November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO: Hatutakuwa na tatizo la umeme

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewahakikishia Watanzania uwepo wa umeme wa kutosha na wa uhakika hata katika kipindi cha upungufu wa mvua za vuli zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA).

Hayo yamesemwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji Umeme wa TANESCO, Mhandisi Pakaya Mtamakaya alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisi za TANESCO Ubungo, Jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Mtamakaya ameyasema hayo kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu muelekeo wa mvua za vuli ambazo zinatarajiwa kuanza kunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka huu ikionesha upungufu wa mvua za kutosha katika kipindi hicho.

Katika taarifa hiyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa imeshauri kuandaliwa nishati mbadala za umeme kutokana na uwezekano wa kupungua au kukosekana kwa mvua za kutosha

Mhandisi Mtamakaya amesema kuwa ikiwa hali hiyo itajitokeza, TANESCO imejipanga vyema kukabiliana nayo kwani hadi kufikia Desemba 08, 2020 saa 2:00 asubuhi, Mabwawa yote ya kufua umeme yalikuwa katika hali nzuri hivyo kuwezesha kazi ya kufua umeme kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Mhandisi Mtamakaya aliongeza kuwa, kina cha maji katika hifadhi za mabwawa yote ni cha kuridhisha na yana uwezo wa kufua umeme kwa miaka mitatu mfululizo bila kuathiriwa na ukame endapo utatokea.

“Hadi sasa maji katika bwawa la Mtera yapo katika ujazo wa mita 697.75 kiasi ambacho ni ujazo wa kutosha kabisa kuwezesha uzalishaji wa umeme”, alisema Mhandisi Mtamakaya.

Aliongeza kuwa, maji hayo ndio yanayo endesha mitambo katika kituo cha Kidatu.

Kwa upande wa Bwawa la Nyumba ya Mungu alisema lipo katika kiwango cha maji ya kutosha ambapo hadi leo maji yako katika kina cha ujazo cha mita 688.32 wakati kiwango cha juu kabisa ni mita za ujazo 688.91.

Hifadhi ya Maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ndio inayotumika kufua umeme kwenye vituo vya Nyumba ya Mungu, New Pangani Falls pamoja na Kituo cha Hale .

Mhandisi Mtamakaya alisisitiza licha ya kuwa na maji ya kutosha Serikali pia imefanya uwekezaji mkubwa katika kufua umeme kwa kutumia gesi asilia na kuongeza kuwa Tanzania ndio nchi pekee Afrika Mashariki iliyowekeza katika kufua umeme kwa kutumia gesi asilia pamoja na Mvuke kwa wakati mmoja (Combined Circle) kupitia mtambo wa kinyerezi II.