Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge ameiomba Serikali kupeleka fedha kiasi cha milioni 900 katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga ili kuifanyia ukarabati wa majengo ya hospitali hiyo.
Hospitali hiyo haina jengo la pamoja la kujifungulia na upasuaji (Maternity Combined), majenereta yake mawili ni mabovu, hivyo umeme ukikatika zaidi ya nusu saa, watoto wenye siku chini ya 28 waliozaliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo njiti wapo hatarini kupoteza maisha.
Mhandisi Ulenge alielezwa changamoto hizo na viongozi wa hospitali hiyo iliyojengwa mwaka 1952 mara baada ya kufanya ziara Aprili 6, 2024 huku changamoto nyingine ni majengo mengi kuwa chakavu na mengine yakivuja inaponyesha mvua.
“Nimeelezwa kuwa kwa bajeti ya miaka mitatu ya fedha (2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024) hospitali imepangiwa kupewa kiasi cha milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa majengo yake, lakini hadi sasa fedha hizo hazijaletwa,”ameeleza Mhandisi Ulenge na kuongeza kuwa:
“Nimeingia kwenye maeneo mengi ikiwemo wodi, hakika hospitali hii inahitaji maboresho ili kuweza kuikoa na iwe tegemeo kwa wananchi wanaotafuta huduma kwa Wilaya ya Korogwe na maeneo jirani ya Wilaya ya Handeni, Lushoto na Muheza,”.
Mhandisi Ulenge amesema hospitali hiyo ambayo kwa sasa inamilikiwa na Halmashauri ya Mji Korogwe, inahitaji jengo la pamoja la wodi ya kujifungulia ambalo litawasaidia wanawake wanapojifungua na baada ya kujifungua, kubaki sehemu moja wakiwa na watoto wachanga, tofauti na sasa wanakuwa wametenganishwa.
Lakini alipokwenda kwa watoto wachanga wenye umri chini ya siku 28 huku wakiwa wamezaliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo njiti, Mhandisi Ulenge hakukutana na wodi, bali ilikuwa chumba tu, huku watoto hao wakiwa wanalala watatu mpaka wanne kwenye kitanda kimoja.
Awali, Kaimu Katibu wa Afya Hospitali ya Magunga Simon Burengeti amemueleza Ulenge kuwa hospitali hiyo majengo yake mengi ni chakavu, na mengine yanavuja. Lakini bajeti ya mwaka 2023-2024 ni ya tatu tangu watengewe fedha kiasi cha milioni 900 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa majengo.
“Maabara ya hospitali ya Magunga ina hadhi ya nyota nne, hivyo inaweza kutumika kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) na wataalamu wa nchi hizo wametoka mwezi Machi kuthibitisha hilo, lakini jengo lake limechoka na halina hadhi,”ameeleza na kuongeza kuwa
“Hospitali ina majenerata mawili lakini yote yamekufa ikitokea TANESCO wakakata umeme hata kwa nia nzuri kwa ajili ya matengenezo, watoto waliozaliwa na changamoto wakikosa umeme kwa nusu saa wanaweza kupoteza maisha,tuna mashine nyingi zinazotumia umeme mwingi, hivyo hospitali kuwa na umeme wa uhakika ni muhimu,”.
Burengeti ambaye pia ni Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Magunga, amesema mpaka mwaka huu vikao vimekaa na kuahidiwa kupata fedha hizo ambazo zingewasaidia kujenga jengo la pamoja la wodi ya wajawazito lenye madirisha makubwa tofauti na sasa pamoja na jengo la kisasa la maabara.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu