Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amebainisha moja ya changamoto zinazoikabili Wizara yake ni upungufu wa maafisa Ustawi wa Jamii hali inayokwamisha changamoto nyingi za jamii kushindwa kushughulikiwa .
Akizungumza wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 na kuomba kiasi cha shilingi bilioni 74.2 kiasi ambacho kimepitishwa na Bunge,Dkt.Gwajima amesema,maafisa Ustawi wanaohitajika ni 5,296 .
“Pamoja na juhudi zote za ushirikishaji jamii zinazofanywa na Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini, bado tunakabiliana na changamoto ya uhaba wa Maafisa hao ambapo, kati ya 5,296 wanaohitajika waliopo hadi kufikia Aprili 2023 ni 3,003 tu .”amesema Dkt.Gwajima na kuongeza kuwa
“Hivyo, upungufu ni 2,293 sawa na asilimia 56.7 ambapo mahitaji makubwa zaidi ya wataalam hawa yapo ngazi ya Kata ambapo kuna changamoto nyingi za jamii zinazopaswa kushughulikiwa. “
Hata hivyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa nafasi za ajira 800 za Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kati ya 2,293 wanaohitajika hivyo, kufanya uwepo wa maafisa hao kuwa asilimia 71.8 kutoka asilimia 56.7.
Ametumia nafasi hiyo kutpoa rai kwa Wadau wa Maendeleo yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoa ajira za muda kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii hususan katika ngazi ya Kata ambapo kuna upungufu mkubwa ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua za kutatua changamoto zinazoikabili jamii hapa nchini zikiwemo za ukatili hususan kwa watoto.
Katika hatua nyingine amesema,Serikali inaendelea kuratibu na kusimamia utoaji wa haki za msingi kwa mtoto ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa.
Hata hivyo amesema, baadhi ya watoto hawazipati haki hizo na hivyo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili katika familia na jamii.
“ Mheshimiwa Spika, moja ya sababu zinazosababisha ukatili dhidi ya watoto hapa nchini ni mwendelezo wa mmomonyoko wa maadili katika jamii unaoambatana na mila na desturi za jamii husika ambazo zinasababisha ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto,
“ Kwa mantiki hiyo, Wizara itaendelea kutekeleza maelekezo ya mamlaka na viongozi wa kitaifa katika kuhakikisha elimu inatolewa kwa jamii ili kudhibiti vitendo vinavyoashiria maadili yasiyofaa pamoja na mila na desturi zenye madhara kwa wanawake na watoto.”amesema Dkt.Gwajima
Kwa mujibu wa Dkt.Gwajima,katika kushughulikia changamoto za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine za Kisekta imeendelea kuratibu na kusimamia utoaji wa elimu ya upatikanaji wa haki za watoto na kupinga ukatili dhidi yao kupitia makundi yote katika jamii.
Amesema,Katika kufikia kundi kubwa la watoto kwenye shule, Wizara imeratibu uundaji wa Madawati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto katika shule za msingi na sekondari nchini likiwa ni jukwaa mahsusi la watoto la kutoa taarifa za viashiria na vitendo vya ukatili vinavyofanywa ndani na nje ya shule kwa usaidizi wa walimu wa malezi na unasihi.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato