Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Dar Es Salaam
KESI inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita katika Mahakama Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam imeendelea wakati shahidi wa tatu akitoa utetezi kwa kuieleza mahakama kuwa yeye ndiye aliyemtibu mshtakiwa kidonda katika mguu wake wa kushoto karibu na kidole chake cha mwisho.
Dk Pembe Zuberi, ambaye ni Daktari wa Zahanati ya Magereza, Gereza la Segerea,
ametoa ushahidi katika kesi ya msingi namba103/2018, akiongozwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala mbele ya Jaji, Edwin Kakolaki.
Shahidi, Dkt Pembe alidai Agosti 24,2016 akiwa katika Gereza la Segerea akihakiki washtakiwa wapya alimuona Miriam Mrita akiwa na kidonda ambacho hakijafanyiwa usafi
Shahidi amedai kidonda hicho kilisababisha mguu kuvimba na kuwa kilikuwa kichafu hakijafanyiwa usafi. Baada ya kuona hivyo, alimfanyia matibabu kwa kumsafisha na kumchoma sindano ya kutuliza maumivu na kuua bakteria pamoja na vidonge.
“Mshtakiwa Mrita alifikishwa katika Gereza la Segerea Agosti 23, 2016. Siku ya pili nilipokagua afya za washtakiwa wapya nilimuona mshtakiwa akiwa na kidonda mguuni” alidai na kuongeza
“Sijajua kidonda hicho kilisababisahwa na nini, kwa jinsi kilivyokuwa, kidonda chake kichafu inawezekana alijigonga, kujichoma na mwiba au kujimwagia na maji ya moto” alisema Dk Zuberi.
Dr. Pembe alidai baada ya kumtibu alijaza jina la mshtakiwa huyo katika kitabu cha wagonjwa wa gereza ambapo hakukipeleka mahakamani kwasababu utaratibu hauruhusu.
“Sheria ya magereza inasema Mganga Mkuu wa Hospitali ya Magereza haruhusiwi kutoa kitabu chochote cha hospitali hadi apate kibali kutoka kwa Mkuu wa Gereza husika.”
Alisema Pembe
Baada ya maelezo hayo jaji Kakolaki alisema mahakama itatoa uamuzi katika kesi hiyo ndogo Februari 21,2022.
Upande wa Jamuhuri ukipngozwa na Wakili Mwandamizi, Erick Tesha wakishirikiana na Wakili Gloria Mwenda na Caroline Matemo walieleza kuwa tayari ushahidi umeshafunga katika kesi hiyo ndogo kwa kuwaita mashahidi watatu akiwemo WP 4707 Sajenti Mwajuma (42), na Deogratius kallanga (36) ambaye ni daktari katika Hospitali ya Temeke.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Kibatala, Omary Msemo na Nehemia Nkoko wamefunga ushahidi kwa kuwaita mashahidi watatu akiwemo mshtakiwa wa kwanza Miriam Mrita na mdogo wake Mbaazi Mrita na Askari wa Magereza Daktari Pembe Zuberi ambaye ni daktarin wa Zahanati ya Gereza la Segerea.
Katika kesi hiyo ndogo mshtakiwa Mrita anapinga kupokelewa kwa maelezo ya onyo akitoa sababu tatu ikiwemo, kuteswa, kuchukuliwa nje ya muda uliowekwa kisheria pamoja na kutopewa haki za msingi wakati wa kuandika maelezo hayo.
Mbali na Mrita, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Revocatus Muyella ambapo kwa pamoja wanadaiwa kumuua kwa kukusudia Aneth Msuya, dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi