December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utafutaji wa maisha kwa wazazi moja ya chanzo cha kushamiri vitendo vya ukatili watoto

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,  Dodoma.

OFISA Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dodoma,Josephine Mwaipopo ametaja utafutaji wa maisha kwa wazazi na walezi kuwa sehemu kubwa inayochangia watoto kukosa uangalizi wa karibu na kujikuta wakifanyiwa vitendo vya kikatili.

Mwaipopo amesema hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumza na walimu,walezi na wamiliki wa shule binafsi za awali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika Tamasha liliandaliwa na walimu wa shule binafsi jijini hapa.

Amesema kuwa sababu hiyo inachangia vitendo vya ukatili kwa watoto kushamiri kutokana na wazazi na walezi kutotimiza wajibu wao wakutoa malezi bora.

Mwaipopo amesema ubize wa kutafuta maisha unamfanya mzazi au mlezi kutokukaa karibu na watoto wao ilikuwapatia elimu ya malezi na makuzi nakupelekea watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Aidha,Mwaipopo ametaja sababu nyingine ya ukatili huo kwa watoto ni mitandao ya simu ambazo wanaachiwa na wazazi wao kuangalia picha mbalimbali zikiwemo za ngono.

“Watoto wa siku hizi wanaachiwa simu za mkononi na wazazi na walezi humo kwenye simu hizo wanakutana na picha chafu zikiwemo za ngono suala ambalo ni hatari kwa kizazi cha sasa,”amesema.

Pamoja  na hayo Mwaipopo amezipongeza shule za awali na binafsi kwa kuisaidia serikali kuwalea watoto na kuwafanya kuwa na maadili ya kiroho na kimwili.

“Serikali lazima iwapongeze shule hizi za awali za binafsi kutokana na mchango mkubwa wa malezi ya watoto na tumeshuhudia sisi wenyewe shule hizi zikishika nafasi hata kwenye matokeo ya mitihani kwa kufanya vizuri,”amesema.

Naye Mkuu wa shule ya kkmataifa ya Almes,  Reuben Kiloy akizungumza kwa niaba ya walimu na wamiliki wa shule binafsi katika Tamasha hilo ametaja lengo la kukutana hapo kuwa ni kujifunza  malezi na makuzi ya watoto ili kuwalinda na vitendo viovu  dhidi ya maadui kwa  mustakabali wa maisha yao ya Sasa na baadae.

Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kuongezeka  kwa wimbi la vitendo vya ukatili  katika Jamii dhidi ya Watoto.

“Malengo ya kukutana ni kuwaleta pamoja na kuwaunganisha walimu wa shule binafsi ili kuwapa walimu fursa ya kujifunza malezi na makuzi ya watoto ili kuwalea na kuwafundisha vema ikiwa ni pamoja na kuwalinda watoto dhidi ya maadui na vitendo viovu n hatarishi kwa maendeleo ya watoto,

“Lengo lingine la kukutanisha walimu hapa ni kutoa mchango madhubuti katika kuhamasisha jamii kuelimisha watoto wetu katika mazingira yasiyokinzana na utamaduni,mila na desturi za kitanzania,”amesema.