December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulaji wa ‘Kitimoto’ huathiri ufanisi wa ARVs

Na Hadija Baghasha, TimesMajira online ,Korogwe

ULAJI  wa Nyama za Nguruwe Maarufu kama ‘Kitimoto’ inasababisha magonjwa takribani 17 ambapo kwa watumiaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs) zinashindwa kufanya kazi sawasawa.

Hali hiyo inatokana na kuwepo mkubwa wa asidi.

Akizungumza katika Kongamano la afya lililokuwa na kauli mbiu ‘Pima afya yako kabla hujaugua’ Mkurugenzi wa Zahanati ya Manundu, Dkt Ali Mzige anasema walaji wa nyama ya nguruwe maarufu ‘Kiti Moto’ wanauwezekano wa kupata tatizo la kifafa linalotokana na tegu inayokimbilia kwenye ubongo.

“Nyama ya nguruwe siyo white meat, hilo wajue lakini nyama hii ina magonjwa karibu 17 na husababisha madhara makubwa kwenye mwili,” amesema Dkt Mzige na kuongeza kwamba ulaji wa mbogamboga unasaidia kuondoa sumu mwilini.

Dkt Mzige amesema magonjwa mengi kama kisukari, shinikizo la damu na saratani husababishwa na watu kutozingatia kanuni za chakula wanachokula.

Ameshauri watu wapunguze nishati lishe za ziada (extra calories) matumizi ya sukari, mafuta yenye lehemu (cholesterol) na chumvi.

“Tutumie vyakula vya asilia vyenye lishe makapi-fibre, kula dona badala ya sembe nyeupe,  mihogo, magimbi, viazi vitamu vikipikwa kwa kuchemshwa bila kukaangwa ni bora kuliko chips,” amesema Dkt Mzige.

Aidha, ametoa tahadhari kwa akina mama wajawazito wanaopendelea kula chips mayai wakati wa mimba kwamba chakula hicho kitawapa uwezekano wa kupata kisukari cha mimba.

Pia ameshauri akina mama wanaotengeneza unga wa lishe kwa ajili ya watoto kwamba unga huo uliokuwa na aina nyingi za nafaka haufai kwa matumizi ya watoto.

Dkt Mzige ametambulisha kituo chake kipya cha Mshangai Preventive Medical Care Polyclinic, itakayokuwa na jopo la madaktari bingwa watatoa huduma zote za magonjwa yanayotokana na matatizo mbalimbali ikiwemo saratani.