January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Upungufu wa vitendea kazi unavyokwamisha juhudi za utendaji kazi wa wauguzi

Na Aveline Kitomary,TimesMajira Online,Dar es Salaam.

UUGUZI ni taaluma ambayo inahitaji watu wenye moyo wa huruma.

Hii ni kwa sababu kazi wanayokwenda kuifanya baada ya kuhitimu ni kubwa na inataka moyo wa ziada kuitekeleza.

Miaka ya nyuma, taaluma hii ilionekana ni ya watu waliofeli masomo yao ya kidato cha nne, na hivyo hutafuta fani ambazo zinaweza kuwafanya wakapata kazi ya kujiongezea angalau kipato na kujikimu kimaisha.

Ukichunguza kwa makini,utabaini kuwa wauguzi wengi ni wale ambao wamehitimu kidato cha nne na au darasa la saba.

Hata hivyo,sasa hivi kiwango cha madaraja ya elimu kwa wauguzi imeongezeka, wapo ambao wana shahada ya kwanza hadi ya tatu (PHD).

Kutokana na hali hiyo, weledi na ujuzi wa wauguzi umeongezeka mara dufu zaidi ambapo sasa wana nafasi kubwa ya kuhudumia jamii kulingana na mfumo wa maisha uliopo.

Hadi sasa,Tanzania ina zaidi ya wauguzi 30,451 katika vituo vya umma na binafsi nchini, ambapo asilimia 80 ya huduma za afya katika vituo vya kutoa huduma za afya zinatolewa na wauguzi.

Mei 5 ya kila mwaka Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya Wauguzi.

Lengo la siku hiyo ni wauguzi wanapata nafasi ya kukumbushana mambo mbalimbali katika taaluma yao zikiwamo changamoto za maslahi na za vitendea kazi.

Pia wanapata fursa ya kujadili changamoto ambazo wanakutana nazo katika maeneo yao ya kazi vilevile kukumbushana sheria,viapo pamoja na majukumu yao kwa ujumla ambayo wanayafanya kila siku kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa.

VITENDEA KAZI/MUDA MWIBA KWAO

Ipyana Mwailaph ni Muuguzi kutoka Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) na pia anahudumu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ingawaje umuhimu wa huduma yao ni mkubwa kwa jamii Ipyana anasema changamoto zinazowakabili ni mwiba kwao katika utendaji kazi.

Upungufu wa vitendea kazi ni hali inayokwamisha jitihada zao katika kuwasaidia wagonjwa.

Kutokana na changamoto hiyo inafanya wauguzi kuongeza muda zaidi kazini wa saa tisa.

“Tunajitahidi kuwasaidia wagonjwa lakini tuna upungufu wa vitendea kazi ni changamoto kwani tunatumia muda mwingi kuwepo kazini.

Hali ya ufanyaji kazi kwa muda uliopitiliza haipo katika mfumo wa malipo wa muda wa ziada Ipyana anasema ” hazipo katika mfumo wa malipo na kwamba hatutambuliki mfano suala la bima.

Anafafanua kuwa bima hazimtambui muuguzi kama ni mtu ambaye ana majukumu ya wagonjwa na kwamba hakuna sehemu ambayo wanahusika moja kwa moja akimuhudumia mgonjwa.

Muuguzi huyo anaongeza kuwa katika fomu ya bima hakuna sehemu anayoweza kusaini kama mtoa huduma hiyo na kwamba fomu zote zinamlenga daktari hata kama mambo mengine ameyafanya muuguzi.

Kwa mujibu wa Ipyana itaonekana kama daktari ndio kafanya kazi maana ndiye anayehusika kusaini fomu hiyo ni ya kimfumo zaidi na ni kero ya muda mrefu.

” Timepiga kelele angalau kama ikiwezekana tuweze kusaidiwa na sisi tuonekana, anasema Ipyana.

Wauguzi wakisherekea siku yao

MAJUKUMU YAO YATOFAUTISHWE

Ipyana anaeleza kuwa wananchi hawana uelewa wa kumtambua muuguzi ni nani kutokana na majukumu mengi anayoyafanya.

Anasema kwa mujibu wa taaluma yao jinsi ilivyo Kuna muuguzi na muhudumu wa afya.

” muuguzi ni mtu ambaye tayari analeseni , amekula kiapo lakini muhudumu wa afya ni yule aliyesomea kwa ajili ya kusaidia wagonjwa.

“mfano kuwasindikiza wagonjwa kuchukua vipimo, kufanya usafi wodini hivyo kutokana na majukumu hayo jamii ina amini kuwa nao ni wauguzi.

Ipyana anasema muhudumu wa afya hata akifanya tofauti inaonekana ni muuguzi kama vile kutoa lugha chafu.

Anasema habari inawez kutoka kwenye vyombo vya habari TANNA itakapofuatilia na kukuta aliyefanya kosa sio muuguzi inachukua muda kujulikana ukweli.

WATAKA TAALUM KUTAMBULIKA

Ipyana anatoa wito kwa Serikali iweze kuwaangalia kwa jicho la tatu taaluma hiyo iweze kutambulika na kujitegemea.

“Muuguzi sio daktari msaidizi ni mtu mwenye taaluma ambayo inajitegemea ana majukumu yake inatakiwa hata wanapoandaa mambo ya maslahi wamwangalie muuguzi ” anaeleza.

Anasema bahati mbaya waliyonayo ni kwamba vikao vyote kwenye Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto vinakaliwa na madaktari.

Ipyana anabainisha kuwa madaktari ndio wanao andaa mipango ya masuala ya maslahi na hata kwenye mfumo wa uongozi.

” Ukiangalia taasisi zote za wizarani Katibu mkuu ni daktari, tukija kwenye taasisi za Umma mkurugenzi lazima awe daktari. ” anasema.

Mwisho