November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uongozi wa Samia unavyochochea
kasi miradi ya TASAF Makambako

Na Reuben Kagaruki,TimesmajiraOnline, Makambako

TANGU Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani Machi, 2021 malengo yake makubwa yamekuwa ni kuinua uchumi na kuwaletea maendeleo wa wananchi.

Matokeo chanya ya dhamira yao yameonekana waziwazi na yamedhihirishwa na ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ambayo imeonesha wazi kuwa uchumi ya Tanzania ni unakuwa kwa kasi kubwa mingoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mbali ya kukua kwa uchumi, baadhi ya mikakati ya Rais Samia ambayo imekuwa ikitekelezwa ni pamoja na kazi ya ujenzi wa hospitali, zahanati, vituo vya afya na madarasa na miundombinu mingine mingi ikiwemo ya umeme.

Aidha, chini ya uongozi wa Rais Samia Serikali imeendelea kuhakikisha maendeleo yanayopatikana na yanamnufaisha mwananchi moja kwa moja.

Kinachofurahisha zaidi utendaji wa Serikali ya Rais Samia umekuwa ni wa vitendo zaidi na siyo kujinadi kwenye majukwaa. Kwa mtu ambaye amekaa mjini pengine hawezi kuyaona haya moja kwa moja, mpaka uende vijijini ambako miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa na mingine kwa tena kwa kuibuliwa na wananchi wenyewe.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ile inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Mfuko huu unatazamwa kama mkombozi sio tu kwa za watu wenye kipato duni, bali hata kwenye ujenzi wa miundombinu.

Sehemu ya madarasa yaliyojengwa na TASAF Shule ya MSingi Makatani iliyopo Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.

Ukiuliza mwananchi yeyote anaonaje miradi ya TASAF, jibu la haraka linaanza kwa kumshukuru Rais Samia kwa usimamizi wake mzuri ambao umewezesha wananchi kunufaika na miradi ya TASAF.

Halmashauri ya Mji Makambano ni miongoni mwa halmashauri nyingi hapa nchini zilizonufaika na miradi ya TASAF. katika makala haya, Mwandishi wetu anaeleza kwa kina miradi hiyo ya TASAF ilivyosaidia wananchi kuchochea maendeleo.

Mfano, miundombinu ya nyumba za mbili za walimu (two in one), hosteli ya wanafunzi, jengo la utawala, jiko na bwalo iliyojengwa katika Shule ya Sekondari Mlowa Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikikabili shule hiyo na kukwamisha utolewaji wa elimu bora.

Miundombinu katika shule hiyo imejengwa TASAF kwa sh. 355,433,812.5 na wananchi kuchangia nguvu kazi kwa asilimia zisizopungua 10.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo mwishoni mwa wiki kujionea miumdombinu hiyo ilivyotatua changamoto zilizokuwa zikikabili hiyo Mwalimu Mkuu, Raymond Kyando ameishukuru TASAF, akisema sasa kiwango cha taaluma katika shule hiyo kimepanda ikilinganishwa na kipindi ambacho haikuwa na miundombinu hiyo.

Baadhi ya Madarasa Shule ya Msingi Umago

Kyando anasema miradi ya TASAF shuleni hapo ilianza mwaka 2018 kwa ujenzi wa hosteli ya wanafunzi 72, ujenzi wa nyumba za walimu, jengo la utawala.

“Kabla TASAF kutujengea hosteli wanafunzi walikuwa wanatembea mbali kilometa kilometa 24 kwenda na kurudi. Tulibaini watoto wanapata shida ilitulazimu kuweka kambi ambapo tulitenga madarasa mawili ambayo walikuwa wanalala wanafunzi,” anasema Kyando.

Anasema kutokana na changamoto ya uhaba wa hosteli kuwa kubwa wananchi kupitia mkutano wa kijiji waliomba TASAF iwajengee hosteli ambayo imekuwa mkombozi mkubwa tangu ilipojengwa.

Kyando anatoa mfano kwamba kabla ya ujenzi wa hosteli hiyo kila mwaka wanafunzi kati ya wanne hadi watano walikuwa wakipata ujauzito. “Lakini tangu TASAF itujengee hosteli hiyo hatujawahi kuwa na changamoto hiyo kwa sababu hosteli hiyo imelenga wanafunzi wa kike.”

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Umago iliyopo Halmashauri ya Mji Makambako wakiwa kwenye moja ya madarasa yaliyojengwa na TASAF

Aidha, anasema tangu kujengwa kwa hoteli hiyo kiwango cha taaluma kimepanda ambapo kwenye mitihani ya ndani na ya nje kwenye kata wanaoongoza ni watoto wa kike wa shule hiyo.

“Hivyo tunaamini kabisa uwepo wa hii hospteli umesaidia watoto wa kike na imewabadilisha kitaaluma na kuwawezesha kuelekea kutimiza ndoto zao, lakini pia vikwazo vingine vimeondoka.

“Ndiyo maana Serikali kuanzia ngazi ya mitaa na kata wakaamua sekondari hii iwe shule ya wasichana na lengo letu ni kuifanya iwe shule teule ya wanafunzi wa kike,” amesema.

Anataja sababu nyingine iliyochangia utoro ilikuwa ni kukosekana kwa chakula cha mchana. Alisema tangu shule hiyo ilipoanza kutoa chakula cha mchana kwenye bwalo ambalo limejengwa na TASAF nayo imekuwa chachu ya kupunguza utoro.

“Watoto wanaondoka shuleni saa 11 jioni sasa kama hawapati chakula cha mchana kunachangia utoro, hivyo tulianzisha kampeni ya kuwa na chakula cha mchana ambayo pia imepunguza utoro,”anasema.

Kwa upande wa nyumba za walimu zilizojengwa na TASAF, Kyando alisema zimejengwa mbili (Two in one sawa na nyumba nne) ambazo ambapo zimewezesha walilimu kuishi karibu na shule na wamekuwa wakisaidia wanafunzi wakatia wakujisomea usiku.

Wanafunzi shule ya msingi Makatani wakiwa darasani

“Muda wote walimu wanakuwa shuleni wanasaidia wanafunzi wakati wa kujisomea usiku na muda wote wanaweza kuwafundisha,” anasema Kyando. Kuhusu jengo la utawala amesema limesaidia shughuli za kiutawala na walimu wana ofisi nzuri ikilinganishwa na hapo nyuma,”anasema.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Irene Mgunda ameishukuru TASAF kwa kuwajengea hosteli hiyo, kwani imewasaidia kumaliza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya ujenzi huo.

Anatoa mfano kwamba wazazi wake wanaishi Makambako hivyo bila kuwepo kwa hosteli hiyo asingemudu kutembea kwa miguu kwenda shuleni hapo. Alisema ujenzi wa hosteli hiyo umekuwa mkombozi kwani watoto wa kike wanaoishi nyumbani wanakumbana na changamoto nyingi wakati wa kwenda na kurudi shuleni.

Naye Esther John anasema ujenzi wa hosteli hiyo unawasaidia wakati wa usiku kupata muda wa kujisomea tofauti na yule mwanafunzi anayetokea nyumbani kwani anakuwa na majukumu mengi, hivyo anakosa muda wa kujisomea.

“Tunapotaka msaada kutoka kwa mwalimu tunaupata kutoka kwa walimu maana wapo hapa shuleni ni tofauti na mwanafunzi anayetoka nyumbani kuja shule na mara nyingi wanakumbana na vishawishi vingi,” anasema.

Kuhusu nyumba za walimu zilizojengwa na TASAF mwanafunzi huyo amesema nazo zimekuwa mkombozi, kwani wanapokuwa wanajisomea wanapata msaada kwa urahisi kutoka kwa walimu kwa sababu wanakuwepo shuleni.

Barabara iliyojengwa na wanufaika wa TASAF kupitia ajira za nyda

Naye mlezi wa wanafunzi katika hosteli hiyo, Upendo John (24) anasema ujenzi wa hosteli hiyo umekuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Mlowa, hasa ikizingatiwa watoto wanatoka sehemu mbalimbali na wengine wanakopita sio salama na kuna vishawishi vya aina nyingi.

Ametoa mfano wakati mwingine shuleni kuna vipindi vya ziada ambavyo vinawafanya watoke shuleni wamechelewa hivyo vinaweza kuwafanya wafike nyumbani usiku.

“Lakini wanapokuwa hosteli wanakuwa sehemu salama hivyo ni vigumu kupata vishawishi. Hosteli hii imefanya wanafunzi kuwa salama,” amesema Pendo.

Nao wananchi wa Kata ya Kitisi katika Halmashauri ya Mji Makambako, mkoani Njombe waeondokana na changamoto ya kupata huduma za afya mbali baada ya zahanati ya Kitisi iliyojengwa na TASAF kuanza kutoa huduma.

Hayo yanathibitishwa na wananchi wa kata hiyo pamoja na wauguzi walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea zanahati hiyo ili kujionea jinsi ilivyoweza kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili wananchi hao.

Muuguzi Daraja la Pili wa zahanati hiyo, Grace Ngule anasema mwishoni mwa wiki kwamba zahanati hiyo ilianza kutoka huduma mwaka jana na kwamba imetatua changamoto nyingi kwa sababu kabla ya kujengwa wananchi walikuwa wanapata huduma mbali na makazi wanayoishi.

“Kwa hiyo baada ya zahanati kujengwa imesaidia sana wananchi, kwani wanapata huduma jirani na makazi wanayoishi na inahudumia wananchi wengine wanaotoka nje ya Kata ya Kitisi,” anasema Ngule.

Ametaja huduma zinazotolewa kwenye zahanati hiyo kuwa ni huduma za mama na mtoto, huduma ya kliniki kwa watoto chini ya miaka mitano, huduma endelevu kwa wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na zile za uzazi wa mpango kwa wanawake na wanaume.

Mwonekano wa barabara hiyo

Aidha, anasema wanatoa chanjo kwa watoto. Kuhusu wagonjwa wanahudumiwa kwa wingi kwenye zahanati hiyo, Ngelu alisema ni watoto chini ya miaka mitano kwa sababu katika Halmashauri ya Mji wa Makambako hali ya hewa ni ya baridi , hivyo wengi wanasumbuliwa na nimonia.

Amesema kwa siku wanahudumia wagonjwa 15 hadi 20 mbali na wale wanaofika kwa ajili ya kupata dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na wale wa uzazi wa mpango.

Anasema tangu Zahanati ya Kitisi ianze kutoa huduma imesaidia wanaotumia dawa za kufubaza VVU, kwani hawazifuati mbali kama ilivyokuwa awali na kwamba wametengewa siku maalum kwa ajili ya kuwahudumia.

Naye Diwani wa Kata ya Kitisi, Navy Sanga anaishukuru TASAF na Samia kwa ujenzi wa zahanati hiyo akisema umesaidia wananchi kupata uhakika wa matibabu jirani na makazi yao.

Diwani huyo ameshauri zahanati hiyo iwe inatoa huduma kwa saa 24 ili wananchi wanaopata changamoto usiku waweze kupata huduma bila usumbufu.

Mmoja wa wananchi, Rehema Ndomba, ameishukuru Serikali kupitia TASAF kwa ujenzi wa zahanati hiyo, kwani imekuwa mkombozi kubwa kwao ikilinganishwa na kipindi haijajengwa.

Naye Hoseah Kyando (62), amesema tangu zahanati hiyo imeanza kutoa huduma yeye amekuwa mmoja wa wanufaika kwa kupata huduma, na ile kero ya kwenda nje ya kata hiyo kufuata matibabu haipo tena.

Kwa upande wa Kijiji cha Makatani kukamilika kwa ujenzi wa madarasa sita, vyoo pamoja na miundombinu ya maji kumewezesha Shule ya Msingi Makatani kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi wa Kata ya Makatani waliokuwa wakikabiliwa na adha ya kutembelea umbali mrefu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makatani, Zawadi Salehe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na jinsi miundombinu hiyo iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ilivyosaidia kutatua changamoto ya wanafunzi kupata elimu mbali na wanakoishi.

Mwalimu Salehe anasema kutokana na wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda kusoma Shule ya Msingi Kiumba, Lyamkene na Ilangamoto, wazazi waliona hiyo ni kero kubwa hivyo waliibua mradi wa ujenzi wa shule.

Anasema wananchi walianza ujenzi wa shule hiyo kwa kuanza na madarasa matatu na ofisi na ujenzi wake waliufikisha hatua ya boma.

Baada ya kufikia hatua hiyo amesema walipeleka maombi TASAF ili iwasaidia kujenga shule.

Kwa mujibu wa Mwalimu Salehe, TASAF imejenga vyumba sita vya madarasa, vyoo na miundombinu ya maji ambavyo vyote vimekamilika na kuanza kutumika.

Anasema shule hiyo imeanza kufanyakazi kuanzia Januari, mwaka huu ikiwa na wanafunzi wa darasa la awali hadi la nne jumla wakiwa 167 wakiume 81 na kike 86.

Anasema watoto hao wamehamishiwa shuleni hapo kutoka shule ya msini Kiumba, Lyamkene na Ilangamoto na kwamba watoto walioanzia shuleni hapo kwa sasa ni wale wa darasa la awali.

Amesema ujenzi wa miundombinu hiyo unasaidia maendeleo ya kitaalum kwenda vizuri, kwa sababu shule ina walimu sita na kulingana na Ikama ya walimu na idadi ya wanafunzi inajitolesheza vizuri.

Kuhusu mwamko wa wazazi kupeleka watoto kusoma shuleni hapo, Salehe anasema ni mkubwa kwa sababu idadi ya wanafunzi inazidi kuongezeka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Makatani, Samson Lukogera (62), anasema waliamua kuomba TASAF iwasaidie ujenzi wa shule hiyo baada ya kuona watoto wanatembea umbali mrefu kwenda shule ya Kiumba na Lyamkena.

Choo cha kisasa katika shule ya msingi Makatani kilichojengwa na TASAF

“Kwa hiyo tuliona wanafunzi hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu, hivyo tuliona tuanzishe ujenzi wa shule na tunashukuru TASAF tuliwaomba watusaidie,” alisema Lukogera.

Anasema baada ya TASAF kukubali na wananchi waliunga mkono uamuzi huo kwa kuchangia asilimia 10 ya nguvu kazi ili kufanikisha ujenzi huo.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Esther John (9) amesema anaishukuru TASAF kwa kufanikisha kuanza kwa shule hiyo kwa sababu ameondokana na adha ya utembea umbali refu kwenda kusoma Kiumba.