Na Mwandishi wetu Timesmajira online
WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema atawapima Mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS ), kwa uwezo wa kutatua changamoto wakati wa dharura ili kuhakikisha barabara zote nchini zinapitika wakati wote.
Ulega ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya za Handeni na Kilindi, alipokagua ujenzi wa barabara ya Handeni-Mafuleta,mkoani Tanga yenye urefu wa kilomita 20.
Amesema Meneja atakayehakikisha barabara za Mkoa wake zinapitika vizuri bila msongamano na kutatua kero za watumiaji wa barabara ndiye atahesabika kuwa Meneja mzuri.
“Rais Samia Suluhu Hassan amenituma nipite kukagua miradi inayoendelea na iliyokwama ili niikwamue,” amesema Ulega.
Amemtaka Mkandarasi Henan Highway Engineering Group (HEGO), anayejenga sehemu ya Handeni -Mafuleta, kuendelea kufanyakazi kwa bidii kwani ameshaanza kulipwa na ataendelea kulipwa ili aendelee kuijenga barabara hiyo usiku na mchana kwa ubora uliokusudiwa.
“Kila mahala kwenye nchi hii kuna ujenzi unaendelea , Rais amedhamiria kuifungua nchi hii katika sekta zote ili kukuza uchumi wa watu”, amesisitiza Ulega.
Katika hatua nyingine Waziri Ulega amehimiza uharaka katika zoezi la kubaini maeneo yenye milima na kona kali katika barabara ya Segera-Chalinze ili zijengwe barabara wezeshi kupunguza msongamano na ajali.
” Vifo na ulemavu vimeendelea kupoteza watu kutokana na ajali za barabarani,hivyo kamilisheni upembuzi yakinifu ili ujenzi katika maèneo korofi uanze mara moja,”amesema Ulega.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta, amemhakikishia Waziri Ulega kufanyiakazi maelekezo yake na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kulinda alama za barabarani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Albert Msando, amesema barabara ya Handeni-Singida ni moyo wa uchumi wa wananchi wa Handeni na Kilindi,kwani ni muhimu katika shughuli za usafiri na usafirishaji hivyo kukamilika kwake kutachochea uchumi waWilaya hizo,na kuunganisha Mkoa wa Tanga na Mikoa ya Kati na Kanda ya Ziwa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilindi Mohamed Kumbi, amesema, maendeleo ambayo Serikali imefanya katika Wilaya hiyo ni mengi na wataendelea kuiunga mkono Serii kufikia lengo.
Barabara ya Handeni-Mafuleta ni sehemu ya barabara kuu ya Handeni -Kiberashi -Singida yenye urefu wa KM 434.33 inayounganisha Mkoa wa Tanga na Mikoa ya Kati na Kanda ya Ziwa kukamilika kwake kutaleta tija kwa bandari ya Tanga.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi