Na Esther Macha,Timesmajira Online, Mbeya
BAADA ya kupanda kwa bei ya zao la Kahawa nchini, kutoka sh 4300 kwa kilo moja na kufikia sh. 6500 hadi 7000, mahitaji ya miche ya zao hilo yamekuwa makubwa ukilinganisha na uzalishaji wa miche kwa sasa hali inayowaibua watalaam wa kilimo kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu ili kukidhi mahitaji kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Ofisa Ubora Mwandamizi wa zao la Kahawa Kanda ya Mbeya, Gerald Mlay amesema kupanda kwa bei ya zao la kahawa nchini ni matokeo ya jitihada zilizofanywa na wadau wote wanaohusika na mnyororo wa thamani wa zao hilo likiwemo shirika la Cafe Africa Tanzania ambalo mbali na kusaidia kutafuta soko la uhakika lakini pia waliwajengea uwezo wakulima namna bora ya kuzalisha bidhaa hizo.
Mlay amesema kuongezeka kwa bei ya kahawa nchini imewasaidia wakulima kumudu gharama za maisha ikiwamo kusomesha watoto, kujenga na kufungua miradi mingine ya kujikwamua na umasikini.
Amesema kupanda kwa bei ya zao hilo kumechangiwa pia na mahitaji ya bidhaa hiyo duniani kutokana na kuzalishwa katika hali ya ubora ambao unamudu ushindani wa soko la dunia.
Alipongeza Shirika la Cafe Africa Tanzania, kuwa daraja katika ya wakulima , serikali na wadau kuwasaidia kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja.
Amesema kwa sasa uhitaji wa miche mipya ya zao la kahawa umekuwa mkubwa kutokana na faida inayopatikana sambamba na kuongezeka kwa uzalishaji ukilinganisha na ilivyokuwa awali.
Licha ya manufaa mbalimbali tunayoyaona kwa wakulima wetu lakini bado wanakabiliwa na tatizo la kupanda kwa pembejeo za kilimo ambazo zinachangia kukwamisha jitihada za uzalishaji.
Amesema licha ya kupanda kwa pembejeo za kilimo hususani mbolea kutoa sh 69000 kwa mfuko mmoja hadi 12000 lakini pia upatikanaji wake umekuwa mgumu hivyo aliiomba serikali kuliangalia kwa jicho la karibu suala hilo.
Akifungua kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa Mbeya, Donald Bombo amesema Shirika la Cafe Africa Tanzania kupitia mradi wa CODE P hadi kufikia Mei 2022 wameweza kuwafikia wakulima 11,999 ambapo kati yake 3,719 ni  wanawake na 8,280 ni wanaume na kwamba katika kipindi cha miaka miwili kutoka 2021 hadi 2022 walikuwa na lengo la kuwafikia wakulima 12000.
Miongoni mwa wakulima wa zao hilo, akiwamo Rashid Mwakosya kutoka Chama cha Ushirika Amcos, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya alisema licha ya bei kupanda lakini bado gharama kubwa za pembejeo za kilimo hususani mbolea imekuwa mwiba kwao.
Ameomba Serikali na wadau wengine wanaohusika na uzalishaji wa mbolea nchini kuangalia namna bora ya kuzalisha mbolea nchini ili kukidhi mahitaji ya wakulima na kununua kwa gharama nafuu ukilinganisha na ilivyo sasa ambapo mfuko mmoja wa mbolea unauzwa kwa sh 12000 kutoka 69000 ambayo ilikuwa ikiuzwa awali.
Kwa upande wake, Meneja Programu kutoka Shirika la Cafe Africa Tanzania, Samora Mnyaonga amesema wakulima, maofisa ugani na wadau wengine wanaohusika kwenye mnyororo wa thamani wa zao hilo kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Ruvuma wamekutana mkoani Mbeya kujadili kwa pamoja masuala ya masoko, uongezaji thamani wa zao la kahawa pamoja na kuhimiza ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika uzalishaji wa kahawa.
Mnyaonga amesema kupitia kikao hicho cha siku mbili kinatoa fursa ya kujadiliana  na kutafuta fursa za masoko sambamba na kufundishana mbinu bora za uzalishaji wa zao hilo.
More Stories
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora