January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulenge atoa kompyuta kumuenzi Chifu Mang’enya

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Muheza

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge ametoa kompyuta tano na vifaa vyake vikiwa na thamani ya milioni 15 kwa shule ya Sekondari Chifu Mang’enya iliyopo Kata ya Genge, Wilaya ya Muheza ili kumuenzi kiongozi huyo.

Chifu Erasto Mang’enya alikuwa Spika wa Pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Novemba 20, 1973 hadi Novemba 5, 1975 pia akihudumu kama Waziri wa Elimu, Mbunge, Chifu wa Kabila la Wabondei, Mkuu wa Shule na nafasi nyingine.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ng’arisha Maisha Foundation Mhandisi Mwanaisha Ulenge akikabidhi kompyuta kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Chifu Mang’enya

Akikabidhi zawadi hizo za kompyuta mbele ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo Mhandisi Ulenge amesema ametoa vifaa hivyo kama chachu ili kuona wanafunzi hao wanasoma na kufaulu vizuri hasa masomo ya sayansi na kuwa viongozi kama Chifu Mang’anya.

“Natoa vifaa hivi kwa ajili ya kumuenzi aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Chifu Erasto Mbwana Mang’enya amekuwa kiongozi mkubwa ndiyo maana shule hii ikapewa jina lake ili kumuenzi ni vizuri wanafunzi wanaosoma hapa wakafanya vizuri na kuwa kwenye uongozi kama yeye,mpate taaluma mbalimbali ikiwemo uhandisi, Mhandisi sio mimi peke yangu kwenye Mkoa wa Tanga, lakini nataka vijana wengi wawe wahandisi ili kuifanya Tanga yetu kusonga mbele,” amesema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge amesema kompyuta ndiyo nyenzo muhimu kwa dunia ya Sayansi na Teknolojia ambapo walimu na wanafunzi wanaweza kusoma vitabu vingi kupitia humo, na kuweza kujifunza mambo mengi ya dunia, hivyo wanatakiwa kuweka mkazo kuweza kutumia vifaa hivyo.

“Ulimwengu wa sasa ni wa Sayansi na Teknolojia,walimu na wanafunzi wanatakiwa kusoma kwa bidii elimu haina mwisho, unaweza kusoma hadi kupita mawingu na kwenda kusikojulikana ili mradi upate elimu hivyo, naamini mtaweza kutunza vifaa hivi,”amesema Mhandisi Ulenge.

Diwani wa Kata ya Genge, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Moses Kisiky akizungumza katika hafla ya kukabidhi kompyuta Shule ya Sekondari Chifu Mang’enya

Diwani wa Kata ya Genge Moses Kisiky amemshukuru Mbunge huyo kwa kuweza kuwapa kompyuta Jumuiya ya Shule ya Sekondari Mang’enya kwani itawasaidia walimu na wanafunzi kujifunza mambo mapya.

Mkuu wa Shule hiyo Ramadhan Mbelwa, amesema zawadi hiyo ni muhimu sana kwa nyakati hizi hivyo wamemuahidi Mbunge huyo kuwa watatumia vifaa hivyo kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi, na wataendelea kuvitunza.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge (katikati) akiwa na viongozi wa UWT Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Muheza, na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chifu Mang’enya