Na Mwandishi Wetu
ANTANANARIVO, Utafiti umebaini kuwa,licha ya kuwepo mashaka na upinzani dhidi ya dawa inayodaiwa kutibu virusi vya corona (Covid-19) nchini Madagascar, Serikali inaendelea kugawa dawa hiyo kwa mataifa mbalimbali.
Kwa mujibu wa runinga ya France 24 iliripoti kuwa, pamoja na wasiwasi wa jamii ya kimataifa kuhusiana na matokeo ya dawa hiyo ya Covid Organics iliyotengenezwa na Madagascar, lakini viongozi wa nchi hiyo wameanza kuisambaza kwa nchi za Afrika kwa lengo la kutibu ugonjwa wa Covid-19.
Dawa hiyo iliyoandaliwa kutokana na mti unaoitwa Artemisia, imegawiwa kwa kiasi kikubwa nchini humo.
Kwa mujibu wa France 24, katika hali ambayo dawa hiyo ambayo ni aina ya kinywaji bado haijafanyiwa utafiti wowote wa kielimu, lakini imeidhinishwa na Rais Andry Rajoelina wa Madagascar na kuanza kusafirishwa katika nchi nyingi za Kiafrika.
Mwishoni mwa wiki Shirika la Afya Duniani (WHO) licha ya kutahadharisha juu ya matumizi ya dawa ya Covid Organics, liliwataka viongozi wa serikali ya Antananarivo kuifanyia utafiti wa kitiba.
Pia Umoja wa Afrika umeitaka Madagascar kuweka wazi matokeo ya uchunguzi wa kitaalamu kuhusiana na usalama wa dawa hiyo kiafya.
Aidha, nchi za Afrika zikiwemo Niger, Equatorial Guinea, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania tayari zimeshaagiza dawa hiyo kwa ajili ya kuifanyia utafiti.
Licha ya Madagascar kusajili kesi 193 za waathirika wa virusi vya Corona, lakini hakuna mtu yeyote nchini humo aliyethibitishwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
WASHINGTON
Mbali na hayo, utafiti mpya unaonyesha kuwa huenda maelfu ya wananchi wa Marekani wakafariki dunia kwa kunywa pombe kupita kiasi, kubugia dozi zilizopitiliza za mihadarati au kujiua kutoka na msongo wa mawazo uliosababishwa na janga la COVID-19.
Utafiti huo uliofanywa na Shirika la Well Being Trust likishirikiana na Taasisi ya Madaktari wa Kifamilia ya Marekani (American Academy of Family Physicians) umeonya kuwa, huenda Wamarekani 150,000 wakajitoa uhai kutokana na kukata tamaa na msongo wa mawazo uliosababisha na athari za janga la corona.
Utafiti huo unaeleza athari ya wananchi wa Marekani wamekata tamaa ya kuendelea kuishi kutokana na matokeo hasi ya janga la corona ambalo limepelekea wengi wao kupoteza ajira, kutengwa na taifa hilo kushuhudia mdororo mkubwa wa uchumi.
Utafiti wa maoni uliofanywa na tovuti ya Yahoo News kwa kushirikiana na YouGov unaonyesha kuwa, karibu asilimia 50 ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa utawala wa Rais Donald Trump umefeli katika kulishughulikia janga la corona, na kwamba hali ingelikuwa tofauti kabisa iwapo mtangulizi wake Barack Obama angekuwepo madarakani hivi sasa.
Kwa mujibu wa ripoti, zaidi ya Wamarekani milioni 20 wamepoteza ajira ndani ya mwezi uliopita wa Aprili pekee kutokana na janga la corona, huku Rais Trump akionekana kutolichukulia kwa uzito suala hilo, na badala yake anajishughulisha zaidi na kutafuta wa kulaumu.
Aidha, kufikia sasa, Wamarekani zaidi ya milioni 1.3 wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19, ambapo zaidi ya 76,000 miongoni mwao wamepoteza maisha, na hivyo kuifanya nchi hiyo iwe muathirika mkubwa zaidi wa corona duniani.
MAANDAMANO
Katika hatua nyingine, watu 10 wamekamatwa na afisa wa polisi kujeruhiwa kufuatia maandamano yaliyotokea mjini Melbourne, Australia.
Waandamanaji hao wanadai kuwa virusi vya Corona ni njama tu iliyobuniwa na serikali ili kudhibiti idadi ya watu.
Zaidi ya waandamanaji wapatao 150 walikusanyika nje ya Bunge la Australia katika jimbo la Victoria na kupinga usitishwaji wa shughuli za kiuchumi ulionuia kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.
Maandamano hayo yalikuwa mfano wa yale yaliotokea nchini Marekani huku waandamanaji wakibeba mabango yalioandikwa “Pigania uhuru na haki yako”.
Hayo yanajiri wakati ambapo majimbo mengi Australia yameanza kulegeza vikwazo japo jimbo la Victoria limechelewa kulfanya hivyo kufuatia hofu ya kuibuka kwa mlipuko mwingine baada ya machinjio ya Melbourne kurekodi maambukizi mapya ya virusi vya Corona.
Australia imeandikisha visa 7,000 vya maambukizi ya virusi vya Corona huku watu wasiozidi 100 wakifariki kutokana na ugonjwa huo.
RIPOTI
Ripoti mpya iliyotolewa na Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) imeeleza kuwa, janga la virusi vya corona (COVID-19) limeathiri utaratibu wa usafirishaji haramu wa mihadarati hususan kwa njia ya anga na hivyo kuwafanya wasafirishaji haramu kusaka njia mbadala.
Ripoti hiyo ya UNODC imeeleza kwamba, hatua zinazotekelezwa na nchi mbalimbali kupambana na janga la COVID-19 zimevuruga usafirishaji haramu wa mihadarati kwa kutumia ndege.
Sambamba na kupunguza biashara hiyo kwa kiasi kikubwa au kuongeza kuingiliwa na kuzuiliwa kwa biashara hiyo kupitia usafirishaji wa njia ya ardhi.
Pia imesema mitandao mingine ya usambazaji wa mihadarati hiyo imebanwa na kuingiliwa na wafanyabiashara sasa wanalazimika kutafuta njia mbadala ikiwa ni pamoja na kutumia usafiri wa baharini.
Ripoti hiyo ya utafiti wa ìmasoko, na mwenendo wa biashara ya mihadarati wakati huu wa janga la COVID-19î imeeleza dawa za kulevya kama vile methamphetamine (methafentamin) huwa zinasafirishwa mabara yote duniani kwa njia ya anga kuliko aina zingine za mihadarati.
Hivyo vikwazo vya usafiri wa anga vinaweza kuwa na athari kubwa sana kwa dawa hizo haramu.
Shehena kubwa ya cocaine imekuwa ikisafirishwa kwa njia ya bahari na kutokana na hatua za kupambana na corona shehena hizo zimekuwa zikigundulika baharini hasa Ulaya.
Pia kwa mujibu wa ripoti hiyo, Heroin imekuwa ikisafrishwa kwa njia ya barabara, lakini kutokana na COVID-19 njia ya bahari inaonekana kutumika zaidi hususan kupitia Bahari ya Hindi.
Nayo bangi ripoti inaeleza huenda isiathirike kwa kiwango kikubwa kama cocaine na heroin hasa ukizingatia kwamba uzalishaji wake kwa kiasi kikubwa hufanyika karibu na masoko ya wateja.
Katika matumizi ripoti inasema nchi nyingi zimeripoti uhaba wa dawa hizo za kulevya katika ngazi ya ununuzi wa rejareja, lakini kwa mihadarati kama heroin kwa mfano ripoti inasema uhaba wa kusambazwa unaweza kufanya kuwa na matumizi hatari, kama vile madawa ya kujitengezenea nyumbani na kuonya kwamba watumiaji wa heroin huenda wakabadili mwelekeo na kuingia kwenye dawa zingine kama fentanyl.
Hatari nyingine itokanayo na uhaba wa mihadarati ofisi hiyo imesema ni ongezeko la kujidunga sindano na kushirikiana sindano hizo ambapo vyote vina hatari ya kusambaza magonjwa kama Virusi Vya Ukimwi (VVU) na ukimwi, homa ya ini aina ya C na virusi vya COVID-19.
Pi ripoti imeonya kwamba, kudorora kwa uchumi kunakosababishwa na COVID-19, kuna uwezekano wa kusababisha mabadiliko makubwa katika soko la mihadarati.
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Dk. Mpango amwakilisha Samia sherehe za Uhuru wa Lesotho