Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari Kayenze iliopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza wanakabiliwa na ukosefu wa taulo za kike hali inayoelezwa kuchangia utoro na kusababisha kutohudhuria masomo kwa takribani siku nne pindi wanapokuwa katika siku za hedhi.
Wanafunzi hao ambao wamekuwa wakitumia kauli ya ‘nimechafua sketi,kufikisha ujumbe kwa walimu ili waweze kuwasaidia taulo za kike,wameeleza kuwa wanajikuta wanashindwa kuendelea na vipindi na badala yake wanatoroka ili wakajistiri nyumbani.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo Nkwimba John, ameeleza kuwa shuleni hapo kuna uhaba wa taulo za kike na zinapatikana mara chache pia ata wakiwa katika jamii kwa maana ya nyumbani changamoto ni hiyo hiyo inayochangiwa na hali duni za familia na wazazi kutotimiza wajibu wao.
Hayo yameelezwa katika zoezi la ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule hiyo lililofanywa na Mwandishi wa Habari mwanamke wa Mkoa wa Mwanza na mdau wa masuala ya wanawake Grace Mbise wakati akisherekea kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwake Machi 28,2024,ambapo amewafikia wasichana 408 huku shule hiyo ikiwa na jumla ya wanafunzi 1036 kati yao wa kike ni 538 na WA kiume ni 498.
“Unamwambia mama,nimechafuka,nimeingia kwenye siku zangu mama anakukaripia,anakuambia umeniambia mimi nikusaidie nini,mimi siwezi kusaidia mwambie baba yako kutokana na mila na tamaduni kuna vitu siwezi kumwambia baba nahitaji msaada wa mama,hivyo wazazi pia wanachangia sisi watoto wa kike kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa taulo za kike ingawa wengine ni kutokana na hali duni ya familia,”ameeleza Nkwimba.
Nkwimba ameeleza kuwa unakuta binti amechafuka akiwa darasani wakati mwingine Mwalimu yupo ana fundisha hali hiyo inamnyima kujiamini na kushindwa kufuatilia masomo kwa umakini kwani anawaza atavaa nini kwa ajili ya kujistiri ili aendelee na masomo na wakati huo ofisini kwa walimu taulo hazipo huku akikosa namna ya kumfuata Mwalimu ili amueleze tatizo lake.
“Kiukweli naweza kuondoka nikaenda nyumbani kwa ajili ya kujistiri kwani kuna vitu ambavyo ninavyoweza kujistiri mbadala wa taulo za kike,hapa shuleni tunapata wakati mgumu sana unakuta binti kachafua sketi anashindwa kupitia hata mbele ya wenzie hali inayotufanya tukose amani unajiuliza nimfuate nani,kwani unakuta nipo na rafiki zangu ambao nao wanakuwa hawana vitu vya kunisaidia inabidi niende nyumbani na unakuta huko siyo kuwa tuna vitu vya kujistiri ila tunaona ni bora,”ameeleza na kuongeza kuwa
“Mbali na kutumia vitambaa kwa ajili ya kujistiri wakati wa hedhi kuna baadhi wamekuwa wakitumia vipande vya godoro kwa kuunganisha na kitambaa kisha kushona na kutumia kama taulo za kike na baada ya masaa kadhaa anafua na kuanika juani kisha anatumia tena ingawa kiafya siyo salama,”.
Kulwa Kadodosa, ameeleza kuwa ukosefu wa taulo za kike kwa wasichana katika shule hiyo kuna changia utoro na kuingia katika vishawishi ambavyo vinaweza kusababisha kupata mimba katika zisizotarajiwa na katika umri mdogo hivyo kukatishwa masomo na ndoto.
“Kama mimi naishi na mama ambaye ni mgonjwa na ninapitia changamoto hasa nikiwa kwenye siku zangu hali,najikuta nakisa ujasiri ‘confidence’ ya kuwa na rafiki zangu ninapikuwa shuleni,maana ukitumia kitambaa akikai sana na wakati wa jua inasababisha michubuko, hali inayosababisha hata ukiwa una soma uelewi sana,”ameeleza.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Kayenze Deogratus Paulo, ameeleza kuwa mwanafunzi wa kike asipokuwa na taulo za kike akiingja katika siku za hedhi anakuwa amechafuka na mara nyingi anakuwa hana amani darasani hata Mwalimu akiwa anafundisha yeye anakuwa na wasiwasi kwaio elimu ambayo anapewa na kwa siku hiyo nakuwa haipati kwa ufasaha.
“Ukosefu wa taulo za kike unasababisha wanafunzi wa kike kutoroka na wakati mwingine kuacha kuhudhuria masomo kwa kutokuja shule kabisa na badala yake anabaki nyumbani hadi atakapo maliza siku zake za hedhi ambazo ni siku tatu hadi nne,kwaio utoro unakuwa ni mkubwa na wengine kuacha shule kwa kukosa msaada pia kunasababisha kutumia vitu mbadala ambavyo vinaweza kuwasababishia michubuko na hatimaye kupata bakteria na magonjwa mengi,”ameeleza Mwalimu Paulo na kuongeza kuwa
“Hivyo kupitia taulo za kike zinazoletwa na wadau mbalimbali zinasaidia angalau kwa wanafunzi hao wa kike kuwa na amani na kuweza kukaa darasani saa zote za masomo na kuhudhuria vipindi vizuri na kurejea nyumbani wakiwa salama pamoja na kupunguza utoro,”.
Ameeleza sababu inayochangia wanafunzi hao kukabiliwa na changamoto hiyo ni kutokana na baadhi ya wazazi kuwa na uchumi na uelewa mdogo kushindwa kumudu gharama kununua taulo za kike na badala yake kuwataka watumie nyenzo mbadala pia wanafunzi wengi wanajilea wenyewe ambapo unakuta amepanga chumba huku wazazi wakiwa mbali aidha visiwani wakifanya shughuli za uvuvi hivyo binti kukosa fedha za kununulia kifaa hicho.
Haya hivyo ameeleza jitihada mbalimbali wanazofanya katika kutatua changamoto hiyo ni pamoja na kuyaomba mashirika mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwaletea taulo hizo za kike na kuzigawa kwa wanafunzi hivyo kubakiza akiba kidogo kwa ajili ya dharura ambapo mwanafunzi atamfua Mwalimu mlezi wa kike(matron) kisha anampatia.
“Ikitokea taulo za kike zimeisha na hakuna akiba na mwanafunzi ameingia katika hali hiyo basi Mwalimu wao mlezi anawashirikisha walimu na kuanza kuchanga lakini pia Diwani wa Kata yetu tukimshirikisha amekuwa akitoa msaada huo mara nyingi tu pamoja na viongozi wengine hatuachi wanafunzi wateseke ingawa changamoto bado ipo kwa sababu hedhi ni suala la kudumu kwa wasichana,”.
Mwalimu mshauri wa wanafunzi katika shule hiyo John Ndaki, ameeleza kuwa licha ya ukosefu wa taulo za kike kwa wanafunzi hao elimu ya matumizi sahihi wa vifaa hivyo vya kujisitiri pamoja na usafi inahitajika.
“Wana msemo wao kuwa ‘nimechafua sketi,ukisikia tu hivyo unamwambia nenda kachukue taulo zenu za kike,tatizo tunalokutana nalo zile zilizotumika mahali pa kuhifadhia hatuna hivyo nawaomba wadau na serikali kutujengea kichomea taka ili tuweze kuzichoma na kuhifadhia mazingira,kwani tumeweka ndoo chooni ya kuhifadhia lakini unakuta zimezaaga ovyo,”ameeleza Mwalimu Ndaki.
Mwandishi wa Habari wa kituo cha Star Tv Mwanza na mdau wa masuala ya wanawake Grace Mbise ameeleza kuwa ameamu kujitolea kusaidia wasichana hao kupata taulo hizo baada ya kuiona changamoto hiyo.
Mbise ameeleza kuwa amewafikia wanafunzi wa kike wa shule hiyo 408 ili kuwahamasisha wanafunzi kusoma na kuepuka vishawishi kwa kisingizio cha kukosa huduma hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa habari hii Diwani wa Kata ya Kayenze Issa Dida, ameeleza kuwa amekuwa akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt Angelina Mabula ambaye amekuwa akizungumza na mashirika mbalimbali ambayo yamekuwa yakipeleka msaada wa taulo za kike shuleni hapo.
“Wakati mwingine nimekuwa nikitoa fedha zangu mfukoni kwa ajili ya kuwanunulia vifaa hivyo vya kujisitiri kwani ni watoto na sehemu ya familia ya wananchi ninaowaongoza ingawa bado uhitaji ni mkubwa,nitakaa na bodi ya shule kuona ni kwa namna gani tutaanzisha benki ya taulo za kike shuleni hapo ili kutatua changamoto hiyo,”ameeleza Dida.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu