December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uongozi wa ACT-Wazalendo wafanya ziara Pemba

Na Mwandishi wetu,Timesmajira,online

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo ,Zitto Kabwe, Makamu Mwenyekiti Zanzibar,Juma Duni Haji, Katibu Mkuu  Ado Shaibu na Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais  Othman Masoud Othman wameanza ziara ya siku mbili kwenye Mikoa yote ya Kichama Pemba.

Akizungumza kwenye kikao cha kwanza cha ziara hiyo kilichofanyika katika Jimbo la Konde na kuhudhuriwa na viongozi wa Mkoa, Majimbo na Matawi yote ya Mkoa wa Kichama wa Micheweni, Katibu Mkuu wa Chama ,Ado Shaibu ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwaeleza viongozi na wanachama wa ACT Wazalendo maazimio ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilichofanyika Unguja Agosti 8, 2021 kilichoitishwa kufuatia hujuma iliyofanyika kwenye uchaguzi wa marudio kwenye Jimbo la Konde. 

Kwenye Kikao hicho, Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Kwanza wa Rais  Othman Masoud, Makamu Mwenyekiti  Juma Duni Haji na Kiongozi wa Chama  Zitto Kabwe waliwasilisha maazimio ya Kamati Kuu kama ikiwemo kusisitiza umuhimu wa mazungumzo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamo wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud ameeleza kuwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa marudio katika jimbo la Konde, yeye na viongozi wengine wa Chama walifanya jitihada na kuchukua hatua mbalimbali kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Ndugu Hussein Mwinyi kutatua kadhia ya Jimbo la Konde.

Aliendelea kufafanua kuwa kutokana na jitihada hizo za pande zote mbili, ndio maana Mgombea wa CCM aliyetangazwa kuwa mshindi kinyume na matokeo halisi ya uchaguzi huo  alijiuzulu.

Masoud aliwaeleza viongozi wa Mkoa wa Kichama wa Micheweni kuwa Kamati Kuu imepongeza hatua hiyo ya mazungumzo na kwamba Kamati Kuu inatoa rai kuwa moyo wa mazungumzo uliooneshwa kutokana na kadhia ya Konde, utumike pia katika kushughulikia masuala mengine makubwa yanayoikabili Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake.

 ziara hiyo inaendelea katika Mkoa wa Kichama wa Chakechake. ambapo ziara itahitimishwa kesho kwenye Mikoa ya Kichama ya Wete na Mkoani.