NEW YORK, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) limebainisha kuwa, wakati janga la virusi vya corona (COVID-19) likiendelea idadi ya wanawake ambao hawawezi kupata upangaji wa uzazi, ujauzito usiopangwa, ukatili wa kijinsia na mazoea mengine mabaya yanaweza kuongezeka kwa mamilioni katika miezi ijayo.
Hayo ni kwa mujibu wa utafiti wa shirika hilo ambao unaangazia kiwango kikubwa cha athari ambayo COVID-19 inazo kwa wanawake wakati mifumo ya afya inapozidiwa, vituo kufungwa au kutoa huduma chache kwa wanawake na wasichana na wengi kuamua kuruka uchunguzi muhimu wa matibabu kwa kuhofia kuambukizwa virusi.
Kwa mujibu wa UNFPA, kuparaganyika kwa mnyororo wa usambazaji na ununuzi duniani unaweza pia kusababisha uhaba mkubwa wa dawa za mpango wa uzazi na unyanyasaji wa kijinsia unatarajiwa kuongezeka kadiri wanawake wanavyokaa nyumbani kwa muda mrefu.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Natalia Kanem alisema,takwimu hizo mpya zinaonesha athari ya janga ambayo COVID-19 inaweza kuwa nayo hivi karibuni kwa wanawake na wasichana ulimwenguni.
“Ugonjwa huo unazidisha kukosekana kwa usawa, na mamilioni ya wanawake na wasichana sasa wako hatarini kupoteza uwezo wa kupanga familia zao na kulinda miili yao na afya zao. Afya ya uzazi na haki za wanawake lazima zilindwe kwa gharama yoyote. Huduma lazima ziendelee, vifaa lazima vitolewe na walio hatarini lazima walindwe na kuungwa mkono,”alisema Kanem.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wanawake milioni 47 katika nchi 114 zenye kipato cha chini na cha kati wanaweza kukosa kupata uzazi wa mpango wa kisasa na ujauzito milioni saba usiopangwa unatarajiwa kutokea ikiwa amri ya kuendelea kusalia nyumbani itaendelea kwa miezi sita na utatokea usumbufu mkubwa kwa huduma za afya.
Aidha, kwa kila miezi mitatu ya kuendelea kubaki nyumbani itakayoongezeka, wanawake milioni mbili wanaweza kushindwa kutumia uzazi wa mpango wa kisasa.
Pia shirika hilo limebainisha kuwa, viza milioni 31 vya ziada vya unyanyasaji wa kijinsia vinaweza kutarajiwa kutokea ikiwa amri ya kuendelea kubaki nyumbani itaendelea kwa angalau miezi sita.
Kwa kila miezi mitatu ya watu kubaki nyumbani, visa vya ziada milioni 15 vya unyanyasaji wa kijinsia vinatarajiwa kutokea.
Hata hivyo, kwa sababu ya kuvurugika kwa programu za kuzuia ukeketaji kutokana na kujikita katika kupambana na COVID-19, visa milioni mbili vya ukeketaji vinaweza kutokea katika muongo mwingine ujao ambao ungeweza kuwa visa hivyo vimefutika.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25