Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Balozi. Dkt. Pindi Chana amezindua ujenzi wa mradi wa majengo ya Idara ya MpigaChapa Mkuu wa Serikali utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 2.5 hadi kukamilika kwake majengo yatakayotumika kuzalisha nyaraka za Serikali.
Waziri Pindi amesema hayo jana wakati wa hafla ya kukabidhi eneo la ujezi huo lenye ukubwa wa mita za mraba 47,214 kwa mkandarasi wa ujenzi huo Hainan International Limited yatakayojengwa Kisasa Jijini Dodoma ambapo alisema kulingana na mkataba wa ujenzi mradi huo unatakiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi 12.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 Ofisi ya Waziri Mkuu ilidhinishiwa fedha za maendeleo ya ndani shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa majengo ya MpigaChapa mkuu wa serikali.
“Ujenzi wa majengo haya utahusisha ujenzi wa jengo la kiwanda, jengo la Ofisi, jengo la Canteen, ujenzi wa duka la vitabu la serikali na ujenzi wa uzio hivyo mradi unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha ambapo mwaka wa fedha 2021/2022 ujenzi utakaofanyika ni wa jengo la kiwanda kwa gharama za shilingi bilioni 2.29,”amesema Pindi.
Akizungumzia kuhusu Mshauri Elekezi amefafanua kuwa ni kampuni ya Aru Built Environment Company Limited kwa gharama za shilingi milioni 389.5 zikijumuisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Aidha amemtaka mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa mkataba unavyoelekeza hatua ambayo itasaidia kufanyika kwa shughuli za uzalishaji wa nyaraka muhimu za Serikali kama ilivyokusudiwa huku akisisitiza Mshauri Elekezi kuhakikisha anasimamia mradi kwa ubora na viwango kwa mujibu wa mkataba.
“Utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati wa malengo haya ya maendeleo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu utafanyika chini ya mkataba yaani miezi 12 na mkandarasi ndiye mtekelezaji wa mradi huu azingatie maelekezo na miongozo ya ujenzi wa mradi kwa ukamilifu,”amefafanua Waziri Pindi.
“Muda wa maandalizi ya kuanza kazi ni wiki mbili kuanzia tarehe Machi 25,2022 kuanza rasmi ni April 08,2022 na kukabidhiwa mradi ni ifikapo Machi 07,2023,”amehimiza.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Hainan International Limited kutoka Nchi ya China, Mhandisi Ding Wu aliahidi atahakikisha watanzania wanapewa kipaumbele cha ajira katika mradi huo ili kukuza uchumi wao na kuchangia pato la Taifa.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuamini na kutupa kazi hii kama Waziri alivyotuelekeza sisi tuna uhakika hii kazi tutamaliza ndani ya muda ikiwa na ubora ambao Serikali inataka kulingana na fedha iliyotolewa na kwa sisi mipango yetu hatutaki kazi ifike miezi 12 ndani ya miezi 10 tutakuwa tumemaliza na kukabidhi,”amemshukuru Mhandisi Wu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa