November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulega ataja mkakati wa kuthaminisha zaidi dagaa

Na Edward Kondela,TimesMajira Online,Mwanza

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema serikali imejipanga kuhakikisha inaboresha uvuvi wa dagaa hasusan katika Ziwa Victoria ili kuliongezea thamani zao hilo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akifafanua kuhusu mikakati ya serikali ya kuliongezea thamani zao la dagaa pamoja na kutafuta suluhu ya upungufu wa malighafi ya samaki viwandani, wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya uvuvi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria kilichofanyika katika Maabara ya Taifa ya Uvuvi jijini Mwanza.

Ulega amesema hayo jana wakati wa mkutano na wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaohusika na uchakataji wa minofu ya samaki na wavuvi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita na Simiyu na kusisistiza kuwa serikali imejipanga kuipa thamani uvuvi wa dagaa ili kuongeza uwekezaji wa zao hilo

“Tunataka tupate vichanja vya kutosha katika kuanika dagaa sio dagaa wanamwagwa tu inatakiwa wawekwe kwenye Vichanja’’ amesema Ulega.

Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaongea na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na wadau mbalimbali ili kuwekeza katika uvuvi wa dagaa.

Ameongeza kuwa dagaa wanatakiwa kupelekwa maeneo mbalimbali nchini na kusaidia kuondokana na tatizo la utapia mlo kwa kuwa dagaa wana madini mengi ya kutosha katika kuupatia mwili afya na kushauri viwanda mbalimbali kuhakikisha vinachakata dagaa vyema na kuuza ndani na nje ya nchi.

Muonekano wa baadhi ya wadau wa sekta ya uvuvi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria waliohudhuria mkutano ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) katika Maabara ya Taifa ya Uvuvi jijini Mwanza, ambapo amesisitiza mikakati ya serikali ya kuliongezea thamani zao la dagaa pamoja na kutafuta suluhu ya upungufu wa malighafi ya samaki viwandani

Naibu waziri Ulega amesema uvuvi wa dagaa umeleta ajira kwa watu wengi sana hususan akinamama hivyo ni muhimu kuhakikisha zao hilo linaendelea kuongeza tija zaidi katika kukuza pato la taifa na mtu mmoja mmoja.

Amewatadharisha pia wavuvi wa dagaa na sangara wasije kujiingiza katika mgogoro kama wa wakulima na wafugaji katika kugombania uvunaji wa rasilimali za uvuvi, hivyo serikali itahakikisha inaweka mazingira mazuri zaidi ya uvunaji wa rasilimali hizo baina yao.

Ulega amewaomba pia wamiliki wa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki kuhakikisha wanawalipa wavuvi stahiki zao kwa wakati ili waweze kuendelea kufanya nao biashara ya kuwauzia samaki kutokana na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wavuvi kudai kuwa wamekuwa hawalipwi kwa wakati wanapopeleka samaki viwandani na kuamua kuuza katika masoko ya ndani.

Pia alibainisha kuwa katika Bajeti ya Mwaka wa fedha 2020/2021 kupitia Sekta ya Uvuvi wamefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 22.6 ambapo serikali ilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 33 na kwamba asilimia 80 ya mapato hayo yametokana na Ziwa Victoria.

Naibu waziri huyo amewataka wadau wa uvuvi wawe wanaishauri serikali kuhusiana na sekta hiyo na kwamba lengo la serikali ni pamoja na kudhibiti maeneo ya mazalia ya samaki ili kupata mazao mengi.

Nao baadhi ya uvuvi wakichangia katika mkutano huo wameiomba serikali iwasaidie katika utoaji wa taarifa ya bei elekezi ili kupunguza kubadilika badilika kwa bei za samaki zinazonunuliwa viwandani.

Wameiomba pia serikali iwasaidie wavuvi katika utungaji wa Sera za Uvuvi pamoja na kutaka soko la samaki kuwa huru ili waweze na kujiongezea kipato.

Baadhi ya wavuvi hao pia wameiomba serikali kusaidia katika upatikanaji wa zana za uvuvi pamoja na pamoja na kudhibiti upatikanaji wa nyavu zisizotakiwa ambazo zinavua samaki wadogo.