November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utafiti wa mbegu watakiwa kuzingatia hali ya hewa

NA MWANDISHI WETU – DODOMA

Watafiti wa masuala ya kilimo nchini wametakiwa kutumia matokeo ya utafiti wao wanaofanya katika kuboresha mbegu bora za mazao zinazoendana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuwa na tija katika sekta .

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu wakati akifungua warsha ya kuelimisha wadau kuhusu Kazi za Muunganiko wa Taasisi za Kimataifa za Utafiti wa Kilimo (CGIAR) Jijini Dodoma.

Dk. Jingu amesema lengo kuu la warsha hiyo ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa kuboresha uratibu wa miradi ya OneCGIAR kwa kuzingatia utafiti utakaongeza uzalishaji.

“Kupitia Mkakati wa Utafiti na Ubunifu wa Mwaka 2030 CGIAR imeanzisha mkakati unaojulikana kama OneCGIAR ambao unalenga kufanya utafiti na maendeleo sasa ili tukuze sekta zetu za kilimo, mifugo na uvuvi lazima tuwekeze katika utafiti na maendeleo hivyo mkakati huu utasaidia katika uzalishaji na tija,” Amesema Katibu Mkuu huyo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. John Jingu (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa warsha hiyo.

Pia ameimiza kwamba utafiti wa mbegu unaofanyika usaidie kuleta tija na faida katika shughuli za wakulima, wavuvi na wafugaji pamoja na kuendeleza ugunduzi wa mbegu mpya hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa.

“Hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko ya hali ya hewa hivyo utafiti tunaoufanya uendane na hali ya hewa ya kipindi husika ukizingatia sasa hivi misimu ya mvua imebadilika kwahiyo tunahitaji mbegu zinazoendana na mazingira na namna ya kukabiliana na wadudu waharibifu,”Ameeleza .

Katika hatua nyingine alisisitiza ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo amesema licha ya uwepo wa sekta zingine kilimo kitaweza kustawi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi endapo vijana watawezeshwa kikamilifu.

“Vijana ili washiriki vizuri kilimo wanahitaji elimu , mafunzo kwa vitendo na namna ya kutumia fursa ya ukuaji wa teknolojia katika shughuli zao za uzalishaji wenye matokeo chanya na wafanye kwa tija itasaidia vijana kujikwamua kiuchumi wao wenyewe na kushiriki katika pato la Taifa,”amesisitza Dk. Jingu.

Aidha ameshauri uwepo wa ushirikiano kati ya Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo kwa kuanzisha miradi mikubwa itakayoleta matokeo chanya katika sekta hizo muhimu kupitia mkakati huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Dk. Geoffrey Mkamilo amebainisha kwamba kufanyika kwa utafiti wa mbegu kunasaidia kubaini hali ya mbegu, changamoto na namna ya kuboresha uzalishaji wake utakaoendana na kipindi husika.

“Warsha hii inatuweka pamoja kama wataalamu na wizara za kisekta kubalishana uzoefu na namna ya kufanya utafiti wenye manufaa katika sekta zote za kilimo. Mifugo na uvuvi kubaini mbegu bora na wakati husika wa kuzifanyia kazi ziweze kuzalisha mazao bora kwa jili ya kuimarisha lishe na kipato,”ameeleza Mkurugenzi.

Naye Mtaalamu kutoka OneCGIAR Dk. Regina Kapinga amefafanua kwamba licha ya kufanya utafiti unaowezesha mazao kuhimili mabadiliko ya tabia nchi pia unazingatia uboreshaji wa virutubishi katika mazao ya uvuvi, mifugo na mimea.