November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Innocent Bashungwa

Ushauri kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Na Philemon Muhanuzi, TimesMajira Online

WAZIRI mpya mwenye dhamana ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, ni mmoja wa mawaziri vijana wa awamu ya tano. Innocent Bashungwa alikuwepo katika baraza lililopita na amekuwa ni mmoja wa mawaziri wanaoendelea kumsaidia Rais Magufuli katika kuliendeleza gurudumu la maendeleo.

Ni waziri kijana kwa maana ya neno lenyewe na kwa maana ya faida ya ujana wake kwa sekta alizopewa dhamana ya kuzisimamia. Yapo mengi yenye kutakiwa kuifikia wizara ya Bashungwa kwa namna ya ushauri na maoni ya wanamichezo.

Siku za karibuni yamekuwepo malalamiko juu ya ubovu wa waamuzi wa mchezo wa ngumi, yanapochezwa mapambano ya kimataifa katika kumbi za Tanzania. Taasisi za kimataifa za ngumi zinayatilia shaka maamuzi ya baadhi ya mapambano ambayo baadhi ya mabondia wetu wamekuwa wakishinda.

Ni katika mazingira haya ya ushindi wa mabondia wetu kuonekana una walakini ndio wenye hoja za kumwambia bondia Hassan Mwakinyo kuwa umefika wakati wa kupambana nje ya Tanzania.

Huwezi kushangazwa na hiyo shaka wanayokuwa nayo wenye kuziendesha taasisi za ngumi za kimataifa juu ya ushindi wa mabondia wetu kimataifa.

Waamuzi wetu wa soka kwa miaka mingi wamekuwa wakikosa nafasi ya kuchezesha mechi za kimataifa za ngazi ya vilabu mpaka zile za michuano mikubwa kama AFCON. Wanaonekana kana kwamba viwango vyao havifikii vigezo vya kimataifa.

Naamini kwamba kutoaminika kwa maamuzi ya waamuzi wetu wa michezo mbalimbali kuna sababu za kitaalam zilizo nyuma yake. Kuna upungufu mwingi ndani ya michezo mbalimbali inayochezwa nchini kwa maana nzima ya upungufu wa utaalam.

Hivi vyama vya ngumi, ipo haja ya kuvikagua kwa undani na kujua vinapungukiwa wapi ili viweze kusimama katika kiwango kimoja na vyama vya mataifa yaliyopiga hatua kwenye usimamizi mzima wa mchezo. Ni aibu kuona Kenya ni majirani wa kaskazini yetu lakini kuna daraja refu sana katika ubora wa mchezo wa riadha kwao na kwetu.

Wao wanafanya lipi mpaka wanaweza kuzalisha wanariadha bora kila mwaka, mpaka baadhi yao wanafikia hatua ya kupewa uraia wa mataifa makubwa kama Denmark na Norway.

Wanaweza vipi majirani zetu hawa wakaitumia fursa ya mchezo wa riadha na ukaweza kuwapatia maisha bora mawakala, makocha na watu wengine wa masuala ya menejimenti?.

Naamini Waziri Bashungwa hataridhishwa tu na ule uwaziri wa kufungua na kufunga matamasha mbalimbali ya michezo huku akitoa risala za jumlajumla za kirasimu.

Ubunifu wake wa kuweza kuwashawishi watu wa mashirika na taasisi mbalimbali wakashiriki katika ujenzi wa viwanja changamani (sports complex) katika mikoa iliyo nyuma kimichezo ni wa muhimu sana.

Vipo vipaji vingi lakini mara nyingi watoto wanazaliwa mpaka wanafikia umri wa kuwa wanamichezo wanakuwa wakikosa sehemu fulani maarufu ya kwenda kucheza mchezo fulani.

Wakati Tanzania ikijivunia mtandao mpana wa wakazi wenye nyumba zenye umeme ndani, haliwezi kuwa ni suala la ajabu kuwepo viwanja vingi changamani huko mikoani.

Na wadau wa michezo wachache wenye kutumia nguvu zao katika kujenga viwanja vya aina hiyo ni watu muhimu kuwekwa karibu na ile mipango ya wizara. Lipo suala la Uganda kuweza kuwa na muendelezo wenye kueleweka wa kulea vipaji vya watoto na vijana.

Mashindano yao ya ngazi za shule ya msingi mpaka vyuo hayajawahi kuacha kuzalisha wachezaji bora. Naamini waziri ataitazama michezo kwa mapana yake, na sio kukubali kumezwa na aina ya ufikiriaji wa watu wanaomzunguka.

Wapo wana michezo wanaoishi kwa mazoea, wanaamini uzoefu wao wa miaka ya nyuma ni muhimu kwa leo na kesho. Waziri Bashungwa ana kila sababu ya kuwakwepa wadau wa aina hii ili aweze kuingiza mtazamo wa ukuzaji wa michezo wa kisasa.

Ni bora kwa faida ya kuacha kumbukizi yenye heshima ya miaka ijayo, akaongozwa na mpango mkakati utakaowekwa hadharani mbele ya wadau.