Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online
KWA kubofya namba *106# katika simu, yako utaweza kuhakiki usajili wa namba yako ya simu, pamoja na kutazama idadi ya namba za simu zilizosajiliwa kwa namba yako ya kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Baada ya kupiga namba *106# utapewa chaguzi kadhaa namba 1 hadi 5, ukichagua namba 3 utaweza kutazama idadi ya namba za simu zilizosajiliwa kwa namba yako ya Uraia iliotolewa na NIDA.
Mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi akibaini namba za ziada, zaidi ya zilizosajiliwa kwa namba yake ya NIDA, atatakiwa kuchukua hatua.
Hatua za kuchukuliwa ni pamoja na kufika katika dawati la huduma kwa wateja ili kutoa taarifa itakayowezesha kufutwa kwa namba ambazo hakuzitambua; hatua hii ni muhimu kwa kuwa inamlinda mtumiaji wa huduma za mawasiliano dhidi ya matumizi mabaya ya namba hizo yakiwemo matumizi yanayohusisha uhalifu.
Ni muhimu mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu kuhakikisha anachukua tahadhari wakati wa usajili wa laini yake ya simu kwa wakala kwa kuhakikisha mtoa huduma ya kusajili na kuhakiki, anasajili namba husika tu. Miongoni mwa mambo ya kuzingatia wakati wa usajili wa laini ya simu kwa alama ya kidole ni kuepuka kurudiwa mara kwa mara zoezi la uchukuaji wa alama za vidole.
Hatua nyingine muhimu ni kuhakikisha wakala anaesajili na kuhakiki laini za simu anacho kitambulisho kutoka kwa kampuni anayoiwakilisha. Hatua hizi ni muhimu kuchukuliwa na mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu wakati anaposajili na kuhakiki laini yake ya simu ili kuepuka ulaghai unaotendwa na baadhi ya mawakala wasio waaminifu wakati wa zoezi la usajili na uhakiki.
Baadhi ya mawakala wasio waaminifu husajili laini nyingine za wateja kwa kutumia utambulisho wa namba yake ya kitambulisho cha utaifa mara ukomo wa idadi ya laini Tano kwa kila mtandao inapofikia wakala huanza kusajili laini za ziada kwa kutumia namba za wateja wasiotambua ulaghai huo ili aongeze wigo wa faida kupitia idadi kubwa ya wateja aliowasajili.
Ili kumfanya mteja asigundue kwa urahisi kuwa namba yake ya NIDA imesajili namba nyingi, huanza kwa kuihakiki na kuichagua namba hiyo kuwa namba kuu kisha nyingine zote kuzifanya kuwa namba za ziada.
Baadhi ya Mawakala hao hufanya kosa hilo licha ya kufahamu ni kutenda kinyume na Sheria, hivyo katika kudhibiti uhalifu huo ni muhimu kila mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kuhakiki idadi ya laini za simu zilizosajiliwa kwa kutumia namba yake ya Kitambulisho cha Taifa inayotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Uhakiki wa laini za simu unaofanywa na mtumiaji mara kwa mara huwezesha kubaini namba za simu ambazo zimefanana majina ya usajili na ambazo hazitambui hivyo kurahisisha hatua za kumbainisha wakala alietenda kosa hilo ili hatua zaidi za ki-nidhamu zichukuliwe dhidi ya mhusika.
Mbinu inayotumiwa zaidi na baadhi ya mawakala wasio waaminifu wakati wa usajili wa laini ya simu kwa njia ya bayometria ni kumtaka mteja kurudia mara kadhaa zoezi la kuweka alama ya kidole ili kuthibitisha usajili; mawakala hao hubainisha kuwa zoezi la kuchukua alama za vidole lirudiwe mara kadhaa kwa madai kuwa hatua ya awali haikufanikiwa, wakati huo alama hizo huhifadhiwa ili zitumike kusajili laini za ziada.
