January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usomaji wa Ankara za maji shirikishi kuondoa malalamiko

Na Joyce Kasiki Timesmajira online

MENEJA Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Idhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) Titus Kaguo amesisitiza Ankara zote za maji kusomwa wakati mwenye Dira yupo ili kuondoa malalamiko ya kubambikiziwa Ankara za maji.

Kaguo ameyasema hayo katika maonesho ya 48 ya  Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) huku akisema tayari EWURA ilishatoa mwongozo wa suala hilo.

“Katika maji  malalamiko makubwa yapo katika ankara ,lakini EWURA  ilishatoa miongozo kwamba ankara zote ziwe zinasomwa wakati mwenye dira yupo,yaan hakuna cha kusema eti geti limefungwa, litafunguliwa halafu unasoma ankara, na  muhusika atapokea ujumbe mfupi kwenye simu unaoonyesha usomaji ambapo mtumiaji atahakiki kama hajabambikizwa,kama hajasema lolote baada ya siku chache atapokea ujumbe wa  ankara ya kulipia,” amesema Kaguo

Amezungumzia upande wa kutibu maji ambapo amesema , wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara kujiridhisha namna ambavyo mamlaka inatibu maji na kama wateja wanaridhika na huduma.

“Tulitengeneza mfumo  wa kushindanisha mamlaka ambapo kuna mamlaka inayoongoza kitaifa na kuna mamlaka inayoongoza kwa kuwa mwishoni hali iliyosaidia kuboreshwa kwa huduma za maji kwa ujumla

“Kila mwaka EWURA huwa inatayarisha ripoti za mamlaka ya maji ambayo inaonyesha mamlaka ipi ni bora kuliko nyingine, inafanya uwajibikaji na uwazi uwe mkubwa,kwenye maji tunapopanga bei tunashirikisha wadau wote na bei inayokuja inakuwa inaeleweka  hii ni kwa ajili ya kukuza uwajibikaji.”amesema

Ameongeza kuwa”EWURA huwa inageuka kama mahakama ya kuendeshea kesi pale Mamlaka ya maji inaposhindwana na wananchi na kusababisha malalamiko,hii ni kwasababu kwenye uwajibikaji watu wakipata huduma isiyoridhisha wanalalamika,kwa hiyo Kama mamlaka ya maji ilitenda kosa italipa fidia kwa muhusika.”

Kuhusu gesi asilia amesema imesaidia katika uzalishaji wa umeme nchini, inatumika kupikia katika baadhi ya taasisi, viwanda zaidi ya 50 Dar es Salaam na Pwani vinatumia lakini pia ni Nishati mbadala katika kuokoa mazingira nchini 

Katika hatua nyingine Kaguo amewasisitiza wananchi wote wenye magari  kuhakikisha wanachukua risiti baada ya kununua mafuta  ili kurahisisha ulipaji fidia pindi inapotokea wameharibikiwa na gari kutokana na mafuta waliyojaza.

Amesema iwapo mafuta yalikuwa na matatizo na kusababisha gari kuharibika mwenye kituo atapaswa amfidie gharama za ukarabati na adhabau atapewa.