Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kuwaepusha watoto dhidi ya madhara ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ili kuepukana na ukatili mtandaoni ikiwemo wa ukatili wa kingono.
Mwanaidi ameyasema hayo leo tarehe 18/03/2022 alipokuwa akizindua Taarifa ya Utafiti kuhusu Hali ya ukatili Dhidi Ya Watoto Mtandaoni, uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo yote ya ulinzi kama ilivyoelekezwa katika Mikataba ya kikanda na Kimataifa kuhusu haki na Ustawi wa Mtoto ili kumlikdatoto na vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili mtandaoni.
“Tutaendelea kusimamia Sera na Sheria mbalimbali zinazomhusu Mtoto na kuandaa miongozo inayohitajika ili kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili” amesema Mhe. Mwanaidi.
Ameongeza kuwa amefarijika kupata taarifa ya hali ya ukatili wa kimtandao katika kipindi hiki ambapo tumeanza kushuhudia watoto wameanza kupata madhara yanayotokana na ukatili wa kimtandao nchini hivyo itasaidia kuongeza afua zaidi za kupambana na ukatili mtandaoni ambao unaonea kwa kasi.
“Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia matumizi makubwa ya vifaa vya kielektroniki hasa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo vifaa hivyo vimekuwa kiungo muhimu kwa ajili ya mawasiliano kwenye kuendesha vikao mbalimbali” amesema Mhe. Mwanaidi
Mwanaidi ameeleza kuwa taarifa ya utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto Mtandaoni uliofanyika mwaka 2018 na Mtaalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt Hezron Onditi inaonyesha kuwa asilimia 4 ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 walifanyiwa ukatili wa kingono ikiwemo kulazimishwa kutoa picha zao za utupu.
“Pamoja na faida nyingi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, tumeshuhudia matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yakihusisha zaidi kundi la watoto na vijana balehe” amesema Mhe. Mwanaidi
Akieleza lengo la utafiti huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Sebastian Kitiku amesema matumizi ya vifaa mbalimbali vya kielekroniki yamekuwa yakitumika kwa wingi, hivyo kumekuwa na changamoto ya kutaka kujua ukubwa wa tatizo hilo. Hivyo, Serikali kwa kishirikiana na wadau wakaona ni vema kufanya utafiti huo.
“Utafiti umetumia mbinu mbalimbali kama uchambuzi wa Sera na Sheria zilizopo Nchini ,Upitiaji wa nyaraka mbalimbali mitandaoni,Mahojiana na Watoto na Wazazi kwa ujumla Pamoja na Mikusanyiko mbalimbali kwa kushirikiana na ngazi za kata hadi mkoa.”amesema Kitiku.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto Nancy Kasembo ameshukuru kwa kushirikishwa kwao katika michakato inayowahusu watoto kwani ina manufaa kwao na kuiomba jamii kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto katika mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
“Watoto hawajui namna ya kutoa taarifa baada ya kufanyiwa ukatili,aidha bado kuna unyanyapaa dhidi ya wahanga wa ukatili hivyo kupelekea wahanga kutotoa taarifa”. amesema Nancy
Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Unicef Shalini Bahguna ameipongeza Serikali kwa kuweka juhudi za msingi za kupinga vikali ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hasa katika jitihadaz.a kupambana na ukatili mtandaoni.
Amesema Shirika hilo limejikita katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama na kuhakikisha watoto wanajengewa uwezo wa kujitambua ili kuepukana na ukatili wa mtandaoni na kuiomba Serikali kuendelea kutoa ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuondoa tatizo la Ukatili mitandaoni.
Baadhi ya wadau wakichangia umuhimu wa utafiti huo wamesema ni vema kuwekeza kwenye kuweka mbinu zinazozuia watoto kufanyiwa ukatili wa mitandaoni kabla haujatokea na hiyo ni kwa mbinu kama kuzuia na kuwakataza watoto kujihusisha na baadhi utumiaji wa mitandao kama watu wazima.
Aidha, wameiomba Serikali kuwajengea uwezo watoa huduma hususani kwenye madawati ya kijinsia na Polisi na kuwaasa wazazi na walezi kujadili masuala ya msingi yanayowahusu watoto wao ili kuwajengea ukaribu na watoto waweze kusema pale wanapofanyiwa ukatili.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best