Ni muhimu kwa mtumiaji huduma anaehitaji kusajili laini yake kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha anaweka alama ya kidole mara moja tu na ikiwa ipo haja ya zoezi kurudiwa ni muhimu wakala akatoa hakikisho kwamba zoezi hilo halilengi kuchukua alama ya kidole mara mbili na inabidi kuthibitisha; ni muhimu mpatiwa huduma akajiridhisha.
Baadhi ya Mawakala mtaani huziuza laini za simu zilizosajiliwa kwa utambulisho wa watumiaji wengine wakiziita “take away”, ni muhimu mtumiaji wa huduma za mawasiliano kuepuka kununua laini hizo kwani kufanya hivyo ni kutenda kosa.
Uhalifu wa aina hii, umekuwa ni mtaji kwa baadhi ya mawakala ambao hutumia alama hizo kusajili laini za simu zaidi ya mara moja, ili baadae kuziuza kwa watu wenye uhitaji wa laini za simu zilizosajiliwa kwa matumizi binafsi; matokeo yake laini hizo hutumika kwa matumizi ya kawaida na matumizi yanayohusisha vitendo vya jinai kama vile wizi wa mtandaoni na uhalifu mwingine.
Hivyo kutokuhakiki laini ya simu kunaweza kumweka mtumiaji wa huduma za mawasiliano matatani ikiwa laini za simu zilizosajiliwa bila kufahamu zitatumika kutenda jinai kwa makossa mbalimbali kama vile utapeli wa mtandaoni, kubagaza, kutusi, kutishia nakadhalika.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitoa muongozo wa usajili wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole (kibiometria) kwa malengo manne ikiwamo kuimarisha na kuendeleza juhudi za kupambana na ulaghai katika miamala na huduma za kielektroniki pamoja na kuhakikisha kuwa watoa huduma wanakuwa na utaratibu unaofanana wa kusajili na kuhakiki laini katika njia ya kibiometria.
Mtoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi, anawajibika kisheria kumlinda mtumiaji wa huduma hizo, dhidi ya uhalifu mtaandaoni kama Wizi na Ulaghai.
Uhakiki wa namba za simu una madhumuni ya kumlinda mtumiaji dhidi ya vitendo visivyofaa vinavyofanywa na watumiaji wengine mfano kutuma ujumbe wa vitisho, matusi na matendo ya kihalifu.
Baadhi ya watumiaji huduma za mtandao wa simu wamekuwa wakikwepa kusajili laini za simu kwa sababu mbalimbali, baadhi yao wamekuwa wakikwepa usajili ili wasiweze kubainishwa kwa matendo ya jinai wanayotenda kwenye mtandao hivyo hutumia mbinu ya kununua laini za simu zilizosajiliwa tayari kwa utambulisho wa watumiaji wengine wa huduma za mawasiliano.
Usajili na Uhakiki wa laini ya simu ni zoezi muhimu kwa kuzingatia kuwa linawezesha mtumiaji wa huduma za mawasiliano kutotumia simu yake kutenda jinai. Kwa nini utumie biometria ili kusajili laini yako ya simu.
Jibu lake ni kwamba tabia za kibaolojia ni za kipekee na haziwezi kughushiwa kirahisi, teknolojia hiyo inaondoa uwezekano wa wizi wa kitambulisho na utambulisho wa mhusika na mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu. Faida hii inafanya teknolojia ya biometria kuwa njia rahisi na salama ya kumtambua mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu.
Pamoja na hakikisho hili la usalama bado baadhi ya watu wasio waaminifu wanavumbua njia mbadala za utapeli ambazo mtumiaji wa huduma za simu anaweza kuzishinda na kuhakikisha huduma anayopata inakuwa salama kwa kuhakiki laini yake ya simu na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na watoa huduma pamoja na Mamlaka inayosimamia mawasiliano.
Hima hakiki laini yako ya simu ili uwe salama kwa kubofya *106# kisha fuata maelekezo kuhakiki namba zako zilizosajiliwa kwa kitambulisho cha Taifa.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika