Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar
Tume ya TEHAMA Tanzania imeingia rasmi kwenye ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya Soft-Tech Consultant Ltd,kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya sekta ya TEHAMA pamoja na kupanua fursa za ajira na ubunifu kwa vijana.
Akizungumza wakati wa kutangaza ushirikiano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga,amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na sekta binafsi katika kuharakisha ukuaji wa kidijitali.

“Tanzania ina idadi kubwa ya vijana wenye vipaji ambao wanaweza kuchangia katika maendeleo ya taifa. Kupitia ushirikiano huu, tunalenga kuunda nafasi zaidi za ajira na kuwawezesha vijana wetu kushindana katika ngazi ya kikanda na kimataifa,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Soft-Tech Consultant Ltd Harish Bhatt,amesema kampuni hiyo ina uzoefu wa zaidi ya miaka 33,inafanya kazi katika nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Malawi, Lesotho, Nigeria na Gambia, imeonesha dhamira yake ya kusaidia mabadiliko ya kidijitali nchini Tanzania.
“Tunaamini katika ushirikiano wa dhati na taasisi za umma kama Tume ya TEHAMA ili kuunda mifumo itakayokuwa na manufaa si tu kwa Tanzania, pia kwa matumizi ya kimataifa,”amesema.

Hata hivyo,ushirikiano huo utazingatia tafiti za pamoja, uundaji wa mifumo ya TEHAMA, pamoja na programu za kujenga uwezo kwa wabunifu vijana, kama sehemu ya dira pana ya Serikali kuelekea uchumi wa kidijitali.
More Stories
Mpango ujenzi wa nyumba ya Katibu Jumuiya ya wazazi kuanzishwa
Waandikishaji wapiga kura watakiwa kuzingatia weledi
CCM Songwe yatoa onyo kwa makada wanaojipitisha kabla ya kampeni