NEW YORK, Shirika la Umoja la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limelaani vikali shambulio lililotokea karibu na shule ya sekondari ya Syed Al-Shuhada huko Kabul, Afghanistan.
Shambulio hilo la linadaiwa kuuwa watoto wanafunzi, wengi wao wakiwa wasichana na kusababisha majeraha mengi.
Katika taarifa iliyotolewa na UNICEF mjini New York, Marekani, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore alisema kuwa vurugu katika shule au karibu na shule hazikubaliki kabisa. “Shule zinapaswa kuwa mahali pa amani ambapo watoto wanaweza kucheza, kujifunza na kujumuika salama,” na shirika hilo limetaka watoto wasiwe walengwa wa vurugu.
UNICEF imerejelea kuwa inaendelea kutoa wito kwa pande zote kwenye mzozo huo kutii sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu na kuhakikisha usalama na ulinzi wa watoto wote.
Kupitia mtandao wa Tweeter, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Volkan Bozkir aliuelezea mlipuko huo karibu na shule mjini Kabul kama shambulio la chuki na la woga.
“Nimesikitishwa sana na maisha ya watu yaliyopotea na majeruhi kadhaa, hasa wanafunzi wadogo. Ninalaani kulengwa kwa raia wasio na hatia na ninatuma salamu zangu za rambirambi kwa serikali na watu wa Afghanistan,”amesema.
Kwa upande wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, bomu hilo ni unyama. Ujumbe huo ulituma ujumbe wake wa masikitiko na kutuma ujumbe wa pole kwa familia za waathirika, ukiwatakia kupona haraka wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo.
Shule ya sekondari ya Sayed Ul-Shuhada ipo katika kitongoji cha Dasht-e-Barchi Magharibi mwa Kabul, makazi ya wengi kutoka kundi la watu wa chache wa jamii ya Hazari ambao zaidi ni waumini wa Shia.
Kufikia sasa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini eneo hilo limekuwa likilengwa mara kwa mara na wanamgambo wa Kiislam wa Kisuni.
Mbali na hayo Umoja wa Mataifa umewaenzi wafanyakazi 336 waliopoteza maisha yao wakiwa kazini mwaka 2020, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea kwa mwaka mmoja.
Hafla ya kuwakumbuka imefanyika kwa njia ya mtandao, kutoa heshima na kuwaenzi wafanyakazi hao ambao ni raia na askari waliokufa kazini kwa sababu ya vitendo vya uasi, majanga ya asili na visa vingine.
Kwa sababu ya janga la COVID-19 na athari zake kubwa, zikiwa ni pamoja na ufikiaji wa huduma za afya idadi hiyo hiyo pia ilijumuisha wafanyakazi waliokufa kwa COVID-19 au magonjwa mengine.
Katika hafla hiyo ya kumbukumbu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema, “Mwaka 2020 haukuwa kama miaka mingine katika historia ya Umoja wa Mataifa. Ulimwengu ulikabiliwa na janga lisilo na huruma ambalo linaendelea kusababisha mateso makubwa. Mamilioni ya familia walipoteza wapendwa wao na familia ya Umoja wa Mataifa haikusalimika.”
Katibu Mkuu alitaka kuwa na muda wa kimya kuwakumbuka wafanyakazi waliopoteza maisha ambao majina yao yalisomwa kwa sauti wakati wa hafla hiyo ya kumbukumbu.
Wakiwakilisha zaidi ya mataifa 80, walitoka kila kona ya ulimwengu, na walionyesha utofauti na utajiri wa uzoefu wa Umoja wa Mataifa.
Guterres aliongeza kuwa, “Walijitolea katika kazi zao kuendeleza maono na maadili ya Umoja wa Mataifa ya kupata amani, kuchagiza maendeleo endelevu na kuendeleza haki za binadamu”.
Patricia Nemeth, Rais wa jumuiya ya wafanyakazi ya Umoja wa Mataifa kwa upande wake aliongeza kuwa wale ambao walitoa, dhabihu kuu ya maisha yao kwa ajili ya shirika hili walifanya hivyo katika juhudi za kulinda uhuru wa walio hatarini zaidi, “na kuwapa mahitaji ya kimsingi ambayo sisi sote tunayafurahia.”
“Wafanyakazi waliokufa mwaka 2020 hawatasahaulika kamwe,”alisema Katibu Mkuu. Pia alisisitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kupitia na kuboresha huduma na usalama wa wafanyakazi.
“Walijumuisha kiini cha upendeleo wa ushirikiano wa kimataifa, watu kote ulimwenguni wakishikamana kujenga dunia bora. Kwa jina lao, tunaahidi kuendelea na kazi hiyo,”amesema
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
Jay-Z aunganishwa na P Diddy kwa kumdhalilisha binti wa miaka 13
Samia avuna makubwa Mikutano ya Uwili G20