December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushirika Katavi unavyopaa kwa mafanikio, kuleta mapinduzi kwa maisha ya wadau

Na Ntambi Bunyazu

USHIRIKA ni moyo wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja katika ngazi mbalimbali kwenye ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi Taifa.

Katika mkoa wa Katavi, vyama vya ushirika vya aina mbalimbali vimeanzishwa vikiwemo vya wakulima wa mazao mchanganyiko, wafugaji, wavuvi na vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS).

Katika kumkokomboa mkulima, mkoa wa Katavi umeanzisha na kusimamia ipasavyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kumpatia bei nzuri na kuondoa mnyororo wa mtu wa kati aliyekuwa akinunua mazao ya wakulima kwa bei ya chini na kujipatia faida kubwa.

Mfumo huu umekuwa ukitekelezwa kupitia masoko ya wazi na soko la bidhaa (TMX).

Akizungumza katika mahojiano maalum Mjini Mpanda, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera, anasema mkoa huo umedhamiria kuimarisha masoko ya mazao ya wakulima ili yaweze kuwapatia bei nzuri na kuwezesha kuinua maisha ya mkulima mmoja mmoja na uchumi wa mkoa kwa ujumla.

“Katika kuimarisha kilimo na masoko bora, kwa ajili ya kumkomboa mkulima wa mkoa wa Katavi tumeanzisha Stakabadhi ya Mazao Ghalani ambayo inaendelea kufanya vizuri sana katika mkoa wetu wa Katavi kwa lengo la kukata mnyororo wa mtu wa kati ambaye anakuwa kama dalali katika masoko ya mkulima,” anasema Mhe. Homera.

Mauzo ya ufuta kwa Vyama vya Ushirika kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umewezesha kilo 1,370,718 kuuzwa katika minada mitatu iliyofanyika mkoani Katavi msimu huu.

Kutokana na mauzo hayo, sh. 2,767,200 zililipwa na makampuni yaliyoshiriki kwenye minada hiyo. Kati ya fedha hizo wakulima walilipwa sh. 2,555,511,910 kupitia akaunti zao za benki.

Aidha, katika fedha hizo jumla ya sh. 82,243,080 zimeingia katika Halmashauri za mkoa wa Katavi kama ushuru ambazo zitatumika katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo hayo.

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Kakozi Amri amesema kuwa kumekuwepo na ushirikiano mkubwa katika usimamizi wa Vyama vya Ushirika kati ya viongozi wa mkoa, wilaya, Halmashauri. Ambapo ushirikiano huo umewezesha kuongezeka kwa idadi ya vyama, wanchama na idadi ya mazao yanayoshughukiwa na vyama vya ushirika.

“Hapo awali ushirika katika mkoa wa Katavi ulikuwa ukishughulikia zao moja tu la tumbaku, lakini sasa vyama vya ushirika katika mkoa wetu vinajihusisha pia na mazao ya pamba, ufuta, korosho na alizeti. Wakulima wameweza kuongeza kipato kutokana na kuuza mazao haya kwa bei nzuri ikilinganishwa na wakati yalikuwa yanauzwa nje ya mfumo wa ushirika,” anasema Kakozi.

*** Kuanzishwa kwa LATCU LTD

Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima mkoani Katavi (LATCU Ltd) kilianzishwa mwaka 1994 na hadi sasa kina vyama vya Ushirika vya msingi wanchama 11 ambavyo ni Mpandakati AMCOS, Nsimbo AMCOS, Katumba AMCOS, Kasokola AMCOS, Majalila AMCOS, Ukonongo AMCOS, Ilunde AMCOS, Mishamo AMCOS, Tanganyika AMCOS, Ilela AMCOS na Utense AMCOS. Aidha vyama vya Kasekese na Kamwendwe vimeomba kujiunga na chama kikuu na vinasubiri kupata ridhaa ya wanachama katika Mkutano Mkuu wa LATCU Ltd.

Chama Kikuu cha Ushirika cha wakulima mkoani Katavi kimekuwa kikiwapatia wakulima kupitia vyama vya Ushirika pembejeo kwa wakati, na kusimamia shughuli za kiuchumi za chama na vyama wanachama wa LATCU Ltd.

Kaimu Meneja Mkuu wa LATCU Ltd, Fatuma Kombe, anasema kuwa mazao makuu ya biashara mkoani Katavi ni pamoja na Tumbaku ambayo ilianza kuzalishwa mwaka 1970; na mazao mengine ni Pamba na Korosho ambayo yameanza kulimwa mwaka 2018.

“Tumbaku msimu wa 2018/2019 tumeuza tumbaku kilo 7,144,032 zenye thamani ya dola za Marekani 10,293,664.41 na pamba msimu wa 2018/2019 tumeuza kilo 8,562,569.10 zenye thamani ya sh. bilioni kumi milioni mia mbili sabini na tano na themanini na mbili elfu mia nane na kumi na mbili (10,275,082,812/=) msimu wa 2019/2020 tunatarajia kuuza kilo 7,250,000 za Tumbaku na kilo. 13,000,000 za Pamba,”anasema Kombe.

***Mafanikio ya chama kikuu LATCU Ltd

Chama kikuu kina rasilimali mbalimbali ikiwemo; majengo na ardhi ambayo inategemewa kuendelezwa kwa kujenga majengo ya biashara; vyombo vya usafiri magari manne na pikipiki saba kwa ajili ya kazi za chama; na kina samani na vifaa kwa ajili ya kazi za chama.

Aidha, Chama Kikuu kwa kushirikiana na vyama vya Ushirika wanachanma wa LATCU Ltd wameweza kununua gari aina ya Toyota Hilux linalosaidia Ofisi ya Mrajis Msaidizi (M) – Katavi kufanya majukumu ya ushirika.

***Chama cha Msingi cha Ilunde AMCOS

Chama cha msingi cha Ushirika Ilunde AMCOS, kiliandikishwa na kusajiriwa Mei 28,1999 kikiwa na wanachama wapatao 214 hadi sasa chama kina wanachama wapatao 482.

Chama hiki kilianzishwa kwa dhumuni moja tu ambalo ni uzalishaji wa zao la tumbaku lakini kwa sasa chama kinajihusisha na mazao mengine kama vile korosho, ufuta, alizeti, mpunga na karanga.

Akizungumzia mafanikio ya Chama cha Msingi cha Ushirika Ilunde Amcos Ltd, Mwenyekiti wa chama hicho, Modesti Yamlinga alisema tangu kuanzishwa kwake kinamiliki mali za aina mbalimbali ikiwemo ofisi ya chama, nyumba ya kulala wageni (guest house), maghala makubwa matatu, stoo moja, jengo la ofisi moja na nyumba ndogo ya chama.

“Mpaka sasa chama chetu kina jumla ya miradi miwili ambayo ni Mradi wa nyumba ya kulala wageni na mradi wa upangishaji wa maghala,” anasema Yamlinga.

Kuhusu upandaji miti, Yamlinga amesema kuwa chama kimekuwa kikifanya hamasa kubwa kwa wakulima wake juu ya upandaji wa miti ili kutunza mazingira kwa ajili ya vizazi vinavyokuja. Chama cha Ilunde AMCOS kinamiliki zaidi ya mashamba manne ya miti na yapo vizuri na kuna mashamba ya mkulima mmoja mmoja.

Mafanikio makubwa ya Chama cha Msingi cha Ushirika Ilunde Amcos Ltd ni pamoja na kulipa madeni ya pembejeo na fedha taslimu kwa asilimia 100 licha ya kuwepo na kulipiana ndani ya vikundi vya udhamini, kuanzisha mradi wa nyumba ya kulala wageni (guest house), Kujenga maghala makubwa matatu matatu ya kuuzia tumbaku; Kusomesha watumishi wawili kwa masomo ya utawala na uhasibu kwa ngazi ya cheti, kupokea na kugawa pembejeo kwa wakulima na wanachama, kusimamia shughuli za masoko vizuri; na Kulipa malipo ya wakulima kwa asilimia 100.

***Chama cha Ushirika cha Msingi Katumba AMCOS

Chama cha Ushirika cha Msingi Katumba AMCOS kiliandikishwa kwenye Daftari la Usajiri wa Vyama vya Ushirika Desemba 1995 kikiwa na wanachama waanzilishi 120 na hadi sasa wanachama wameongezeka na kufikia 1,282 na kina wanachama wanaozalisha mazao mbalimbali kwenye kata za Litapunga, Kanoge, Katumba, Mtapenda na Kata ya Urwira.

Katumba AMCOS kilianzishwa kwa lengo la kuwapatia Wanachama nguvu ya pamoja ya uzalishaji wa mazao bora na kuuza kwa pamoja kwenye soko la faida. Pia Wanachama kupitia Ushirika wameweza kupata dhamana na kuweza kukopeshwa na Taasisi za fedha na kuweza kuendesha miradi mingine ya faida kwa Wanachama na Wanajamii kwa ujumla.

Katika Utekelezaji wa Mwongozo wa Serikali kwa Vyama na Wanachama wake kuzalisha mazao mchanganyiko na hasa yale ya kimkakati yanayostawi kwenye maeneo husika ili kuongeza mapato kwa wanachama na Chama.

Katumba AMCOS kilifanya maboresho ya masharti yake kutoka uzalishaji wa zao la tumbaku na kufanya wanachama kuzalisha mazao mengine ikiwa ni pamoja na pamba, alizeti na korosho.

***Mali za Chama cha Katumba AMCOS

Chama cha Ushirika cha Katumba AMCOS kinamiliki Jengo la Ofisi lenye thamani ya sh. 113,400,000, maghala manne yenye thamani ya sh. 321,400,000, gari aina ya Land Cruiser lenye thamani ya sh. 62,933,214 na viwanja vinne vyenye thamani ya sh. 28,913,250. Mali nyingine ni pamoja na kompyuta za mezani nne, kompyuta mpakato nne, mashine ya ya kudurufu moja, jenereita mbili, viti, meza na kabati. Vilevile chama kinamiliki mashamba saba ya miti yenye jumla ya hekari 75.

“Kwa kutumia udhamini wa vikundi kwenye kilimo cha tumbaku, usimamizi wa Farm committee na wajumbe wa Bodi kwenye maeneo wanayosimamia; Chama kinafanikiwa kurejesha mikopo ya pembejeo na ya fedha kwa msimu husika.

Kwa utaratibu huo, Chama kilifanikiwa kununua mali na samani na Chama kinashiriki kwenyeshughuli za kijamii kwa kutoa michango na huduma katika elimu na afya,” Mwenyekiti wa Katumba AMCOS Azory Ntondelo.

***Chama cha Ushirika cha Ukonongo AMCOS

Chama cha msingi Ukonongo AMCOS kimesajiliwa kisheria mwaka 1991 kina jumla ya wanachama 1,691 na katika msimu wa Kilimo 2018/2019 kina idadi ya vikundi vipatavyo 251 ambapo kila kikundi kina idadi ya wakulima wasiozidi kumi, vikundi hivi husaidia Wakulima kudhaminiana ili kuweza kupata Pembejeo za Kilimo.

Chama cha msingi Ukonongo kilianzishwa kwa madhumuni ya kushughulika na kilimo cha zao la Tumbaku pekee lakini kutokana na mabadiliko ya masharti ya Chama yaliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 ambayo yamepelekea Chama cha msingi Ukonongo kujishughulisha na mazao mchanganyiko.

Kutokana na mabadiliko hayo, Chama kinaendesha shughuli za Kilimo cha mazao ya biashara na chakula hususani tumbaku, mahindi, mpunga, karanga, alizeti, ufuta na korosho kwa wanachama.

Hadi hivi sasa Chama cha msingi Ukonongo kinaendelea na utekelezaji wa agizo la Serikali la kuanzishwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya alizeti na ufuta.

Pia Chama kinaendeleza shughuli nyingine za kiuchumi kama ikiwemo Kuendeleza elimu ya Ushirika kwa wanachama; Kukusanya, kutafuta masoko na kuuza mazao ya wanachama na Kununua, kuhifadhi na kuuza zana za kilimo pamoja na Pembejeo.

Akizungumzia kuhusu mali za chama cha msingi Ukonongo AMCOS, Mwenyekiti wa chama hicho, Malilo Godfrey anasema kuwa chama kinamiliki jengo la biashara la sh. 18,750,000, ofisi ya chama ya yenye thamani ya sh. 13,997,184, Jengo jipya la chama lenye thamani ya sh. 43,675,000, ukumbi wa chama thamani yake sh. 57,807,274 gari – Scania 93 thamani yake ni sh.33,000,000 na maghala 11 yenye thamani ya sh. 410,000,000.

“Chama chetu cha Ukonongo AMCOS kimefanikiwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo: Kuwalipa Watumishi wake mishahara kwa wakati; kuboresha zaidi kilimo cha zao la tumbaku na kimeendelea kusimamia shughuli za masoko na malipo ya tumbaku; kuendesha semina kwa watendaji na wajumbe ili kuwajengea uwezo wa utendaji wa kazi za Chama na kuboresha mahusiano mazuri na wadau wake kama vile Premium Active (T) LTD, Bodi ya Tumbaku, Mabenki na Chama Kikuu LATCU LTD,” alisema Malilo.

***Chama cha Ushirika cha Mazao Kasokola AMCOS

Chama cha Ushirika cha Mazao Mchanganyiko cha Kasokola AMCOS kilianzishwa mwaka 2014 chini ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013 kikiwa na wanachama 332. Hadi sasa idadi ya wanachama wameongezeka na kufikia 409 na kinahudumia vijiji nane, ambavyo ni Manga, Shankara, Kasokola, Itenka, Majalila, Nsanda, Kasolwa na Ivungwe.

“Chama chetu tangu kianzishwe kimekuwa kikishughulika na zao la Tumbaku, mpaka kufikia mwaka 2018 tulianza kuwahudumia wakulima wa Pamba na kuongezeka kwa mazao ya Ufuta na Alizeti kwa msimu wa 2019/2020,” anasema Mwenyekiti wa Kasokola AMCOS, Jonas Msusa.

Chama cha Ushirika cha Kasokola AMCOS kina jengo lenye thamani ya sh. 59,705,000 ambazo ni ushuru uliotokana na zidio la uzalishaji msimu wa 2016/2017 pamoja na michango ya wanachama. Aidha, chama kina shamba la hekari 15 ambazo hekari 4 zimepandwa miti 19,110 ambayo ni mali ya wanachama.

Kasokola AMCOS kimepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake, mafanikio hayo ni pamoja na; kukopa mikopo ya pembejeo na Cash Advance kwa misimu mitano na kurejesha mikopo hiyo kwa asilimia 100 kila msimu; kupata jengo la ofisi lenye thamani ya sh. 59,705,000; kuwa na shamba la miti la hekari 15 lenye thamani ya Shilingi 5,800,000; kutoa ajira za kudumu na mikataba kwa wakazi wa eneo husika; kujenga majiko ya kisasa na mabani na kuwezesha wanachama kuwa na mashamba ya pamoja ya miti kwa kila kijiji; na chama kimeongeza mazao mengine kama Pamba, Alizeti na Ufuta.

***Mfumo wa Stakabadhi za Ghala

Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni biashara ambapo bidhaa huwekwa kwenye ghala zilizopewa leseni na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Ghala lilopewa leseni linasimamia na kampuni ya kibiashara iliyosajiliwa na hujulikana kama Mwendesha Ghala.

Stakabadhi ya ghala ni nyaraka maalum ambayo inathibitisha umiliki wa mazao husika kwa kuonesha idadi, thamani, aina na ubora wa bidhaa; Stakabadhi ya Ghala huweza kutolewa kwa njia ya karatasi au kielectroniki; Mazao yanawekwa ghalani kwa ajili ya kuhifadhi, biashara, au kupata huduma za fedha kama mikopo.

***Madhumuni ya Kuanzisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala

Kukuza juhudi za Serikali kurasimisha mifumo ya masoko ya bidhaa; Kuweka uwanja sawa zaidi wa kufanya bishara kati ya wazalishaji na wanunuzi, kupunguza hasara baada ya kuvuna, matumizi ya viwango na vipimo, kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi na za kuaminika za soko, kuondoa vikwazo vya kufanya biashara za ndani na zile za kimataifa na kuongeza vipato kwa wakulima na wafanya biashara.

***Manufaa ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala

Manufaa ya Mfumo huu ni pamoja na kumwezesha mwenye Stakabadhi ya Ghala ambaye ni mmiliki wa bidhaa kupata kutunza, kufanya biashara au kukopa katika asasi za fedha kulingana na mahitaji yake, kupunguza mashaka na gharama za miamala na katika shughuli za kuzalisha na kufanya biashara.

Kuwawezesha wakulima wadogo wadogo, wafanyabiashara na wasindikaji kushiriki zaidi katika biashara ya bidhaa kuboresha ufanisi wao na tija katika mfumo wa ugavi wa soko, kutoa uhakika wa ubora na bidhaa na mfumo wa uthibitisho, kuweka utaratibu wa kupata taarifa za soko na mauzo za kuaminika kwa wadau mbalimbali, kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wa bidhaa wenyeji katika biashara ya kimataifa.

Manufaa mengine ni kuhimiza usindikaji nchini wa mazao ya msingi kwa lengo la kuongeza thamani nakukuza uendelezaji wa viwanda; Kuimarisha sekta binafsi kwa kuongeza sehemu za kuhifadhia mazao zilizo bora, kupunguza hasara za baada ya kuvuna na kuimarisha uhakika wa chakula katika nchi na baadae katika ukanda wa afrika mashariki; Kusaidia kuunganisha mfumo wa ugavi wa pembejeo na biashara ya zao lenyewe; na Kuongeza ajira na mchango kwenye juhudi za taifa katika kuongeza upunguzaji umaskini hasa vijijini.

***Soko la Bidhaa Tanzania (Tanzania Mercantile Exchange – TMX)

Soko la bidhaa ni mahali rasmi ambapo wanunuzi na wauzaji wa bidhaa hukutanishwa pamoja ambapo wote huwakilishwa na mawakala. Mawakala hao huendesha shughuli zao kwa kuzingatia taratibu za soko na sheria ili kuwa na ufanisi na kuepuka mambo ya udhalimu.

Katika Mfumo wa Soko la Bidhaa, muuzaji huwa na uhakika wa kulipwa pesa zake baada ya mauzo na hivyo hivyo mnunuzi huwa na uhakika wa kupata mazao aliyoyanunua yakiwa na ubora na kiasi kilichokubalika kwenye mkataba.

Biashara katika soko la bidhaa husimamiwa kisheria ili kuhakikisha kuwa hatua muafaka zinachukuliwa kwa wote ambao wanakiuka taratibu za soko kwa lengo la kujinufaisha na kuwaathiri wengine.

***Manufaa ya Soko la Bidha

Manufaa ya Soko la Bidhaa ni pamoja na kuleta uwazi wa bei za bidhaa na mwenendo wa soko, kuwezesha kila mtu kujua bei ya bidhaa sokoni, kupitia vyombo vya habari, mitandao ya simu, tovuti na pia kwenye maghala huko vijijini.

Mengine ni kutoa bei zenye ushindani kwa kuzingatia upatikanaji wa bidhaa na mahitaji ya bidhaa, hupunguza gharama za kuuza na kununua kwa kuwa soko litawaleta pamoja wauzaji wengi na wanunuzi wengi itakuwa ni rahisi kwa wauzaji kuwapata wanunuzi na wanunuzi kupata bidhaa.