Na Daud Magesa
Ukatili wa kijinsia ni janga la kitaifa na kidunia ambapo changamoto hiyo inaendelea kuwatesa na kuwaumiza watu wengi hasa wanawake na watoto ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa ina mbalimbali hasa watu wa karibu.
Kutokana na changmoto hiyo ipo haja wadau mbalimbali wanaotoa elimu ya ukiukaji wa haki za binadamu kufikisha elimu hiyo ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii nchini.
Pia elimu hiyo ya kupinga ukatili isiwe tu inatolewa katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia badala yake ifikishwe shuleni,katika mikusanyiko mbalimbali ya jamii zikiwemo nyumba za ibada (kanisani na msikitini) na katika jamii yenyewe ili kuiwezesha kupata uelewa wa kutambua madhara ya ukatilim
Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) ni miongoni mwa wadau waliozindua kampeni maalumu ya kupinga ukatili wa kijinsia ukiunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kupinga ukatili huo wanaofanyiwa wanawake na watoto ili lengo la serikali kukomesha vitendo hivyo nchini.
Rais wa UTPC, Deo Nsokolo akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa kampeni maaluum ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii anasema kitaifa,takwimu za ripoti ya mwaka 2023 ya Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC),inaonesha kuwa taarifa za polisi katika kipindi cha miaka 5 (2018 hadi 2022) wanawake 2,438 waliuwawa sawa na wanawake 43 kila mwaka.
Anasema katika kipindi cha kuanzia Septemba 2022,wanawake 472 waliripoiwa kuuawa idadi ambayo ni sawa na wanawake 53 kila mwezi.
“Tafiti zinaonesha ukatili dhidi ya wanawake unaathari kubwa sana si tu kwa wanawake bali pia katika uchumi wa nchi na maendeleo kwa ujumla.”
“Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia inaonesha upotevu wa uzalishaji unaosababishwa na ukatili wa jinsia unaokadiriwa kuwa kati ya asilimia 1.2 ya pato la taifa la Brazil na Tanzania ni asilimia 2,”anasema Nsokolo.
Anasema wakati kauli mbiu ya mwaka 2023 katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia inasema Wekeza Kuzuia Ukatili wa Kijinsia,idadi ya watu duniani mwaka 2019 inaonesha takribani asilimia 35 ya wanawake wote wamekutana na aina nyingi za ukatili na udhalilishaji wa kingono katika maisha yao.
Mkurugenzi wa UTPC Kenneth Simbaya akizungumza na waandishi wa habari anasema ni wadau muhimu wanaopaswa kuhakikisha vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vinaripotiwa na kuibua vyanzo vinavyosababisha ukatili wa kijinsia ukiwemo wa wanaume,wanawake na watoto.
“Takwimu hizo za kidunia si dalili nzuri,kama nchi tunapaswa kutafuta suluhu ya kadhia hiyo kuhakikisha tunakuwa na jamii na kizazi salama kisicho na ukatili wa aina yoyote,”anasema.
Ester Joseph (si jina halisi) anasema licha ya baadhi ya wadau na wataalamu wa masuala ya jinsia kutoa elimu bado jamii inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukatili wa kijinsia,kimwili,kihisia na ukatili wa kiuchumi hivyo sio jukumu la Jeshi la Polisi pekee kupambana na changamoto hii bali jukumu hilo ni la kila mmoja kupaza sauti.
Anasema wananchi wote wanapaswa kuungana kupaza sauti wakati wote dhidi ya vitendo vya ukatili wa jinsi ikiwemo kutoa elimu katika jamii,kazi ambayo kwa kiwango kikubwa imenafanywa na wanaharakati na wadau mbalimbali ambao wanaunga mkono jitihada za serikali katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili.
“Kila mmoja wetu anapaswa kutofumbia macho vitendo hivyo vya ukatili maana bado vinagalipo katika jamii na vinaendelea huku kundi kubwa linaloathirika likiwa ni la watoto na wanawake ingawa pia wapo baadhi ya wanaume, hivyo wazazi wanao wajibu mkubwa kuhakikisha wanakilinda kizazi hiki,”anasema Gerald Machumu.
Mkuu wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Mwanza Faraja Mtinga anasema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha linawafikisha kwenye vyombo vya sheria wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Anatoa wito kwa wananchi kujitokeza kutoa taarifa kwenye madawati ya jinsia yameliyoanzishwa kushughulikia changamoto za matukio yanayohusiana na watu kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia huanza kila ifikapo Novemba 25 ya kila mwaka na kufikia kilele Desemba 10 ya kila mwaka ikilenga kutokomeza vitendo vya ukatili kwa jamii.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika