April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ukamilishaji wa miradi ya maji kwa chanzo Cha ziwa Nyasa kuwa mkombozi kwa afya

Makala

‘’Tumechoka kuugua homa za matumbo kwa kunywa maji yasiyo salama,mchakato wa chanzo cha ziwa nyasa uharakishwe,tulinde afya zetu’’.

Na Israel Mwaisaka,Kyela

WANANCHI wa Tarafa zote mbili za Unyakyusa na Ntebela zilizopo wilayani Kyela mkoani Mbeya,wameiangukia Serikali wakihitaji miradi ya maji iharakishwe wajikwamue na kuugua homa za matumbo kwa kunywa maji yasiyo salama.

Asilimia kubwa ya wakazi wa Kyela hasa vijijini wanatumia maji ya visima vilivyochimbwa kienyeji ambavyo usalama wake kiafya ni mdogo huku maji ya bomba yakiwa ya shida hali inayopelekea waugue homa za matumbo.

Kwa wakazi waliopo Kyela mjini baadhi yao wamekuwa wakiyatibu maji kwa kuweka dawa katika visima na wale wasiokuwa na uelewa huo nao wameingia kwenye tatizo hilo la kuugua homa za matumbo hasa watoto wadogo.

Wilaya ya Kyela yenye kata 33 ikiwa na Tarafa mbili,Ntebela Kyela vijijini na Unyakyusa Kyela mjini ikiwa na vitongoji 405 na vijiji 99 huku ikiwa na idadi ya watu 266,426 kwa sensa ya mwaka 2022.

Wakazi hao wamekuwa wakitoa kero mara kwa mara kupitia mikutano ya hadhara pindi viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri wenye dhamana ya maji wanapozungumza nao.

Katika Sekta za miundombinu yaani barabara,madaraja na makaravati baadhi ya maeneo,umeme,Elimu na Afya wilaya ya Kyela ipo vizuri tatizo kubwa lililosalia ni upatikanaji wa maji safi na salama.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa Tarafa hizo wanasema wana kila sababu ya kuishukuru serikali kwa kuing’arisha wilaya kwa kuwajengea miradi mikubwa na midogo wakidai ombi lao kuu kwa sasa wanahitaji maji.

Salome Mwafyuma mkazi wa Ipinda tarafa ya Ntebela,anasema kwa miaka ya hivi karibuni Tarafa hiyo imejengewa miradi mingi karibu ya idara zote isipokuwa miradi ya maji bado ni changamoto kwa baadhi ya maeneo.

Anasema wananchi wanaoishi vijijini wamekuwa wakitumia maji ya kwenye mito kwa shughuri mbalimbali ikiwemo kunywa ambayo si salama na wengi wao wamekuwa wakiugua homa za matumbo huku akiiomba serikali imalize changamoto hiyo.

Nae Samwel Mwaisumo mkazi wa Bondeni Tarafa ya Unyakyusa,anasema Kyela imekuwa ni moja ya wilaya nchini zinazopaa kimaendeleo kwani miradi yote ipo vizuri lakini changamoto iliyopo ni ukosefu wa maji safi na salama.

Anasema wamekuwa wakiiona miradi ikijengwa kwa muda mrefu bila kukamilika, hivyo wameiomba serikali kukamilisha miradi hiyo ili waondokane na kunywa maji ya visima ambayo siyo safi na salama.

‘’Tumechoka kuugua homa za matumbo kwa kunywa maji yasiyo salama,mchakato wa chanzo cha ziwa nyasa uharakishwe,tulinde afya zetu’’,anasema Mwaisumo.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji Kyela –Kasumulu, Mhandisi Raphael Francis anasema ni kweli kuna changamoto hiyo lakini serikali imeleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya maji.

Anasema kuna mradi mkubwa wa Bilion 4.7 unajengwa chanzo ni mto Mbambo halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe ambao upo asilimia 70 na maji tayari yamefika.

Anasema kazi iliyopo ni kutanua mtandao wa maji kwenda pembezoni mwa mji ambayo ni kusambaza mabomba kutoka bomba kubwa ambapo wamesambaza kilometa 30 na kazi bado inaendelea.

Anasema pia wameweka mpango wa kujenga tenki la maji la ujazo wa lita Milioni 2 ambapo wapo katika hatua ya manunuzi,ikiwemo kufunga Dira 2,000 za maji.

Anasema katika mamlaka ya mji mdogo wa Kyela hali ya upatikanaji wa maji upo asilimia 54 na kwamba mradi huo ukikamilika watafikia asilimia 83 hali ambayo itapunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Anasema mbali na mradi huo,pia kuna miradi miwili ambayo ni mradi wa maji Ipinda uliogharimu shilingi Milioni 697 utekelezaji wake upo asilimia 90, na mradi wa Bondeni uliogharimu shilingi Milioni 300 umekamilika kwa asilimia 100.

Kutokana na hali hiyo, Mhandisi Francis amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati serikali inaendelea kutekeleza miradi hiyo itakayokuwa suluhisho la tatizo la maji ndani ya mamlaka ya mji wa Kyela.

Nae Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Kyela mkoani Mbeya,Mhandisi Tanu Deule,anasema ni kweli wananchi wanahaki ya kuiharakisha miradi kutokana na maji yaliyopo kuto tosheleza.

Anasema kutokana na hilo,serikali ipo kwenye mkakati wa muda mrefu wa kumaliza kabisa changamoto hiyo kwa kutumia chanzo cha Ziwa Nyasa ambapo upembuzi yakinifu unafanyika kwa gharama ya shilingi Milioni 321,na kazi ipo asilimia 90.

Anasema baada ya kukamilika kazi hiyo ya usanifu,serikali itatangaza tenda kumpata Mzabuni na gharama halisi ya utekelezaji wa mradi itajulikana baada ya Mzabuni kupatikana.

Mbali na mkakati huo wa muda mrefu pia anasema ipo mikakati ya muda mfupi ya kuboresha miradi kwa kuweka mabomba makubwa ili iweze kusaidia angalau kwa miaka 20 ijayo baada ya kubaini vyanzo hivyo vinayo maji kiasi cha kuhudumia kwa miaka 20 ijayo.

Anasema katika Chanzo cha Mwega shilingi Bilioni 8 zinatumika kuboresha mradi wa Ngana Group kwa kuweka bomba kubwa,pia upo mradi wa Shinyanga Group uliotengewa Bilioni 1.7 za maboresho, ambapo million 960 zimeshatumika kulaza mabomba tayari.

Aidha Mhandisi Deule,anasema mradi wa maji Makwale nao unaboreshwa kwa kujengwa inteki mpya na kuwekewa mabomba makubwa ukitumia chanzo cha maji mto Mwalisi utakao tumia Shilingi Milioni 160.

Na pia anasema Chem chem ya Mapumba iliyopo Kibole Busokelo unaohudumia mradi wa Ngamanga Group inaboreshwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 150.

Sambamba na maboresho hayo anasema wilaya ya Kyela ni miongoni mwa wilaya iliyonufaika na mradi wa visima 900 ambapo serikali ilitoa fedha Milioni 530 zilitolewa kwa kila jimbo nchini kuchimba visima 5.

Anasema kwa sasa wilaya ya Kyela inatumia maji kutoka vyanzo vya mto Mwega (Ileje) Mwalisi (Kisyosyo),Kigange (Rungwe),Mwalalo (Matema),Nsebele (Ikombe),Saga (Mababu) na mto Itinginya (Lema) na kupelekea hali ya upatikanaji wa maji kuwa asilimia 65.

Anasema wameshindwa kuitumia mito mikubwa ambayo ni Kiwira, Songwe,Mbaka na Lufilyo kwa kuwa vyanzo vya maji vina tope na kemikali nyingi zinazohitaji matibabu.

Anasema serikali imedhamiria kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya mradi mkubwa wa chanzo cha ziwa Nyasa utakapo kamilika.

Anasema mradi huo mkubwa wa kutumia Ziwa Nyasa utakuwa na sifa kuu tatu ambazo ni:- (a)-utakuwa mradi mkubwa na wa kihistoria,(b)-utatumia nishati ya kusukuma maji kwenda kwenye matenki,(c)-Utahitaji madawa ya kutibu maji kwa ajili ya usalama.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kyela Baraka Mwamengo,anasema ameridhishwa na mipango hiyo ya serikali ya kumaliza tatizo la maji katika jimbo hilo.

Anasema kwa sasa yupo Bungeni kwenye vikao vya bajeti vinavyoendelea na anaendelea pia kuupambania mradi huo mkubwa wa Ziwa Nyasa pamoja na miradi inayoendelea kujengwa hivi sasa iweze kukamilika.


Show quoted text