December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meneja wa Kitengo wa Shirika la Plan International Tanzania Mkoa wa Mwanza Dkt.Majani Rwambali akizungumza na Waandishi wa habari katika maadhimisho ya mtoto wa Afrika Duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo June 16 kila mwaka ambapo kwa Mkoa wa Mwanza yameadhimishwa June 17 yaliyoandaliwa na Shirika hilo.picha na Judith Ferdinand

Ukatili wa Jinsia kwa Watoto bado Tatizo

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

IMEELEZWA kuwa takwimu bado zinaonesha  matukio ya ukatili wa jinsia bado yapo kwa watoto hususani wa kike katika Mkoa wa Mwanza,hivyo wito umetolewa kwa maofisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Mkoa na Halmashauri kuimarisha  utoaji wa elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi na walezi.

Huku wazazi wakiwa karibu na watoto wao kwa kuhakikisha wanawapatia elimu ya afya ya uzazi,makuzi pamoja na elimu ya kujitambua itolewe mpaka shule za msingi, vijijini na Klabu katika shule za binafsi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Dkt.Severine Lalika aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Mongella katika maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Afrika Duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo June 16 kila mwaka, ambapo kwa  Mkoa wa Mwanza yamefanyika leo(jana June 17,2020) yaliyoandaliwa na Shirika la Plan International yenye kauli mbiu “Mifumo rafiki ya upatikanaji haki za mtoto, msingi imara ya kulinda haki zao”.

Dkt.Lalika amesema,elimu hiyo itolewe ili waelewe wajibu wao wa kulea watoto kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa wa kijinsia ambapo taarifa  kutoka Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza inasema mwaka 2019 jumla ya matukio ya ukatili ya kingono 420 kati ya hao wasichana 393 na wavulana 37.

Anasema,kati ya hayo mimba za wanafunzi 188,kubaka 148,kulawiti 39 na kufanya mapenzi na wanafunzi 34 huku mwaka 2020  katika kipindi cha Januari hadi Machi jumla ya matukio 232 yaliripotiwa huku wavulana wakiwa 17 na wasichana 219 na kati ya matukio hayo mimba za wanafunzi 143,kubaka 57 na kulawiti 17.

Aidha anasema,watoto wahimizwe kutumia vifaa vya kielektroniki kama vile simu,kompyuta  kwa usahihi kwa ajili ya kujifunzia huku wazazi na walezi wakielekezwa kusimamia matumizi ya vifaa hivyo kwa watoto wao ili kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vya ngono na ukatili mwingine wa mitandaoni.

” Usalama wa watoto ni muhimu wakati wote hivyo wakiwa nyumbani katika kipindi hiki kwenda kwenye maeneo yatakayohatarisha usalama wao huku mtoto anapaswa kutimiza waji wako wa kuwaheshimu wazazi,walimu na jamii kwa kufanyia kazi maelekezo unayopewa ili ulinde haki zako ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasisitiza umuhimu wa Serikali,wazazi,walezi na jamii kuwekeza katika mifumo mizuri  ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili aweze kukua katika ukamilifu wake,” anasema Dkt.Lalika.

Meneja wa Kitengo wa Shirika la Plan Internation Tanzania  Mkoa wa Mwanza, Dkt.Majani Rwambali anasema wametoa elimu na mafunzo ya kuwahamasisha vijana ambao yameleta hamasa kwa vijana kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili huku mipango na  rasimali zao wamezielekeza katika kumlinda na kumwendeleza mtoto na kutekeleza sheria zote za nchi ili kuweza kufikia malengo mbalimbali yaliyowekwa kwa ajili ya kusaidia na kumwendeleza mtoto huku mkakati uliopo ni utoaji wa elimu katika  sehemu mbalimbali za Mkoa wa Mwanza .

“Kwa nini idadi ya matukio yanaongezeka kwa sababu watoto wanaopata mimba ni wengi, baada ya kutoa elimu jamii imepata uelewa na ujasiri wa kutoa taarifa kwenye vyombo ambapo inawezekana huko nyuma kulikuwa na matukio mengi zaidi na watu hawakujua wapi pakuyasemea lakini sasa wanatambua haki zao,”anasema Dkt.Rwambali.

Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Aidath Ismail, anasema wazazi,walezi na jamii iwalinde watoto na kuwawekea muda maalumu wa kutumia vifaa vya kielektroniki huku watoto wote wakitumia mitandao hiyo kwa ajili ya kujifunzia na kuiendeleza nchi yetu na siyo kufanyia masuala mengine ambayo yanachangia ukatili.

Mjumbe wa Baraza la Watoto Mkoa wa Mwanza,  Swamweli Lucas anasema ukatili wa kingono kwa watoto ambapo kwa kipindi hiki watoto wa kiume wamejikuta wakilawitiwa kutokana na wazazi na jamii kutokuwa na utambuzi  wa masuala hayo pamoja na  ulinzi mfano anaweza kutokea mgeni wa kiume kaja kutembelea nyumbani kisha akaambiwa alale na mtoto huyo ambapo unakuta hawajui tabia yake hivyo kupelekea mtoto kufanyiwa ukatili huo na  unakuta ana uwezo wa kujieleza kama amefanyiwa kitendo hicho.

Mjumbe wa Baraza la Watoto Mkoa wa Mwanza, Mariam Daud anasema njia inayotakiwa kutumika kupunguza ukatili ni Serikali  kuhakikisha kuwa inatoa elimu ya masuala ya kujitambua kwa watoto kuanzia elimu ya msingi, vijijini ambao wanaathirika zaidi kutokana na kukosa sehemu ya kutoa taarifa dhidi ya ukatili hivvyo wadau kwa kushirikiana na Serikali ipeleke watu maeneo hayo ambao wataenda kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya kikatili.

Baadhi ya wajumbe walioshiriki maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Afrika Duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo June 16 kila mwaka ambapo Mkoani Mwanza yamefanyika June 17 mwaka huu na yameandaliwa na Shirika la Plan International wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dkt.Severine Lalika.picha na Judith Ferdinand

Hata hivyo Tanzania kama nchi nyingine barani Afrika watoto bado wanakabiliwa na changamoto ya vitendo vya ukatili wa aina mbalimbali ikiwa ni ubakaji,ulawiti,utumikishwaji wa watoto katika ajirahatarishi,ukeketaji,ndoa na mimba za utotoni huku takwimu za Jeshi la Polisi nchini zinaonyesha kuwa vitendo vya ukatili vinaendelea kuongezeka kutoka matukio 14,491 mwaka 2018 hadi matukio 15,680 mwaka 2019.

Huku Mikoa ya kipolisi iliyoongoza kuwa na takwimu za juu kwa mwaka 2019 ni Mkoa wa Tanga matukio 1,156,Mkoa wa Kipolisi Temeke 844,Mbeya 791 na Mwanza 758 huku matukio ya ukatili yaliyoongoza ni ubakaji matukio 6,506,mimba za wanafunzi 2,830 na ulawiti 1,405.