama ya michezo ni kazi yetu, ni kujituma kwetu sisi wenyewe.

Napenda kuishauri serikali ihakikishe kunakuwepo na ukaribu kati ya sekta ya utalii na ile ya michezo. Mtalii anayekwenda Misri kutazama pyramids akiwa ndani ya basi la watalii na akaamua kusoma magazeti ya Cairo anakutana na habari ya Al Ahly kutawala soka la afrika.

Anajikuta akipata wazo la kuwa mmoja wa wanahisa wa klabu hiyo akiwa pale pale njiani kuelekea kutazama vivutio ambavyo ni sehemu ya urithi wa kidunia. Tunao mlima Kilimanjaro, tunayo kreta ya Ngorongoro, tunazo mbuga nyingi tu.

Lakini mtalii anayekuwa njiani kuelekea kutazama vivutio vyetu akisoma magazeti yetu haswa zile kurasa za michezo anakutana na habari zisizo na mvuto.

Hapati ile hamu ya kufikiria kuwa sehemu ya vilabu vyetu, haupati ule mvuto unaomfanya awazie masuala mengine zaidi ya utalii uliomleta.

Baraka ya vivutio vya utalii tuliyopewa na Mungu ni fursa iliyojificha ambayo ikiwekwa vyema hadharani itainua sana sekta nyingine haswa ile ya michezo. Jezi yenye maandishi karibu Tanzania imeshakaribisha raia wengi wa kigeni katika kila uwanja ambapo imeonekana.

Hao waliokwisha kukaribishwa wanaweza pia kuwekeza kwenye michezo. Serikali imejiandaa kuwa na ufanisi wenye kulingana na matakwa ya hao waliokaribishwa ili wepesi wa kiutendaji uwe na tija michezoni?.

Zile pyramids kule Cairo zinaingiza mamilioni ya pesa kwa Serikali kuu ya Misri lakini kwa upande mwingine hata ubora wa kina Al Ahly, Zamalek na Ismailia na wenyewe unaguswa na neema za utalii.

%%%%%%%%%%%%%%%